Lakini hili haitoi uhalali wa kinachoshuhudiwa kwa vyakula wanavyouziwa abiria wanaotumia Stendi Kuu ya Mabasi Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mwandishi wa habari hizi, baada ya kufuatilia kuanzia uandaaji wa vyakula hivyo hadi vinavyofungashwa, amebaini dosari ambazo si tu zinakiuka miongozo na kanuni za afya, bali pia zinakinzana na maelekezo ya Sheria ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2009.
Sheria hiyo katika kifungu cha 32, inaelekeza mfanyabiashara anapotaka kutoa huduma ya chakula, sharti awe na eneo la kuhifadhi chakula lenye ukubwa wa kutosha, lisitunze unyevu, pawe na mwanga wa kutosha, penye kupitisha, pawe safi na pasiwe na wadudu vamizi, pasiwe karibu na msalani, pawe na sakafu, kuta na dari zinazosafishika.
Hata hivyo, kilichobainika Moshi, vyakula vinaandaliwa mazingira hatarishi yanayojumuisha maeneo ya karibu na msalani, mifereji ya maji machafu na dampo.
Vinakouzwa vyakula hivyo ni katika eneo la Stendi Kuu ya Mabasi Moshi na vichochoro vya kuingia katika stendi hiyo inayotumiwa na wastani wa watu 1,000 kwa siku kwa mwezi Februari hadi Oktoba na wastani wa watu 3,000 kwa mwezi Novemba hadi Januari.
Mfanyabiashara wa nguo jijini Arusha ambaye mara kwa mara hupita katika Stendi Kuu ya Mabasi Moshi, Jonathan Mchomvu, anasema amekuwa shuhuda wa abiria wengi kukumbana na maradhi ya tumbo wawapo safarini kutokana na kula vyakula vinavyoandaliwa katika mazingira hatarishi.
"Mimi binafsi ni miongoni mwa abiria waliopata madhara baada ya kununua mishikaki katika eneo la pembezoni mwa lango kuu kutokea hapa stendi.
"Shida hii ya vyakula vya aina hii haipo hapa Moshi pekee. Hata Stendi Kuu ya Arusha na Dar es Salama kuna tatizo hili. Kuna siku nilichukua keki zinazopitishwa kwenye magari kule Arusha, ilinisababishia shida ya tumbo. Kwa sasa nimejitambua, ninatembea na dawa za tumbo," anasema Mchomvu.
Abiria mwingine Ester Elinathani aliyezungumza na mwandishi katika Stendi Kuu ya Moshi wakati akiwa safari kwenda Morogoro, anatoa angalizo kwa walaji wa vyakula hivyo, vingi haviandaliwi katika mazingira salama kiafya, hata uhifadhi wake unatia shaka.
Hata hivyo, Ester anasema wengi wa walaji wa vyakula hivyo, kipato chao kiko chini. Hawawezi kununua vyakula katika hoteli ambazo wamiliki wa mabasi wameingia nazo ubia kupitisha abiria wao huko.
"Uchumi umekuwa mgumu sana. Mtu anatoka nyumbani kwenda msibani au katika utafutaji wa maisha, hawezi kuacha kununua sambusa ya Sh. 500 akanunua ya Sh. 1,000 au akaacha kununua chakula cha 'buku jero' (Sh. 1,500) akanunue cha Sh. 7,000," anafafanua Ester, mkazi wa Njoro, Manispaa ya Moshi.
Shabani Mzava ni dereva wa basi linalofanya safari za Moshi-Arusha. Anasema: "vyakula hivi vinaandaliwa katika mazingira ambayo wakati mwingine tunamwachia Mungu tu.
"Sambusa zinapikwa Kibosho, Marangu, Njoro Pasua na Mailisita huko. Anapewa kijana, analeta hapa stendi (Moshi) kuuza na zikibaki anazirudisha, kesho zitauzwa tena, zikibaki keshokutwa zitaendelea kuuzwa.
"Kula sambusa iliyochacha ni jambo la kawaida tu. Hawa wanaouza keki wakati mwingine haziivi, zimeharibika, basi tu kwa kuwa umeshauziwa unapotezea, lakini kwa kweli Kilimanjaro hakuna uongozi unaosimania afya za watu," analalama.
Mfanyabiashara wa simu katika stendi hiyo, Hamad Mzee, anasema hali mbaya zaidi kwa vitafunwa wanavyouziwa kutokana na kuandaliwa katika mazingira machafu karibu na stendi.
"Ninaona vituo vingi vya afya vinajengwa. Kama uuzaji wa vyakula vya aina hii vitaendelea katika stendi na maeneo mengi yenye mkusanyiko wa watu, vituo hivyo vya afya havitakosa wateja.
"Ukipita katika stendi, pembezoni mwa eneo wanalokaa polisi wa usalama barabarani ni moja kati ya maeneo ambayo yanaandaliwa chakula katika mazingira machafu, kuna mitaro ya maji machafu na watu wanaandaa chakula hukohuko na kuwapatia wateja.
