Baadhi walidhani Yanga ingepata ushindi mkubwa Taifa kana kwamba inacheza na timu dhaifu ya Ligi Kuu.
Yote hii ilitokana na ushindi wa mabao 2-1 ilioupata ugenini.Mwenye macho aliona na mwenye masikio alisikia. Yanga ilibanwa kila kona.
Kwa mara kwanza baada ya miaka mingi, nimeshuhudia wachezaji wa Yanga wakionekana kuchoka. Walikata pumzi.
Walikutana na timu iliyokuwa inacheza soka la kushambulia na kutanua uwanja muda wote wa mchezo.
Ilifika wakati mashabiki wa Yanga waliokuwa uwanjani walikuwa wanaombea mpira umalizike na si kuomba dakika ziongezwe ili magoli yaongezeke.
Mashabiki walionekana kushangilia pale mabeki wa Yanga walipokuwa wakiokoa na si kushambulia.
Kila dakika zilivyozidi kusonga mbele zilionekana ni hatari zaidi kwa Yanga na si APR.
Kocha wa APR Nizar Khanfir raia wa Tunisia alisema kuwa kilichowabeba zaidi Yanga ni matokeo mazuri ya ugenini, vinginevyo hali ingekuwa mbaya kwao.
Nakubalina na kocha huyo ambaye wakati anaichukua hadi anacheza mechi dhidi ya Yanga alikuwa na wiki moja tu.
Kocha wa Yanga Hans van Der Pluijm alikiri hali ilikuwa mbaya na kutoacha kuwasifia vijana wa APR kuwa wanatandaza kandanda la uhakika na hii ni kwa sababu wengi wao wamechukulia kutoka kwenye 'akademi'.
Kwa mtazamo wangu, kilichowaangusa zaidi APR ni kwamba pamoja na kuwa na vijana kwenye vipaji, lakini wengi wao bado ni vijana na hawana uzoefu na mechi za kimataifa.
Pia walionekana kucheza soka la kishule zaidi. Katika mechi ya juzi kama wachezaji wale wangekuwa ni wazoefu, hali ingekuwa mbaya zaidi kwa wawakilishi wetu.
Hii ni ishara kuwa michuano ya Ligi ya Mabingwa si lelemama. Ni michuano migumu.
Na hii ni raundi ya kwanza tu, bado kuna raundi nyingine ya pili ambayo Yanga inakwenda kucheza.
Tayari timu inayocheza dhidi ya Yanga inajulikana. Nayo ni Al Ahly ya Misri, mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo.
Timu hiyo iliifunga Libolo ya Angola mabao 2-0 nchini Misri baada ya sare ya bila kufungana nchini Angola.
Azam ambayo ilipata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Bidvest ya Afrika Kusini, inatarajia kupambana na Esperance kama ikilinda ushindi wake nyumbani.
Mechi kati ya Yanga dhidi ya APR ni kengele ya hatari kwa wawakilishi wetu kuwa kila hatua inayopiga sasa ni ngumu, hivyo inabidi kujipanga.
Yanga na Azam zikumbuke kuwa Al Ahly na Esperance ni timu ambazo kwao kuingia makundi ni jambo la kawaida, hivyo zinahitajika juhudi na maandalizi ya hali ya juu ili kupambana nazo.
Tatizo ninaloliona kwa klabu za Tanzania ni kwamba zinatumia gharama na maandalizi ya hali ya juu zinapotaka kupambana zenyewe kwa zenyewe kwenye Ligi Kuu na si mechi za kimataifa, hasa timu ngumu kama hizo.
Huwa tunaona Yanga inapotaka kucheza na Simba maandalizi yake yanavyokuwa, timu inapelekwa Pemba na kupewa kila kitu.
Kama APR iliweza kuishika kooni Yanga, basi ijue Al Ahly inaweza kuwa ni mara tano yake, hivyo maandalizi yake yawe ya hali ya juu.
Kwa upande wa Azam nayo ikumbuke kuwa Esperance si Bidvest, nayo inahitaji maandalizi ya hali ya juu ili kuiondoa kwenye michuano hiyo.
Nikisema maandalizi nina maana ikiwemo kucheza mechi za Ligi Kuu ili kuangalia mapungufu na kuyarekebisha na si kuomba kuahirishwa mechi.
Wenzetu wakati mwingine hutumia mechi za ligi kama maandalizi ya michuano hiyo na kuangalia viwango vya wachezaji wao, tofauti na sisi tunaopenda kufanya maandalizi bila kucheza mechi yoyote.Hakuna kisichowezekana chini ya jua.
Yanga inaweza kuiondoa Al Ahly au Azam ina uwezo nje ya michuano Esperance kama zikijipanga sawasawa.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








