Agness Masogange afariki Dunia

21Apr 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Agness Masogange afariki Dunia

MSANII maarufu nchini aliyepata umaarufu wa kupamba video za wasanii wa muziki wa bongo fleva, Agness Gerrad 'Masogange' amefariki dunia jana jijini Dar es Salaam.

Agness Gerrad 'Masogange'.

Masogange, alifariki kwenye hospiatali ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge alipokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa za kufariki kwake zilianza kuzagaa kwenye mitandao jana jioni huku wasanii maarufu nchini wakiandika kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii juu ya kifo cha msanii huyo.

Dokta Kihama Ngoma aliyekuwa akimtibu Masogange aliwathibitishia waandishi wa habari kufariki kwa msanii huyo maarufu.

Chanzo cha kifo cha msanii bado hakijawa wazi huku wadau wengi wa sanaa wakishtushwa na taarifa hizo.Wasanii wamlilia

Baadhi ya wasanii walionyesha hisia zao kwenye kurusa zao za mitandao ya kijamii kila mmoja akionyesha kuguswa na kifo cha ghafla cha msanii huyo, Steve  Nyerere kwenye ukurusa wake aliandika "Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo chako makubwa".

Aunt Ezekiel aliandika "Jamani jamani.., nimeogopa mimi, nimeshtuka mimi R.I.P Masogande.

Kwa upande wake, msanii mkongwe nchini, Monalisa aliandika "Gone to Soon (umeondoka mapema).., mimi simaini".

Masogange alianza kupata umaarufu baada ya kutumika kwenye video ya msanii wa bongofleva, Bere 9 inayoitwa 'Masogange' ambapo jina hilo likaibuka kuwa jina la utani la Agness.