Yanga, Azam FC tunahitaji ushindi mnono leo

12Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Yanga, Azam FC tunahitaji ushindi mnono leo

SAFARI ya timu za Tanzania kusaka mataji ya klabu Afrika, inaendelea tena leo kwa Yanga na Azam FC kurusha karata zao ugenini.

Mabingwa wa Bara, Yanga watakuwa mjini Kigali, Rwanda kucheza na APR katika mchezo wa kwanza hatua ya awali, Ligi ya Mabingwa Afrika.

Azam FC, wako nchini Afrika Kusini kucheza na wenyeji wao, Bidvest Wits katika mechi ya Kombe la Shirikisho. Azam ndiyo kwanza wanaanza mashindano.

Yanga inakutana na APR baada ya kuvuka kikwazo cha kwanza walipoiondoa timu kutoka Mauritius.
Kwa muda mrefu timu za Tanzania zimeendelea kuwa na rekodi mbovu kila zinaposhiriki mashindano ya kimataifa, siyo klabu wala timu ya taifa.

Kama tuna rekodi ya kujivunia, basi ni ile ya timu zetu kutolewa kwenye mashindano katika hatua za awali.
Kwa mfano, rekodi ya juu kwa timu za Simba na Yanga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikuwa 2003 Simba ilipoishia hatua na makundi na hatua kama hiyo kwa Yanga mwaka 1998.

Pengine rekodi nzuri ni ile iliyowekwa na Simba mwaka 1993 ilipofikia hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho.
Tangu wakati huo hadi sasa, hakuna timu yenye rekodi ya kujivunia kwenye michuano ya kimataifa Afrika.

Leo wakati Yanga na Azam wakipeperusha bendera ya nchi Afrika, wana kila sababu ya kujiona wana deni kubwa la kulipa, siyo tu kwa mashabiki wao, bali taifa kwa jumla.

Katika mashindano makubwa kama hayo, hakuna timu dhaifu, wala hakuna mechi rahisi. Kikubwa ni wachezaji kupambana na kuifanya kila mechi kubeba taswira ya fainali.

Tunafahamu kila timu imejiandaa, lakini siku zote tunaamini kuwa, timu inayojiandaa vizuri ndiyo inayokuwa jirani na mafanikio kuliko ile isiyofanya hivyo.

Kama mashabiki wa soka, tunaamini kuwa walimu wa timu zote mbili wanafanya maandalizi ya kutosha kwa timu zao.
Maandalizi haya siyo ya kushiriki tu, bali ni yale ya kushindana na kuleta mafanikio, ambayo ndiyo kiu ya kila Mtanzania.
Tunafahamu wachezaji wana kiu kubwa ya kuleta mafanikio. Lakini lazima wafahamu kuwa, mafanikio huja kwa vitendo na siyo nadharia.

Tungependa kuona wachezaji wa Azam na Yanga wakicheza kwa kujituma na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu.
Katika mashindano makubwa kama hayo, nidhamu ni msingi mkubwa wa kufanikiwa. Inatosha kujiridhisha kwamba, wachezaji wamepewa maelekezo ya kutosha na mbinu za kusaka ushindi. Kazi kubwa mbele yao ni kutekeza maagizo kwa vitendo.

Ratiba ya mechi zao kuanza ugenini, iwatie moyo wa kusaka ushindi mkubwa ili iwe rahisi katika mechi ya marudiano.

Watanzania watakaokuwa wakifuatilia michuano hiyo wana kiu ya ushindi na kinyume na matokeo ya ushindi, maana yake tunaendelea kutengeneza njia yetu ya kuaga mashindano katika raundi za awali.

Tunazikitakia kila la heri Yanga na Azam katika mechi zao leo hii.