Mtindo huo umekuwa ukisababisha serikali za wilaya na mikoa katika maeneo yenye utoro kuanzisha msako dhidi yao, ili wapatikane waende shule kuendelea na masomo.
Inawezekana wapo wale ambao wazazi wao huwahamishia katika shule nyingine badala ya zile walizochaguliwa, lakini ninadhani si wengi kwani unaweza kukuta shule moja wanafunzi zaidi ya 200 hawajaripoti.
Ikumbukwe serikali imeongeza nafasi ya elimu ya sekondari, ili kusaidia watoto wa Kitanzania kupata elimu hiyo, lakini ajabu ni hao wanaochaguliwa lakini wanaingia 'mitini'.
Ili kukabiliana na hali hii ipo haja kwa serikali kufuatilia zaidi ili kupata kiini cha utoro huo na kukipatia ufumbuzi wa kudumu na kuachana na msako wa kila mwaka dhidi ya wazazi na wanafunzi wenyewe.
Wakati mwingine inawezekana miongoni mwa wanaofaulu ni wale wasio na mwamko wa elimu au ugumu wa maisha, wazazi wako tayari kuwaozesha binti zao ama kuruhusu wakafanye kazi za ndani ili wapate chochote cha kulisha familia.
Lakini inawezekana wengine wanalazimishwa na wazazi kubaki wakifanya shughuli za nyumbani, kutokana na kwamba hawana mwamko wa elimu hivyo wanaona elimu ya msingi inatosha.
Aidha, wakati mwingine mazingira ya sekondari za kata yanaweza kuwa chanzo kutokana na kwamba baadhi si rafiki kwa wanafunzi, kwa kukosa mabweni, umbali na pia ubovu wa miundombinu ya shule zenyewe.
Hilo halina ubishi, kwani unakuta mwanafunzi anatembea umbali wa kilomita 10 kwenda shule na kurudi nyumbani, halafu shuleni hakuna walimu wa kutosha, wala vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Hata hivyo, pamoja na yote hayo, sidhani kwamba yanaweza kuwa kigezo cha mwanafunzi kuacha kwenda shule, kwani wapo waliosoma katika mazingira hayo na wakafanya vizuri.
Ingekuwa vyema kama wazazi na walezi watawakazania watoto wao kwenda shule wakati taratibu nyingine za kuboresha mazingira ya shule zikiendelea, badala ya kuruhusu wawe watoro.
Lakini shule za umma ni mali ya wazazi na walezi, hivyo hawana budi kuzihudumia ili ziwe katika mazingira bora kwa manufaa ya watoto wao badala ya kujiweka pembeni na kudhani hawahusiki.
Sidhani kama ni sahihi wanafunzi kuziona sekondari za kata kana kwamba haziwafai, kwani zimekuwa ni mkombozi wa watoto wa maskini na ninaamini wapo waliofika mbali kupitia shule hizo.
Hivyo, wazazi na walezi wa wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kisha wanakaa nyumbani, ni vyema wakatambua kuwa pamoja na changamoto katika shule hizo, elimu bado ni ya muhimu.
Kwa maana hiyo, wakati serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya shule zake ili iwe rafiki kwa wanafunzi, ni muhimu wanafunzi nao kutokubali kuwa watoro kwa kisingizio kisicho na msingi.
Ingekuwa vyema kama wanafunzi wataacha kudharau elimu kwa visingizio kuwa haiwasaidii, bali watambue kuwa mataifa yaliyoendelea, wananchi wake wamesoma lakini wafahamu kuwa elimu ni ufunguo wa maisha ya kila mmoja. Ni kupitia elimu watu wanafahamu masuala ya afya, kilimo, chakula bora, usafi wao na mazingira.
Aidha, ni kupitia elimu hiyo kuna wasomi na wataalamu wa kada zote kuanzia wahandisi, wabunge, matabibu, walimu, wanahabari, wachumi, wakulima, wanasayansi na wafugaji pamoja na wataalamu wengine wote si wa Tanzania hata duniani kote.