Hii ni mara ya pili mfululizo kutwaa ubingwa huo, huku ikipata tena nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Wakati zimebaki raundi hizo, timu zitakazoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao zimeshapatikana, timu hizo ni Simba itakayoungana na Yanga kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam na Singida Big Stars zitaiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Kuingia fainali ya Kombe la FA, kati ya Yanga na Azam kumechangia timu itakayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu kushiriki michuano hiyo.
Tayari timu moja imeshateremka daraja kati ya timu tatu zinazotakiwa kushuka, nayo ni Ruvu Shooting, huku nyingine ikitarajiwa kushuka moja kwa moja, na zitakazoshika nafasi ya 13 na 14 zitacheza mechi za mchujo, kutafuta timu moja itakayokwenda kucheza mchezo wa mchujo na timu kutoka ligi daraja la kwanza 'Championship'.
Mpaka hapa ligi ilipofikia klabu mbalimbali zimeweka rekodi na takwimu mbalimbali nzuri na mbaya, huku wachezaji pia wakitengeneza rekodi zao.
Mwandishi wa makala haya amekusanya rekodi na takwimu ambazo zimewekwa kwa mtindo wa namba.
74 - Ni pointi za mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga walizonazo ikiwa tayari wameshatawazwa kabla ligi haijamalizika.
67- Hizi ni pointi za mshindi wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba ambazo hazitafikiwa na timu yoyote, zikimpa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
66- Hii ni idadi ya mabao ambayo Simba imefunga kwenye ligi mpaka sasa, ikiwa ni timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi mpaka sasa kabla ya mechi mbili za kumaliza msimu.
56 - Namba hii inasimama kama ni mabao ya kufunga ya Yanga ambayo tayari imetwaa ubingwa na inashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi mpaka sasa.
53 - Azam FC ina idadi ya pointi hizi ikishika nafasi ya tatu mpaka sasa kwenye ligi, ikiwa imejihakikisha kucheza Kombe la Shirikisho barani Afrika msimu ujao hata kama ikimaliza kwenye nafasi ya nne.
51- Pointi hizi ni za Singida Big Stars iliyopo kwenye nafasi ya nne, nayo ikiwa imeshajihakikishia kucheza Kombe la Shirikisho msimu ujao.
45 - Ni idadi ya mabao ya kufunga ya Azam FC, timu inayoshika nafasi ya tatu kwa kufunga mabao mengi mpaka sasa kwenye ligi.
44 - Mtibwa Sugar ndiyo timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi kuliko yoyote ile kwenye Ligi Kuu na hii ni idadi ya mabao hayo.
40 - Ni idadi ya mabao ya kufungwa ya timu mbili za Mbeya City na Polisi Tanzania zinazoshika nafasi ya pili kwa kuruhusu wavu wao kuguswa mara nyingi mpaka sasa.
39 - Timu ya Namungo inayoshika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ina idadi hii ya pointi kabla ya kumalizia mechi zake mbili zilizobaki.
37- Ni mabao ya kufungwa ya Dodoma Jiji ambayo inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo ya ligi ikiwa na pointi 31.
36 - Prisons iliyo kwenye nafasi ya nane ya msimamo imefungwa idadi hii ya mabao mpaka sasa kwenye ligi ikiwa na pointi 34.
35 - Ni pointi za Kagera Sugar ambayo ipo kwenye nafasi ya saba ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
33 - Timu ya Geita Gold imefunga idadi hii ya mabao na ipo kwenye nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi mpaka sasa.
30 - Ni idadi ya mabao ya kufungwa ya timu mbili, Coastal Union inayoshika nafasi ya 10 na KMC ambayo ipo nafasi ya 13.
29 - Ni pointi za KMC iliyo nafasi ya 13 na Mtibwa Sugar ambayo ipo kwenye nafasi ya 14 ya msimamo wa Ligi Kuu.
28 - Timu zote 16 za Ligi Kuu tayari zimecheza idadi hii ya mechi mpaka sasa.
22- Ni idadi ya mabao ambayo Saido Ntibazonkiza ameyachangia kwa kufunga na kutoa pasi za mwisho akiwa na klabu mbili tofauti msimu huu, Geita Gold na Simba.
16 - Straika wa Yanga, Fiston Mayele ana idadi hii ya mabao mpaka sasa akiwa ndiye kinara wa upachikaji mabao kwenye Ligi Kuu zikiwa zimebaki mechi mbili msimu kumalizika.
14- Clatous Chama wa Simba, anaongoza kuwa na pasi nyingi za mwisho 'asisst' kuliko mchezaji yoyote kwenye ligi, akifuatiwa na Saido ambaye ana 'asisst' 12 mpaka sasa.
13- Ni idadi ya mechi ambazo Yanga imeshinda ikicheza uwanja wake wa nyumbani kwa mechi 15 ambazo imecheza, ikiwa inaongoza kwa kushinda mechi nyingi nyumbani kuliko timu yoyote.
12- Ni mabao aliyofunga straika wa Yanga, Fiston Mayele akiongoza kwa wachezaji waliofunga mabao mengi kwa mguu huo, akifuatiwa na Jeremiah Juma na Prisons alipachika mabao tisa kwa mguu huo.
11- Simba na Azam kila moja imeshinda kwa idadi hii zikicheza nyumbani. Wakati Simba ikicheza mara 13 nyumbani na Azam imecheza mechi nyumbani mara 14.
9- Ni idadi ya mabao aliyofunga kiungo mshambuliaji wa Yanga Stephane Aziz Ki kwa mguu wa kushoto, akiwa ndiye kinara kupachika mabao mengi kwenye ligi kwa mguu huo wa 'dhahabu', akifuatiwa na straika wa Simba, Moses Phiri aliyefunga mabao matano kwa mguu huo katika magoli yake 10 aliyofunga mpaka sasa kwenye Ligi Kuu.
5- Mabao ya vichwa aliyofunga straika wa Polisi Tanzania, Kelvina Sabato ambaye ndiye kinara wa kufunga mabao kwa staili hiyo kwenye Ligi Kuu mpaka sasa.
4- Idadi ya mechi ilizoshinda Dodoma Jiji mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
3- Ihefu ndiyo timu inayoshika nafasi ya pili kwa kutoa sare chache zaidi mpaka sasa, ikiwa imefanya hivyo kwa idadi hiyo.
2- Yanga imetoa sare kwa idadi hii, ikiwa ni timu inayoongoza kwa kutoa sare chache zaidi, lakini pia namba hiyo inasimama kama idadi ya mechi ilizopoteza mpaka sasa.
1- Simba inaongoza kwa kupoteza mechi chache zaidi msimu huu kwenye Ligi Kuu, ikipoteza mara moja tu dhidi ya Azam FC kwa kufungwa bao 1-0, Oktoba 27 mwaka jana.
Straika wa Yanga, Fiston Mayele anaongoza mpaka sasa kwa kufunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na mabao 16, lakini akiongoza kwa kufunga mabao mengi kwa mguu wa kulia, akifanya hivyo mara 12.









