Agizo hilo la Waziri Simbachawene linakuja baada ya uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kushindwa kufanyika mara mbili mwaka huu pekee, lakini mara tatu tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Oktoba 25, mwaka jana.
Kushindwa kufanyika kwa uchaguzi huo, tunakumbuka Nipashe, kumekuwa ni kutokana na ama sababu ambazo hazijulikani, kuzuka kwa vurugu na hata kuwepo kwa amri feki za mahakama zinazokataza kufanyika kwa uchaguzi, mpaka kesi ya msingi iliyo mahakamani iamuliwe.
Kesi ya msingi ipi?
Kimsingi hakuna kesi halali ya kupinga kufayika kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam iliyopo mahakamani kwa mujibu wa ufahamu wetu, Nipashe, na hata Waziri Simbachawene alikiri juzi kuwa zuio la muda lililodaiwa kutoka mahakamani na kusababisha Uchaguzi wa Meya huyo uliokuwa ufanyike Februari 27 ushindikane, lilikuwa feki.
Pamoja na nia njema ya serikali kutaka haki itendeke na wakazi wa jiji hili kubwa zaidi kibiashara nchini wapate maendeleo wanayostahili kutokana na maamuzi ya vikao halali vya wawakilishi wao, hatuna hakika Nipashe kama Meya wa jiji atapatikana kabla ya Machi 25, kama Waziri alivyoagiza.
Hatuna hakika Nipashe kama Meya wa jiji atapatikana kabla ya Machi 25, tunasema, kwa sababu kuna kila dalili kuwa upande mmoja katika uchaguzi huo umepania kuona uchaguzi haufanyiki kwa gharama yoyote.
Tungeweza kuficha jina la upande ambao tunaaamini, Nipashe, umepania kuona uchaguzi haufanyiki kwa gharama yoyote lakini idadi ya wajumbe wa mkutano wa uchaguzi huo unaweka wazi chama husika.
Kwa mujibu wa orodha rasmi ya wajumbe wa mkutano wa Halmashauri ya Jiji, katika wilaya ya Kinondoni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ina wajumbe 38 kulinganisha na 20 wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Wakati katika wilaya ya Ilala, Ukawa ina jumla ya madiwani na wabunge 31 huku CCM ikiwa na 23, chama tawala kinaongoza wilayani Temeke kwa kuwa na wajumbe 31 kulinganisha na 18 wa Ukawa.
Unapojumlisha namba hizi, ndipo siri ya upande ambao umepania kuona uchaguzi haufanyiki kwa gharama yoyote inapowekwa wazi maana wakati CCM ikiwa na jumla ya wapiga kura 74, Ukawa ina 87 hivyo kuwa katika nafasi ya kutoa Meya wa Jiji kwa mara ya kwanza tangu uhuru.
Tumeona CCM ikija na mbinu ya kuwasilisha pingamizi feki za mahamaka, kutaka kuhalalishwa kwa wajumbe kutoka Zanzibar licha ya kuwa masuala ya Serikali za Mitaa si ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Na imtosha sasa, tunaona Nipashe.
Ifike mahali basi CCM ikubali uchaguzi wa kabla ya Machi 25 ufanyike kwa kufuata misingi ya kisheria na kidemokrasia ili wananchi wa Dar es Salaam waanze kupata huduma kupitia chombo chao cha uwakilishi.










