Unajua huyu mzungu anafanyaje na kwanini ameamua ajirekodi na kutuma taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari? Ipo hivi.
Kocha huyo amekuwa akirekodi sauti yake na kuelezea mambo mbalimbali ya kiufundi, yanayohusu mchezo uliomalizika, pia mipango na malengo ya timu kwenye michezo ijayo.
Alisema, “Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) linatuelekeza jinsi gani ya kuzungumza kwenye vyombo vya habari na ni kitu gani sahihi kwaajili ya kulizungumza kwenye vyombo vya habari.
“Najirekodi mwenyewe na kuweka taarifa kwenye mtandao wangu wa kijamii kwa ajili ya kuwarahisishia waandishi wa habari ili wasiangaike kunitafuta kwaajili ya mikutano. Nafahamu nini kinahitajika kutoka kwa kocha kabla na baada ya mchezo hivyo ninapenda kuwatumia kwenye simu na barua pepe.
“Pia kufanya hivyo kunasaidia kuitangaza timu ya Toto kwasababu watu wengi wameweka akili kwa timu kama Simba na Yanga jambo ambalo si sahihi hivyo ninatumia uwezo wangu kuitangaza timu,” alieleza kocha huyo mwenye leseni ‘B’ ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA).
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 25 amekuwa mshauri mkubwa kwa kocha Mkuu John Tegete na mara kwa mara amekuwa karibu na wachezaji kuwapa ushauri na kuwapa maelekezo.










