Hamad Rashid aipiga kijembe CUF tuhuma za kuitwa msaliti

10Apr 2016
Rahma Suleiman
Nipashe Jumapili
Hamad Rashid aipiga kijembe CUF tuhuma za kuitwa msaliti
  • *Amshukuru Dk. Shein kumkumbuka katika uteuzi

WAZIRI wa Kilimo na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Hamad Rashid Mohamed, amemshukuru Rais Ali Mohamed Shein kwa kumteua kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na baadaye waziri huku akirusha kombora kwa Chama cha Wananchi (CUF)

HAMAD RASHID

kwa kudai kuwa kimewasaliti Wazanzibari kwa kususia uchaguzi wa marudio visiwani humo uliofanyika Machi 20, 2016.

Hamad aliyegombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ADC, aliteuliwa kuwa waziri katika serikali ya Rais Shein jana, akiwa ni miongoni mwa wapinzani wawili waliopata nafasi hiyo kutoka nje ya Chama Cha Mapinduzi. Mwingine ni Juma Ali Khatib ambaye pia aligombea urais kupitia TADEA.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe siku moja kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri, Hamad aliyekuwa akiepuka kuitaja CUF moja kwa moja, alisema chama chochote kilichosusia uchaguzi mkuu wa marudio ndicho kinachostahili jina la ‘usaliti’ kwa sababu uamuzi huo (wa kususia) ndiyo uliokiwezesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuibuka na ushindi wa kishindo katika nafasi ya urais na pia kuzoa viti vyote vya uwakilishi.

Katika matokeo ya uchaguzi mkuu wa marudio visiwani humo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, yalionyesha kuwa Dk. Shein wa CCM ametetea nafasi yake ya urais kwa kuibuka na ushindi wa zaidi ya asilimia 91 ya kura zilizopigwa.

Akieleza zaidi, Hamad alisema wale waliosusia uchaguzi huo wa marudio ndiyo wasaliti kwa sababu kwa kiasi kikubwa ndiyo walioiwezesha CCM kuibuka na ushindi kwa kupata kura nyingi katika kila jimbo.

“Mwenye akili apime. Hapa msaliti ni nani… yule aliyewaachia CCM kuchukua majimbo yote na kuhalalisha mfumo wa chama kimoja au wale walioshiriki ili kutimiza wajibu wao wa Kidemokrasia?” alihoji Hamad na kuongeza:

“Mimi dhamira yangu ilikuwa niwe Rais wa Zanzibar au kushika nafasi ya umakamu wa kwanza wa Rais… lakini kura hazikutosha. Na kwakuwa haikuwezekana, nasema cheo chochote nitakachojaaliwa nitakitumia kuwatumikia wananchi kwa moyo wangu wote bila ya kujali itikadi, rangi, dini au kabila.

” Hamad alisema uamuzi aliouchukua Dk. Shein wa kumteua yeye (kutoka ADC) kuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi ni wa hekima na busara za hali ya juu na hivyo anamshukuru.

Aidha, Hamad aliwashukuru pia Wazanzibar waliompigia kura katika uchaguzi wa marudio na kumuwezesha kupata asilimia takriban tatu ya kura zilizopigwa, huku akiahidi kuwa daima chama chake hakitasusia chaguzi kwa sababu ndiyo njia pekee iliyopo katika kushika dola na kwamba, pia ndiyo msingi wa kuanzishwa kwa chama chochote cha siasa duniani.

“Nitaendelea kupambana katika demokrasia. Nawahakikishia wanachama wa ADC kuwa nitawatumikia kwa nguvu zote katika kukijenga chama na kuhakikisha kuwa tunashika dola katika uchaguzi wa mwaka 2020,” alisema Hamad.

ATAKA SHEIN AUNGWE MKONO

Hamad alisema Dk. Shein amekuwa mzalendo wa kweli na mara zote amekuwa akijielekeza katika mambo ya msingi kwa maendeleo ya Wazanzibar na hivyo, kuna umuhimu kwa kila Mzanzibari kumuunga mkono ili kupeleka mbele gurudumu la maendeleo.

“Raisi (Dk. Shein) ametumia uzalendo wa hali ya juu katika kusimamia mambo ya maendeleo nchini kwani bado lipo tatizo katika kuifanya siasa kuwa ndiyo kila kitu. Huwezi kupata maendeleo katika mazingira hayo na kufikia uchumi unaotakiwa.

Hivyo ni jambo la msingi kuona maendeleo yakisimamiwa kwa nguvu zote,” alisema. Alisema uchaguzi umeshapita na hivyo ni vyema kwa kila Mzanzibari kuondokana na siasa za chuki na badala yake kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo.

Aidha, alisema ni vizuri kuhakikisha kuwa mtu yeyote anayevunja sheria au kuvuruga amani ya nchi anachukuliwa hatua zinazostahili kwa sababu mambo hayo huchangia kukwamisha maendeleo ya nchi.

