Hilo ndilo neno linalostahili kusemwa tangu Rais John Magufuli, alipoingia madarakani mwaka jana.
Hiki ni kibwagizo maarufu katika moja ya nyimbo za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinazotumika wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ama mdogo unapotokea popote hapa nchini.
Ni kibwagizo ambacho huenda hakuna mtu aliyewahi kubaini mtunzi wa wimbo huu, marehemu John Komba alikuwa anamaanisha nini, lakini kwa sasa Watanzania wakiwamo wana CCM wameanza kuuelewa.
Mmoja wa mfano dhahiri kwamba sasa 'CCM mbele kwa mbele’ ni huu uliotokea wiki hii baada ya Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, kuagiza Wakuu wa mikoa, wilaya na viongozi wengine katika ngazi hizo pamoja na madereva, warudishe posho walizochukua.
Watumishi hao walichukua posho hizo kwa ajili ya kusafiri kwenda kushiriki sherehe za uzimaji wa Mwenge, mkoani Simiyu.
Kilichofanywa na Rais siyo kitu cha kawaida kama ambavyo baadhi ya watu wanaweza kufikiria, bali ni cha kijasiri na cha kuigwa na viongozi waliopo sasa na watakapokuja baada ya yeye kuondoka madarakani.
Sikuwahi kufahamu kama sherehe hizo za uzimaji wa Mwenge huwa zinahudhuriwa na Wakuu wote wa mikoa na wilaya na kukusanyika mkoa mmoja kwa ajili ya kazi hiyo.
Sherehe hizo pekee zinadaiwa kugharimu mabilioni ya fedha, lakini kwa bahati nzuri Dk. Magufuli, kachungulia mbali na kuona hasara hiyo na kuamua kuokoa jahazi.
Mara ya kwanza Rais Magufuli aliokoa Sh. bilioni nne ambazo zingetafunwa katika Siku ya Uhuru, Desemba 9 mwaka jana, akaokoa
tena fedha Siku ya Muungano na sasa ameokoa tena zingine.
Katika kipindi cha miezi 11, ameokoa Sh. bilioni 16.
Hili siyo jambo la kubezwa kwa kuwa naamini kiasi cha fedha kitakwenda kufanya kazi zingine za msingi ambazo zinagusa maisha ya kila mmoja.
Kwa hiki anachojaribu kupambana nacho Rais Magufuli, kumbe kingewezekana kwa miaka 30 kuanzia walau utawala wa Mwinyi, Mkapa na Kikwete.
Lakini katika miaka yote hiyo, serikali imeendelea kuishi kwa mazoea ikiwamo kufanya kila aina ya sherehe, huku kiasi kikubwa kikitumbuliwa kwa siku hiyo moja.
Rais Magufuli amekuja na aina mpya ya kuisimamia serikali, ikiwamo kuondoa vitu ambavyo havina msingi sana kwa jamii kama
hiki cha kuandaa sherehe kubwa kwa ajili ya kuzima Mwenge.
Kuzima Mwenge ni tendo ambalo haliwezi kuchukua zaidi ya dakika tano, lakini katika miaka yote hiyo kitendo hicho kila mwaka kimekuwa kikitafuna kiasi kikubwa cha fedha za walipa kodi.
Mimi sijawahi kuwasha Mwenge na wala sijui unazimwaje, ingawa nimewahi kuuona kwa macho yangu nikiwa mkubwa.
Kwa nchi yenye uongozi makini kama hii, nadhani hakuna gharama yoyote katika tendo la kuzima Mwenge.
Sherehe kama hizi zipo nyingi ndani ya mwaka mmoja, na kwa miaka mingi yamekuwa mazoea kwa watumishi wa umma kulipana posho bila kujali jamii nyingine inahitaji huduma za afya, elimu, maji na barabara.
Madhumuni ya kuwasha Mwenge Mlima Kilimanjaro, yalikuwa ni kumulika nchi nzima ili kuleta upendo penye chuki, kuleta amani penye vita, kuleta umoja penye mfarakano na kazi hii ilifanywa kwa kujitolea.
Sina hakika kama Siku ya Uhuru ambayo Mwenge uliwashwa katika Mlima Kilimanjaro, kama waliofanya kazi hiyo walilipwa posho nono kama hizi tulizoona Rais kaziokoa.
Kama waliowasha Mwenge walifanya kutokana na uzalendo, kwa nini leo hali ibadilike na kuonekana kama siku hiyo ni siku ya watu kuvuna pesa kupitia posho wanazolipwa wanaposafiri?
CCM mbele kwa mbele, nadhani sasa imeanza kwenda mbele na kupitiliza na kugusa makada wa CCM ambao ni Wakuu wa mikoa na wilaya, walioamuriwa kurejesha posho za serikali walizokuwa wamelipwa.
Ndiyo maana siku zote mawaziri na watendaji wengi wa serikali, walikuwa wakipenda kulia kwamba serikali haina fedha, kumbe fedha zilikuwa zinapotea kupitia vitu hivi ambavyo vinawafaidisha wachache.
Kila ukigusa sekta ya afya ni kilio cha ukosefu wa fedha, elimu nayo hivyo hivyo, huduma ya maji safi utasikia Waziri analia, yaani kila kona ni kilio, kumbe fedha zinapotea kupitia vitu visivyokuwa vya msingi.
Rais Magufuli CCM mbele kwa mbele na sasa ninavyoona wanaoisoma namba zaidi ni wana CCM, ingawa waliotungiwa wimbo huo wa kuisoma namba ni wapinzani.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu Mbariki Rais Magufuli na zaidi ya yote muongezee busara azidi kufuta posho za watumishi wa umma ambazo siyo za lazima pamoja na kufuta sherehe za mazoea.