"Ikiwa mamlaka zipo zinaangalia tu, wapishi wana nguo chafu, vyombo vyao havioshwi kwa sabuni, mvua ikinyesha kunakuwa na uwezekano wa kupata magonjwa ya mlipuko," anasema Mzee.
Wakala wa mitandao ya simu katika stendi hiyo, Zuhura Bakari, anasema kuwa mbali na wauzaji hao, wapo wanaopika vyakula nyumbani kisha kupeleka katika stendi hiyo na kuviuza. Hawafuati kanuni za afya zinazowataka kuweka chakula katika eneo safi, watoa huduma kufunika vichwa vyao na kuvaa sare maalum.
Eva Munisi, muuzaji dawa katika duka la dawa lililoko katika Stendi Kuu ya Mabasi Moshi, anasema dawa za kuzuia kuhara zinaongoza kwa mauzo dukani. Anabainisha kuwa kwa siku ni kawaida kwake kuuza dozi zaidi ya 30 hasa asubuhi na mchana. Wengi hufika dukani wakilalamikia kuumwa tumbo au kuhara.
Hata hivyo, hairuhusiwi kumuuzia dawa mteja pasipo kuwapo na maelekezo ya daktari.
WAUZAJI VYAKULA
Mmoja wa wauzaji chakula katika stendi hiyo, Hamida Jumaa, anasema bidhaa zake huziandaa nyumbani kwake Njoro, Manispaa ya Moshi, akitumia nishati ya kuni au mkaa.
"Wako wengine kweli wanapika kwenye mazingira ambayo hayaridhishi, na hawazingatii usafi. Hii ni kutokana na mamlaka za serikali kuanzia ngazi ya mtaa zinatilia mkazo kuchukua fedha tu bila kufanya ukaguzi.
"Wapo wateja wanaokuja na kusema wameona nzi, mende na hata nywele kwenye vyakula ikiwamo mchuzi na uji kwa baadhi ya wafanyabiashara wenzangu," anasema Hamida.
Mfanyabiashara wa sambusa katika stendi hiyo, Samson Isaya, anasema wanalazimika kuuza bidhaa hizo bila kujali usalama wake kiafya kwa wateja ili wapate fedha.
"Bosi anatengeneza nyumbani kwake, anakupa wewe kwa idadi unayoweza kubeba. Unakuja hapa stendi kuuza, jioni unapewa Sh. 3,000. "Sambusa ikianguka chini, hauwezi kuiacha, ni lazima kuifuta na kuirudisha kwenye kindoo chake ili baadaye ulipwe ujira kamili kulingana na makubaliano.
"Ni kweli mazingira hayaridhishi, lakini tutafanyaje? Tupo hapa kusaka kipato. Sambusa zisiponunuliwa zote, hatupewi fedha yote, hivyo itakulazimu kuuza hadi zitakapoisha. Kwa sasa hali ni ngumu, sambusa zinakwenda hadi siku tatu bila mafanikio, ndiyo maana wapo wanaolalamika zimechacha," anafafanua.
Mfanyabiashara mwingine katika stendi hiyo, Zenobia Mgaya, anasema, "ninauza chakula, ninaandaa keki na sambusa na kuleta hapa maeneo ya stendi kwa mwaka wa tisa sasa.
"Ukaguzi upo lakini tuna mbinu tunavyomalizana nao ili na sisi tupate riziki. Haitatokea kumwaga chakula hata siku moja, nitakihifadhi na kukiuza kesho yake. Si mimi tu, bali pia hata wenzangu.
"Tuna mitaji ya tia maji tia maji (midogo), wengi wametelekezewa watoto au kufiwa na waume. Tunasomesha, majukumu ni mengi. Chakula tunapika kwenye mazingira ya kawaida, vyakula vyote vyenye nyama ni Sh. 1,500, vya maharage Sh. 1,000, vyenye samaki Sh. 2,000 hadi 2,500," anasema pasi na shaka, bila kufahamu kwamba kuwa na majukumu mengi hakutoi uhalali wa kuvunja sheria na kanuni za usalama kiafya.
MADEREVA WALONGA
Mmoja wa madereva wa mabasi wanaopita katika stendi hiyo, Ruben Mfoi, anasema katika safari zao za kusafirisha abiria, kumekuwa na changamoto ya abiria kuhara wakiwa safarini.
"Watu kuugua matumbo ni kawaida wawapo barabarani na hii ni kutokana na aina ya vyakula wanavyotumia. Mwezi Februari, mwaka huu, kuna mtu tulimwacha katika Hospitali ya Same. Tulitoka naye Kibosho lakini kwa bahati mbaya tuliporudi tulijulishwa alipoteza maisha. Sasa hatujui ni kutokana na hali hiyo ya vyakula vya njiani au alikuwa na maradhi mengine," anasema.
Dereva huyo anasema wamekuwa wanakabiliwa na adha ya kusimama mara kwa mara njiani kutokana matatizo yanayowakumba abiria njiani, yakiwamo maradhi ya tumbo na kuhara.
