Adoo Shaibu ateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo

07Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Adoo Shaibu ateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo

Leo tarehe 7 Machi 2024, Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo imeidhinisha uteuzi wa Ado Shaibu kuwa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo.

Kwenye Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Hakainde Hichilema uliopo kwenye Jengo la Maalim Seif (Makao Makuu ya ACT Wazalendo), Wajumbe wa Halmashauri Kuu wamethibitisha kwa kauli moja mapendekezo yaliyofanywa na Mwenyekiti wa Chama Othman Masoud Othman.

Akizungumza baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ado Shaibu amesema kuwa baada ya kufanya kazi kubwa ya kujenga mtandao wa Chama ngazi za chini, kipaumbele chake kitakuwa ni ujenzi na uimarishwaji wa Chama kitaasisi.

"Niliposimama mbele yenu mliponichagua kuwa Katibu Mkuu wa Chama mwaka 2020  niliwaahidi kuwa nitakuwa Katibu wa 'field', sitajikita ofisini. Matunda ya kazi hiyo mmeyaona. Kwa kushirikiana na watendaji wenzangu, tumejenga mtandao imara zaidi wa matawi, kata, majimbo na mikoa. Kazi inayofuata ni kukijenga Chama kitaasisi. Ninawaahidi kuwa kwa kushirikiana na viongozi wenzangu, tutakijenga kitaasisi kama Chama madhubuti zaidi kitaasisi Afrika" amesisitiza Ado.