Uongozi wa chama hicho pia umetangaza awamu nyingine ya maandamano yatakayofanyika kwa wiki nzima ifikapo mwezi ujao.
Ni maazimio yaliyotangazwa jana baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kujifungia Mtwara, maandamano yakipangwa kufanyika katika kila makao ya makuu ya mikoa yote nchi nzima kuanzia Aprili 22 hadi 30 mwaka huu.
Akisoma maazimio hayo kwa niaba ya Kamati Kuu ya chama hicho jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema miongoni mwa mambo wanayoendelea kusisitiza yaboreshwe ni kupatikana Katiba mpya, nchi iwe na tume huru ya uchaguzi na kubadilishwa mfumo mzima wa kusimamia na kuendesha uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hoja ya pili, Mbowe alisema ni kubadilishwa mfumo mzima wa kutenga majimbo ya uchaguzi ili kuhakikisha yanazingatia idadi sawa ya watu wanaowakilishwa.
"Kuna mbunge wa Dar es Salaam leo anawakilisha wapigakura 500,000 au 600,000, lakini katika nchi hii hii kuna mbunge ambaye anawakilisha watu 30,000. Uwiano uko wapi? Haki iko wapi?
"Tunataka mgawanyo wa majimbo uwe kwa mfumo unaoitwa 'population quarter', ili watanzania wote wawe na haki ya uwakilishi," Mbowe alisema.
Alitaja hoja yao ya tatu ni nchi kuwa na mfumo unaotoa fursa kwa wapigakura wote wenye sifa kwa kuboresha daftari la wapigakura ili kuondoa dosari ambazo hujitokeza wakati wa uchaguzi.
Mbowe pia alisema wanataka kubadilishwa mfumo wa uteuzi wa wagombea ili kuondoa vikwazo vya kuengua wagombea wa upinzani.
Hoja ya tano, Mbowe alisema wameazimia kubadilishwa mfumo wa uendeshaji kampeni za uchaguzi ili kuondoa vitendo vya kunyanyasa wagombea wa vyama vya upinzani na kuwezesha matumizi sawia ya vyombo vya habari.
"Na hapa ninazungumzia zaidi vyombo vya habari vya umma. TBC ni mali ya wananchi wa Watanzania, gazeti Habari la Leo, Daily News, hivi ni vyombo vya habari vya umma, lakini vinatumika kama mali binafsi wakati vinaendeshwa na kodi ya Watanzania wote," alisema Mbowe.
"Sita, tunataka kubadilishwa mfumo mzima wa gharama za uchaguzi na namna ya kuusimamia. Pia tunataka kubadilishwe mfumo mzima unaohusu maadili ya uchaguzi na namna ya kuyasimamia ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji wagombea wa upinzani kwa kisingizio cha maadili ya uchaguzi.
"Nane, tumeazimia kuwe na mabadiliko katika utaratibu wa upatikanaji na uapishwaji mawakala wa vyama au wagombea wakati wa kupiga, kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya urais.
"Tisa, tunataka kuwekwa mfumo mpya na bora zaidi wa kutatua migogoro yote ya uchaguzi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi.
"Kumi, tunataka kubadilisha uteuzi wa madiwani wa viti maalum ili kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaowezesha wagombea binafsi kushiriki katika uchaguzi kama wagombea katika ngazi zote za uchaguzi kwenye taifa.
"Tunachokipigania hapa ni uhuru wa watu, matakwa ya kisheria, ulazima wa kugombea kupitia chama cha siasa ni kuwanyima Watanzania uhuru wao.
"Tutatembea mpaka viatu vyote viishe soli, na kama wanafikiri ni masihala waendelee kupuuza, tutaandamana mpaka haki zetu zipatikane na huu ni mwendelezo tu, tunamaliza awamu tunasikiliza mnasemaje, hayo mengine tutatangaziana mbele ya safari, hatua kwa hatua," alisema.
Mbowe alisema chama hicho kiko tayari kwa mazungumzo wakati wote na mazungumzo hayatazuia wala kusitisha maandamano yao.
"Tutaandamana, anayetaka kuzungumza tuzungumze huku tunaaandamana. Mambo ya msingi yakisikilizwa, basi twendeni tukaijenge demokrasia, tukaviandae vyama vyetu kwa uchaguzi, lakini wakiendelea kutupuuza, wakafikiri ni nguvu ya soda, watashangaa," alisema Mbowe.
DIASPORA
Mbowe aliema Kamati Kuu ya chama hicho pia imeagiza wanachama wao walioko katika mabara yote duniani, nao wajiandae kufanya maandamano katika miji yote mikubwa duniani.
"Tutaandamana Umoja wa Mataifa, London, Ujerumani, Japan, China, Afrika Kusini, Nairobi, Ufaransa na kila mahali kwa sababu tukikaa kimya tunaoteseka ni mamilioni, wakati wachache wetu wanaendelea kuneemeka katika taifa ambalo ni letu sote.
"Tutazidisha na kuendeleza mapambano hayo hadi hapo madai halali ya muda mrefu ya Watanzania ya kupata Katiba Mpya, mfumo wa kidemokrasia na uchaguzi, Watanzania watakapopata nafuu na hali yao ya maisha na kupunguziwa gharama za maisha, bei za bidhaa na huduma zote muhimu katika maisha yao," alisema.
Mbowe pia alisema wamechoka kuvumilia alichokiita dharau na ukaidi wa serikali kukataa haki na madai yao ya muda mrefu.
Alisema kuwa mwaka 1991, Tume ya Rais ya mfumo wa chama kimoja wa vyama vingi vya siasa, maarufu Tume ya Nyalali, iliyoundwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, ilipendekeza kutungwa Katiba Mpya na ya kidemokrasia kwa ajili ya Tanzania.
Alisema tume ililenga mfumo huo mpya wa demokrasia uwe na tume huru, sheria mpya na bora za uchaguzi zitakazohakikisha uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika.
Alisema Tume hiyo ilipendekeza kufutwa kwa sheria zote za ukandamizaji na kutungwa sheria mpya zitakazohakikisha kila Mtanzania anapata haki sawa ndani ya taifa lake.
"Serikali si tu imekataa mapendekezo hayo ya Tume ya Nyalali, bali pia imekataa mapendekezo ya mengi yaliyotolewa na tume nyingine nyingi zilizofuata ambazo iliziunda yenyewe," alisema Mbowe.
MAISHA MAGUMU
Mbowe pia alisema Kamati Kuu imeelekeza kamati ya wataalamu wa chama hicho kuandaa mpango wa taifa wa kunusuru wananchi dhidi ya ugumu wa maisha, kupunguza bei za vyakula na bidhaa muhimu ambazo alizitaja ni mzigo mkubwa wa maisha magumu unaokabili wananchi.
"Tuliomba serikali itangaze mkatati wa kunusuru wananchi na ugumu wa maisha, lakini haijafanya hivyo.
"Kwa hiyo, licha ya kuwa hatuko serikali, tuna watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri. Kamati Kuu imeagiza kuandaliwa mpango huo wa kunusuru hali ya ugumu wa maisha unaokabili wananchi kwa sasa," alisema Mbowe.
Tayari chama hicho kimeshafanya maandamano katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha kikishinikiza kufanyika marekebisho ya sheria zinazohusiana na uchaguzi na serikali kuja na suluhisho la ugumu wa maisha unaokabili wananchi kutokana na mfumuko wa bei za bidhaa huku vijana wengi wanaohitimu vyuo vikuu na vyuo vya kati wakikosa ajira.