Dereva mwingine wa basi, Harrison Mnzava, anasema kuna haja viongozi kuanzia ngazi ya mtaa hadi kitaifa kuwajibika kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kudhibiti uuzaji huo holela wa vyakula.
"Mara kwa mara inatulazimu kusubiria abiria wanaokumbana na tatizo la kuhara. Ukifuatilia, unagundua walinunulia vyakula huko stendi na kuvila. Sisi tunashauri abiria wachukue chakula kwenye maeneo rasmi kwa huduma hiyo, lakini tatizo hili ni kubwa. Wenye mamlaka wamelala usingizi wa pono," anasema.
Katika uchunguzi wake ulioanza Machi, mwaka huu, kwenye maeneo ya Njoro, Pasua, Mboya, Majengo na vichochoro vya mjini Moshi, mwandishi wa habari hii alibaini kuwa kati ya waandaaji 39 wa vyakula aliowafikia, 32 wako katika mazingira yanayokinzana na sheria na miongozo ya kiafya iliyobainishwa hapo juu.
Mwandishi pia alizungumza na wauzaji 24 wa vyakula katika stendi hiyo na maeneo ya jirani. 20 kati yao walikuwa wamefungasha vyakula vyao kwa kutumia vyombo vya plastiki na wengine waliosalia walitumia vikapu maalum vya kubebea vyakula.
Wauzaji hao hawakuwa na sare huku baadhi yao wakiweka vikapu vyao chini walipopakua chakula kwa ajili ya wateja wao. Pia hawana vifaa vya kuvaa mikononi, wakipakua chakula kwenye sahani za plastiki na wengine kwenye mifuko plastiki.
MAMLAKA ZINASEMAJE?
Ofisa Afya Mkoa wa Kilimanjaro, Happynus Pilula, anaanza kwa kutaja matakwa ya kisheria katika uanzishaji biashara ya chakula.
Anarejea Sheria ya Afya ya Jamii (2009) kifungu cha 32 inayoelekeza kwamba ili mfanyabiashara afungue eneo la biashara ya chakula, lazima awe na eneo la kuhifadhia chakula ambalo lina ukubwa wa kutosha, lisitunze unyevu, liwe na mwanga wa kutosha, lenye kupitisha hewa, liwe safi na lisiwe na wadudu vamizi, lisiwe karibu na choo, liwe na sakafu, kuta na dari zinazosafishika.
Pilula anasema wakati wa utoaji huduma watoahuduma wanapaswa kuvaa sare safi na viatu vya kufunika, wanawe mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka, wafanyiwe uchunguzi wa kiafya mara moja kila baada ya miezi sita na wanapaswa kutoa taarifa haraka ya kiashiria cha ugonjwa wowote unaoambukizwa kwa chakula.
"Mtoahuduma hapaswi kushika chakula ikiwa ana ugonjwa wowote wa ngozi hususani katika mikono, hasa ikiwa hilo eneo haliwezi kufunikika, asiteme mate, kutoa kamasi, asipige chafya, asivute sigara wala kutafuna chochote wakati wa kuandaa chakula au kuhudumia.
"Hapaswi kuvaa pete kidoleni, hapaswi kuvaa ndala, hapaswi kuwa na kucha ndefu wala zilizopakwa rangi na hina, hapaswi kuweka rangi kwenye nywele, lazima awe amefunika kichwa.
"Masharti haya yanakwenda sambamba na ukaguzi wa jengo ambao hufanywa na TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na leseni ya biashara kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)," anafafanua.
Ofisa Afya Pilula anasema uuzaji holela wa chakula ni jambo lisilokubalika kisheria. Kutokana na dosari zilizobainika katika Stendi Kuu ya Moshi na maeneo jirani, watakaa na wataalamu wa mkoa wake ili kutatua changamoto hiyo.
TBS katika ufafanuzi wa Novemba 14, mwaka huu, kupitia kupitia kwa Meneja Uhusiano na Masoko, Gladness Kaseka, ilisema Sheria ya Viwango, Sura 130 na kanuni zake, imepewa jukumu la kusimamia usalama wa chakula na ubora wa bidhaa za chakula na vipodozi kwa lengo la kulinda afya ya jamii.
"Maeneo ya biashara yanayohitajika kusajiliwa ni pamoja na hoteli za kitalii, na za kawaida, supermarkets (maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali), maduka ya jumla na rejareja ya vyakula na vipodozi.
“Mashine za kuchakata nafaka na mazao mengine yasiyofunganishwa, wauzaji na wasambazaji wa chakula kwenye mikusanyiko, vioski, baa na maghala ya vyakula na vipodozi, migahawa na magari yanayobeba vyakula na vipodozi," anasema Kaseka.
Alitoa tahadharisha kwa wafanyabiashara wote kuwa atakayekutwa anauza, kuhifadhi au kusambaza bidhaa za chakula na vipodozi bila kusajili jengo lake, atachukuliwa hatua za kisheria.
ITAENDELEA KESHO









