Elimu Vyuo Vikuu izingatie viwango

21Feb 2016
Mhariri
Dar
Nipashe Jumapili
Elimu Vyuo Vikuu izingatie viwango

Wakati Serikali ikiendelea kupanua wigo mpana kwa wananchi kupata elimu ili kupambana na soko la ajira katika fani mbalimbali, ina wajibu mkubwa pia kutanguliza tahadhari ya ubora wa elimu itolewayo,

Ikiwa ni pamoja na kuzingatia mitaala ya taaluma zinazotolewa kuanzia elimu katika shule za Sekondari hadi Vyuo Vikuu vyote nchini.

Elimu ndio msingi mkubwa wa kupambana na umaskini, na ndio maana Serikali imetanguliza elimu bure kuanzia shule za msingi hadi kidato cha nne kama kipaumbele chake katika mapambano ya kuzikomboa familia maskini zisizoweza kugharimia kusomesha watoto.

Dhamira ya Serikali ni kuiwezesha jamii ya Watanzania kuingia katika karne ya Sayansi na Teknolojia, katika uchumi wa kati utakaotegemea uwezo wa kitaaluma katika teknolojia ya kisasa ili kujitosheleza katika kuendesha viwanda pamoja na maeneo mengine ya kisayansi.

Tunaamini kuwa ili kufikia lengo hilo, vyuo vikuu vilivyopo ni lazima vitoe elimu yenye viwango vya ushindani kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wahitimu wa vyuo vikuu wanakuwa na elimu inayokubalika katika masoko ya ndani na nje.

Tunaunga mkono maamuzi yaliyofikiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) mwishoni mwa wiki hii ya kuvifuta vyuo vishiriki vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph (SJUIT) kutokana na kukiuka sheria na utaratibu wa uendeshaji.

Vyuo hivyo, vilivyoko Songea na ambavyo vilikuwa vikitoa taaluma ya sayansi ya kilimo na teknolojia ya habari, vimethibitika kuwa vilikuwa havitoi elimu ya chuo kikuu kwa kiwango kinachokubalika.

Kwa kuepusha hasara kwa wanafunzi husika pamoja na taifa, TCU imeamua kuwahamisha wanafunzi wote 2,046 waliokuwa wakisoma katika vitivo mbalimbali chuoni hapo, kwenda vyuo vingine vyenye programu za masomo zinazofanana na vyuo hivyo kwa kutumia utaratibu ambao hautawaathiri.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya alisema Tume imevifutia vibali vya kuanzishwa kwa vyuo hivyo vishiriki na kuidhinisha uhamisho wa wanafunzi wote waliokuwa wanasoma vyuo hivyo, na akaongeza kuwa mikopo yao iliyokuwa inatoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) itahamishiwa kwenye vyuo watakavyohamia.

Profesa Mgaya alikiri kuwa kwa muda mrefu, vyuo vikuu vishiriki huwa na mlolongo wa matatizo mengi yakiwemo ya ubora, uongozi, ukiukwaji wa sheria na taratibu za uendeshaji kama zinavyobainishwa kisheria.

Vyuo vya aina hiyo mara nyingine hukosa walimu stahiki, kwa maana ya wenye shahada ya uzamili ambao ndio wanaopaswa kufundisha wanafunzi wa shahada, pia kukosa maabara zinazotakiwa na wakati mwingine kujitokeza matatizo ya ufundishaji kwenye mitaala na kukosa uongozi imara.

Athari za mapungufu hayo, zinawapata moja kwa moja wanafunzi kwa kutopata elimu kwa kiwango stahiki na hatimaye taifa linaweza kujiaminisha kuwa na wataalamu waliofuzu vyema kumbe bado yapo mapungufu kwao na ambayo yanaweza kuwakwaza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kitaaluma.

Ni wakati muafaka sasa kwa TCU kuhakiki vyuo vishiriki vyote nchini kama vinakidhi vigezo vilivyowekwa kiuendeshaji, na kama ikigundua mapungufu, TCU isisite kuchukua hatua stahiki ili kulinda viwango vya wasomi wa nchi hii viendane kulingana na matarajio ya kimataifa.