Ipo sababu ya kufanya hivyo kutokana na kile kinachoonekana kuwa mwendelezo wa kauli za kufurahisha na zisizo na taji kwa ustawi wa soka.
Kuna tatizo kubwa kwa viongozi wetu waliopewa dhamana ya kuongoza, na hii siyo tu kwenye michezo bali hata katika sekta nyingine.
Kinachowasumbua wengi wa viongozi wetu ni utumwa wa kutegemea kauli kama ndiyo kiini kufanikiwa badala ya vitendo.
Kuzungumza kwetu imekuwa rahisi zaidi kuliko dhana ya vitendo, ambayo kwa nchi zilizoendela ndiyo msingi wa hapo walipofika sasa.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika soka letu kumezwa na mambo ya siasa, kwamba pale panapohitaji utaalamu tunaingiza usanii.
Ndiyo maana hatuwezi kuiacha kauli ya Malinzi ya kuhakikisha Tanzania inacheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
Kuanzia sasa hadi 2026 ni miaka 10 tu imebaki, je ni kwa mkakati gani unaoweza kutengeneza wachezaji wazuri ndani ya miaka 10 na kwenda kucheza fainali hizo kubwa, pekee na aina yake?
Tunaweza kujiuliza. Tanzania ilicheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mara ya mwisho mwaka 1980 nchini Nigeria.
Leo hii ni zaidi ya miaka 35 hatujawahi kutia mguu kwenye fainali hizo, halafu tunafikiria kucheza Kombe la Dunia ndani ya miaka 10 ijayo.
Kwa kujiamini, Malinzi alimweleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa, mkakati wa kwanza wa Tanzania kuelekea kuchezaKombe la dunia ni kuwa mwenyeji wa fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17.
Hivi kweli kuwa mwenyeji kunatosha wa fainali hizo kunatosha kuwa sehemu ya safari ya kwenda kucheza kombe la dunia?
Nipashe, tunadhani kuwa dhamira ya Malinzi kuona Stars inacheza Kombe la Dunia, ndiyo tumaini la kila mmoja wetu.
Hata hivyo, mawazo hayo yamekuja mapema zaidi kulingana na muda uliobaki. Kuna msemo unasema; 'Timu inayojiandaa kwa ajili ya mashindano, ndiyo huwa karibu na mafanikio kuliko isiyofanya hivyo.'
Sasa leo Malinzi anatuambia habari ya mwaka 2026, kwa wachezaji wapi? Kwa mashindano gani ya vijana nchini yatakayozalisha wachezaji bora ndani ya miaka 10. Tusidanganyane.
Tunadhani, Malinzi yuko sahihi kutokana na utamaduni wetu wa kutoa kauli za kujifurahisha, lakini kwenye ukweli, ni ndoto kwa Tanzania kucheza fainali hizo mwaka 2026.
Kwa mara nyingine tena, tungependa kuishauri TFF kuwekeza nguvu nyingi kuandaa timu itakayocheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya hapo ndipo tufikiria kucheza Kombe la Dunia.
Ieleweke, hatuna nia wala siyo dhamira yetu kuwakatisha tamaa TFF kwa mipango yao mizuri, lakini kwetu tunachojaribu kueleza ni ushauri wa kitaalamu kutegemeana na mahitaji ya soka la sasa.










