Mayanja ndiye kocha sahihi Simba

14Mar 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Mayanja ndiye kocha sahihi Simba
  • Mayanja ni kocha wa Kiafrika ambaye anajua aina ya soka letu -- lazima uwe na wachezaji wenye utimamu wa mwili na ili kuwa nao, panahitaji mazoezi magumu na uwalinde kwa kuhakikisha wanakuwa kambini muda mwingi.

BAADHI ya wanachama na mashabiki wa Simba walikuwa wakipiga kelele kuwa 'mchawi' aliyekuwa akisababisha timu yao isifanye vizuri ni viongozi.

Wakaenda mbali zaidi na kusema kuwa hata usajili walioufanya msimu huu ni mbovu.

Siku hazigandi, sasa simsikii mwanachama au shabiki wa Simba akiongea maneno hayo. Habari kubwa kwa wapenzi wa Simba kwa sasa ni ubingwa tu!

Simba ya sasa ina uhakika wa ubingwa na uwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa mwakani, lakini ikiwa itafanya vema katika mechi zote zilizobaki na iziombea njaa Azam FC na Yanga.

Kwa nini Simba kwa sasa imeonekana kufanya vizuri kwenye mechi zake za Ligi Kuu na Kombe la FA na wakati ina wachezaji walewale waliokuwa wakidaiwa kuwa ni wa pesa ndogo?

Ni kocha Jackson Mayanja. Kocha huyo ameshusha presha kwa viongozi wa Simba ambao walikuwa wakitwishwa 'zigo' kila kukicha kutokana na timu yao kuwa na mwenendo wa kusuasua hasa duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Nakumbuka wakati kocha Dylan Kerr alipoondolewa, baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba walichachamaa na walikuwa akisema wazi kuwa tatizo la klabu yao si kocha, ila ni viongozi kwa sababu hawakuwa makini katika usajili.

Lakini haohao wamebadilika na kudai "Kerr alichelewa kuondolewa" na pengine angeondoka mapema, Simba ya Mayanja ingekuwa inaongoza ligi kwa pointi nyingi zaidi ya hizi ilizonazo.

Simba ya Kerr ilikuwa dhaifu katika utimamu wa mwili kwa wachezaji kutokana na aina ya mazoezi yaliyokuwa yakitolewa na Mwingereza huyo.

Simba ya Mayanja inacheza mpira wa kasi, pasi nyingi na ina uhakika wa kuihimili timu pinzani kwa kmuda wote wa mchezo.

Mayanja anaonekana kujua tatizo sugu la muda mrefu ambalo limekuwa likiitafuna timu hiyo ya Msimbazi, na amelitibu.
Mfumo na aina ya uchezaji wa Simba ni wa pasi fupifupi na kuburudisha zaidi, lakini timu hiyo ilikuwa ikishindwa kufikia malengo hayo kwa kukosa pumzi na stamina.

Pamoja na kuendeleza utamaduni huo, amewaimarisha nyota wa Simba. Mayanja ni kocha wa Kiafrika ambaye anajua aina ya soka letu -- lazima uwe na wachezaji wenye utimamu wa mwili na ili kuwa nao, panahitaji mazoezi magumu na uwalinde kwa kuhakikisha wanakuwa kambini muda mwingi.

Hili ndilo lililomshinda Kerr. Alidhani wachezaji wa Kiafrika hasa kwenye ligi za kwetu wanaweza kulinda mazoezi ya stamina yanayoyapata mwanzoni mwa msimu kujiandaa na ligi kama inavyokuwa huko majuu.

Mayanja ni miongoni mwa makocha wazuri wanaotengeneza timu imara, yeny pumzi na stamina ya hali ya juu.

Ndiye aliyeitengeza Kagera Sugar ikawa moja ya timu tishio kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo chini yake ilizipiga Simba na Yanga kila zilipokanyaga kwenye Uwanja wa Kaitaba na hata kwenye Uwanja wa Taifa.

Simba na Yanga zote zilifungwa bao 1-0 kila moja msimu wa 2012/13 zilipokanyaga Kaitaba.

Uwanja Taifa, Simba na Yanga zilikuwa zikiifunga kwa tabu Kagera Sugar, lakini wakati mwingine pia zilishindwa kuifunga.

Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 na Kagera ya Mayanja kwenye Uwanja Taifa msimu wa 2012/13, ikitangulia kufunga magoli mawili, lakini yalirudishwa yote kutokana na stamina na pumzi za wachezaji wa timu hiyo chini ya Mganda huyo.

Hata msimu uliofuata wa 2013/14, Kagera Sugar ya Mayanja ilirudisha bao dakika za majeruhi dhidi ya Simba na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo ya Msimbazi wang'oe na kurusha viti Uwanja wa Taifa.

Binafsi ninafikiri viongozi wa Simba wanapaswa kumwongeza mkataba Mayanja na kumfanya kuwa kocha wa kocha mkuu na si kocha wa muda kama ilivyo kwa sasa,
Iko wazi kwamba viongozi wengi wa timu kubwa nchini, hasa Simba na Yanga, wanapenda kuajiri makocha wazungu na pengine Simba watataka Mayanja awe chini ya mzungu.

Naamini uamuzi wa kuleta mzungu tena Msimbazi utakuwa na athari kwa timu hiyo kutokana na hofu yangu ya kutowiana kwa falsafa ya Mayanja na kocha huyo atakayeletwa.

Kocha ajaye anaweza kuwa na falsafa yake tofauti na ya Mayanja, hivyo kutowina kiufundishaji kwa asilimia 100.
Kadri ya uelewa wangu wa soka la Tanzania, Simba ya msimu ujao itamhitaji zaidi Mayanja kuliko yeye anavyoihitaji Simba kwa sasa.

Kama atapewa mahitaji yake na kuongezewa wachezaji wa kiwango cha hali ya juu, nina uhakika chini yake, timu hiyo itafanya vizuri zaidi.

Sioni sababu kuntu kwa Simba kuhangaika kutafuta kocha mzungu ilhali wazungu wengi walioajiriwa Msimbazi wameshindwa kuipa mafanikio.

Mayanja aachwe andelee kuwa kocha mkuu Simba kwa kuwa mtu sahihi kwa sasa na baadaye.