Mikoa yote ianzishe vita dhidi ya magendo

23Feb 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Mikoa yote ianzishe vita dhidi ya magendo

MOJA ya maeneo ambayo yamekuwa yakisababisha serikali kukosa mapato yake ni biashara ya magendo.

Wafanyabiashara kadhaa ambao kwa makusudi wanataka kupata faida bila kutimiza wajibu wa kulipa kodi ya serikali, wamekuwa wakiingiza bidhaa nchini kutoka nje kwa kutumia njia za panya.

Hali hiyo imekuwa ikiIsababishIa serikali kukosa kodi ambayo ni chanzo chake kikuu cha kuingiza mapato ya kujiendesha pamoja na kutoa huduma muhimu kwa wananchi kama za elimu, afya, maji miundombinu kwa kutaja baadhi.

Njia hizo za panya ziko katika maeneo mengi, lakini zinazojulikana zaidi ni bandari bubu zilizoko katika mwambao wa bahari.

Bandari hizo hutumika kuingiza bidhaa mbalimbali kama mafuta ya kula, sukari, maziwa, biskuti, juisi, betri na nyinginezo.

Mikoa iliyoshamiri bandari bubu hizo ni Tanga, Dar es Salaam na Pwani.

Kwa mfano, katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna Mbweni, Ununio, Kigamboni na kwingineko ambako bidhaa hizo zinaingizwa kutoka Zanzibar kwa kutumia vyombo vya majini kisha kusambazwa katika maeneo kadhaa kwa ajili ya kuuzwa kwa kutumia magari na pikipiki mchana na usiku.

Biashara hiyo ambayo ni hujuma ya uchumi imekuwa ikifanyika kwa miaka mingi bila mamlaka husika hususan Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) na Jeshi la Polisi kuchukua hatua za dhati na endelevu kuidhibiti.

Yamekuwapo malalamiko mengi kwamba baadhi ya maofisa wa vyombo hivyo wamekuwa wakiwalinda wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

Hata hivyo, hatua za kupambana na hali hiyo zimeanza kuonyeshwa na serikali ya awamu ya tano kwa kuanzisha doria na msako wa usiku na mchana katika maeneo yote karibu na bandari bubu kwa kuwashirikisha polisi na maofisa wa TRA.

Kuna taarifa za kukamatwa kwa shehena ya bidhaa hizo katika nyumba za baadhi ya wakazi wa maeneo hayo.

Kwa kuwa maeneo yote yenye bandari bubu yanafahamika, kuna haja ya serikali kuwaagiza wakuu wa wilaya na mikoa husika kuhakikisha wanaanzisha na kusimamia operesheni za kudumu za doria na msako wa kuunasa mtandao mzima wa biashara hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, amenukuliwa akisema kuwa serikali inayo majina ya wahujumu uchumi wote ambao wanahusika na uingizaji wa biashara za magendo kupitia bandari bubu 19 zilizopo mkoani humo na kuwataka wahusika hao kujisalimisha kwenye vyombo vya dola.

Mahiza alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo inayo majina ya wafanyabishara wakubwa na ya vyombo vya usafiri wanavyotumia kusafirishia vikiwamo vya majini na nchi kavu, majina ya manahodha, maghala wanayohifadhia pamoja na maduka wanayosambazia.

Mahiza alisema pamoja na changamoto kuwa miongoni mwa wahusika ni wanasiasa, watumishi wa serikali na wafanyabishara wakubwa, lakini kwa sababu Rais John Magufuli, amewapa kinga na kuwataka tuwashtaki kama wahujumu uchumi, hawataogopa mtu kwa kujali rangi, kimo, cheo wala umri bali sheria itachukua mkondo wake.

Tunapongeza hatua ya Rais Magufuli ya kuwapa mamlaka viongozi wa serikali kuwasaka na kuwashtakiwa wahujumu hao wa uchumi kwa sababu magendo imekuwa kichaka cha watu wanaokwepa kulipa kodi za serikali kujificha bila kujali kwamba kutokulipa kodi ni kikwazo cha maendeleo ya nchi.

Ni matumaini yetu kwamba kila mkuu wa mkoa na wilaya ataanzisha vita ya kudhibiti magendo kwa kushirikisha Jeshi la Polisi, TRA na TPA.