Mganda huyo alisema anashangaa kuona mechi za Ligi Kuu zinazowahusisha wapinzani wake wakuu katika mbio za ubingwa msimu huu, Yanga na Azam FC, zikipigwa kalenda pasi na sababu kuntu.
Na utaratibu huo usiofaa umeifanya Simba kuwa mechi tatu mbele ya Wanajangwani na Wanalambalamba ambao pia wako pointi saba nyuma ya timu hiyo ya Msimbazi.
"Utaratibu huu nimeukuta Tanzania tu, tumeona timu inacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na inacheza pia mechi zake za ligi ya nyumbani," alisema. "Lakini hapa (Tanzania) timu inaacha kucheza mechi za ligi ya nyumbani eti kisa inacheza mechi za Afrika."
Binafsi namuunga mkono Mayanja kutokana na ukweli kwamba TFF imekuwa ikisigina taratibu na kanuni za soka na kuonekana dhahiri kuwa na upendeleo kwa baadhi ya timu.
Na hali inazidi kuwa mbaya zaidi katika soka la Tanzania Bara tangu kuingia madarakani kwa rais wa TFF, Jamal Malinzi mwishoni mwa mwaka 2013. TFF ya Malinzi, kwa mfano, iliiruhusu Azam FC kukacha ratiba ya ligi ya Bara kwenda kushiriki mashindano ya 'ndondo' nchini Zambia miezi miwili iliyopita.
Baada ya uamuzi huo kupondwa vikali na wadau wa soka nchini, Malinzi alijitokeza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuomba radhi kwa udhaifu huo huku akiahidi kutorudia makosa, lakini vurugu za kupangua ovyo ratiba ya mechi za Ligi Kuu zinaendelea.
Kinachoshangaza zaidi, wakati Yanga na Azam FC wako nyuma kwa mechi mbili za Ligi Kuu, TFF juzi iliruhusu mechi tatu za ligi ya Bara kuchezwa, tena katika muda sawa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na APR ya Rwanda.
Jana pia kulikuwa na mechi ya Ligi Kuu kati ya African Sports na Tanzania Prisons ilhali Dar es Salaam Azam FC walikuwa wenyeji wa Bidvest Wits ya Afrika Kusini katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Juni 8-12 mwaka jana, Nipashe ilichapisha ripoti maalum iliyofichua mbinu mbalimbali zinazotumika kupanga matokeo ya mechi za ligi za soka nchini, upanguaji wa ovyo wa ratiba na utitiri wa mechi za viporo ukiwa miongoni mwa mbinu hizo zinazodimimiza soka la Tanzania.
Hainiingii akilini kuona TFF ya Malinzi yuleyule aliyesimama mbele ya waandishi wa habari mwaka jana na kutamba kuwa atambana na wapangaji matokeo, ameruhusu kufinyangwa kwa ratiba ya mechi za ligi ya Bara.
Ndiyo maana naiona TFF kama taasisi inayopaswa kuingizwa kwenye utaratibu wa 'kutumbua majipu' unaosimamiwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli.
Lakini shughuli za shirikisho hili hazipaswi kuingiliwa na mamlaka za nchi, kwa mujibu wa taratibu za Shirikisho la Soka la Kimataifa. Watendaji wakuu wa TFF wakiongozwa na Malinzi, wanapaswa kubadilika na 'kujitumbua' wenyewe kwa manufaa ya soka la Tanzania na maendeleo ya taifa kwa ujumla.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








