Dabo abaini tatizo la kukosa mabao Azam FC

31Aug 2023
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe
Dabo abaini tatizo la kukosa mabao Azam FC

LICHA ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo, ameeleza kukerwa na wachezaji wake kwa kushindwa kutumia nafasi wanazozipata.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo.

Azam FC juzi walivuna alama tatu zingine katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuibuka na ushundi wa mabao 3-1 dhidi ya Prisons, kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Baada ya kukamilika kwa dakika 90, Dabo alisema bado ana kazi kubwa kwenye safu yake ya ushambuliaji kuitengeneza iweze kutumia vema nafasi wanazotengeneza ili kupata idadi kubwa ya mabao.

Alisema hakufurahishwa na wachezaji wake kushindwa kutumia nafasi wanazotengeneza huku wakionekana kuridhika mapema baada ya kupata bao la kuongoza badala kupambana kutafuta ushindi mwingine.

“Tunapata matokeo mazuri, lakini sijaridhishwa na jinsi wachezaji wangu wanavyocheza hasa pale tunapoongoza, tunashindwa kutumia nafasi tunazotengeneza.  Kazi kubwa nitaifanya kipindi hiki ligi ikiwa imesimama kuhakikisha tunarejea na kuwa vizuri,” alisema Dabo.

Aliongeza kuwa mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa kwa Tanzania Prisons kucheza mpira mzuri kwa kutengeneza nafasi nao kushindwa kuzitumia, hivyo alilazimika kufanya mabadiliko kwa kumtoa Lusajo Mwaikenda na kumuingia Yannick Bangala.

“Tulilazimika kufanya mabadiliko hayo baada ya Lusajo kuumia na Yannick kuchukuwa nafasi yake, alicheza vizuri, ninaimani atakuwa vizuri na msaada mkubwa kwa timu baada ya kupata muunganiko,” alisema kocha huyo.

Kocha Mkuu wa Prisons, Fred Minziro, alisema wamefanya makosa ambayo yalikuwa faida kwa Azam FC kuwaadhibu mabao 3-1.

Alisema mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa na kutumia ufundi na mbinu na hatimaye Azam FC walifanikiwa katika mipango yao ya kuondoka na alama tatu.

“Wachezaji wamepambana, tumetengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia, sasa tunarudi uwanja wa mazoezi kufanyia kazi mapungufu yetu, kuhusu washambuliaji wangu kuna wachezaji watatu wa kigeni bado tunakamilisha utaratibu wa vibali vyao nina uhakika mechi ijayo nitawatumia,” alisema Minziro.

Alisema ligi imekuwa ya ushindani mkubwa kuliko msimu uliopita, hivyo anarejea uwanja wa mazoezi kufanyia kazi yale yaliyojitokeza katika mechi mbili walizocheza kwa sababu hawataki kuwa sehemu ya timu itakayocheza ‘Play off’ mwishoni mwa msimu.