KUTENGWA KIMATAIFA

Akizungumzia kuhusu uamuzi wa baadhi ya wahisani kusitisha misaada yao ya maendeleo kwa Tanzania kutokana na kile kilichotokea katika uchaguzi wa Zanzibar, Hamad anasema Zanzibar siyo masikini kiasi cha kutegemea misaada kwa sababu ina rasilimali nyingi, hasa zinazohusiana na uvuvi. Aliwataka Wazanzibari kuondokana na fikra za kutegemea misaada kwa kudhani kuwa ndiyo itakayoikwamua nchi yao.

“Zanzibar inapaswa kutegemea rasilimali zilizopo zikiwamo za mafuta na gesi,” alisema Hamad. Alisema siyo jambo la busara kushinikiza mambo wanayoyataka wahisani yatekelezwe ili kupatiwa misaada.

AKANA KUTUMIWA NA CCM

Hamad alisema kuteuliwa kwake kuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi haimaanishi kuwa yeye ni kibaraka wa CCM kama wanavyodai baadhi ya watu, hasa kwa kutambua ukweli kwamba hiyo siyo mara ya kwanza kwa yeye kupata nafasi za uteuzi wa rais.

Alisema hata mwaka 2001, wakati wa utawala wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, aliteuliwa na Rais (Mkapa) kuwa mbunge katika lililokuwa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

NGUVU YA BARAZA LA WAWAKILISHI

Kuhusiana na nguvu ya Baraza la Wawakilishi lililojaa wajumbe wengi kutoka CCM, Hamad anasema hadhani kwamba hiyo ni sababu kwa baraza hilo kuwa dhaifu kiutendaji.

“Hoja ni ubora wa mtu na siyo wingi wa wajumbe. Naamini kama nilivyoweza kuongoza Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndivyo pia nitakavyokuwa katika Baraza la Wawakilishi. Licha ya kuwapo kwa wajumbe watatu kutoka upinzani ndani ya baraza hili, bado tuna fursa ya kufanya mambo makubwa kwa manufaa ya Zanzibar,” alisema Hamad.

Akieleza zaidi, Hamad alisema kuwa katika Bunge la Tisa, alikuwa akiongoza kambi ya upinzani na walikuwa wachache wakati CCM ilikuwa na asilimia zaidi ya 80 ya wabunge lakini bado alifanya vizuri.

Alisema haoni sababu kwa wajumbe wa baraza la wawakilishi kutoka upinzani kushindwa kufanya vizuri katika baraza lenye wajumbe 85 wakati yeye alishajiwekea rekodi nzuri ya utendaji wakati akiwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema jambo muhimu ambalo litamuwezesha yeye na wenzake kufanya vizuri ndani ya baraza hilo ni nia na uwezo wa kuwatumikia wananchia, sifa ambazo yeye anaamini zote amejaaliwa kuwa nazo.

MATARAJIO

KISIASA Alisema matarajio yake katika chaguzi zijazo, hasa wa mwaka 2020, ni kuwa Rais wa Zanzibar kupitia chama cha ADC kwa sababu bado hajakata tamaa maana hakuna chama cha siasa chenye hatimiliki ya kushika dola visiwani Zanzibar.

ILIVYOKUWA UCHAGUZI MARUDIO

Katika matokeo ya uchaguzi wa marudio, Jecha alitangaza kuwa waliokuwa wagombea wa uwakilishi kupitia CCM walishinda nafasi zote, Unguja na Pemba na hivyo kukipa fursa chama tawala kuwa kinara pekee kwa mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

Kabla ya hapo, CCM ilikuwa ikikaliwa kooni na CUF katika kila uchaguzi na kugawana majimbo kwa uwiano unaokaribiana. Aidha, tangu mwaka 1995, CCM haijawahi kuwa na nguvu kisiwani Pemba na kabla ya uchaguzi wa Machi 20, majimbo yote ya Pemba yalikuwa chini ya CUF.

Hata hivyo, mchuano mkali uliozoleka baina ya CCM na CUF haukuwapo katika uchaguzi wa marudio baada ya CUF kususia na kuwataka wafuasi wake wasishiriki uchaguzi huo waliodai kuwa siyo halali bali ulikuwa na lengo la kuibeba CCM iliyoelekea kuanguka katika uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25 kabla Jecha hajafuta matokeo yake yote.

CUF waligomea uchaguzi wa marudio kwa madai kuwa uchaguzi wa awali haukuwa na kasoro yoyote kubwa kiasi cha kustahili kufutwa na kwamba, hata ripoti za waangalizi wote wa uchaguzi huo kutoka nje na ndani ya nchi zinaeleza kuwa ulikuwa ‘huru na wa haki’.

CUF Waliitaka ZEC iendelee na majumuisho ya kura za Oktoba 25 na kumtangaza mshindi halali, wakimiani kuwa mgombea wao, Maalim Seif Shariff Hamad alikuwa akielekea kushinda kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa kutokana na kile walichodai kuwa ni nakala za matokeo walizopata kutoka kwa mawakala wao kwenye kila kituo cha uhaguzi baada ya kusainiwa na mawakala wa kila chama kilichoshiriki.

Hata hivyo, ADC iliyomsimamisha Hamad Rashid kuwa mgombea wao wa urais wa Zanzibar, haikukubaliana na CUF na vyama vingine kadhaa vya upinzani vilivyosusia uchaguzi huo, bali kushiriki kama walivyofanya CCM.