Uhamasishaji ulifika hadi kwenye rekodi za muziki, nyimbo zilieleza umuhimu wa usafi, mfano na ipo nyimbo iliyokuwapo miaka hiyo naikumbuka, ‘Mtu ni Afyaa! mwananchi elewaaa…’ ulipigwa na Morogoro Jazz.
Ujumbe uliomo na mpangilio wa mashairi, lazima ukisikia utaguswa na kuanza kubadilika taratibu na kuweka maeneo yako kuwa safi.
Wiki iliyopita, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, alihimiza kila mmoja atunze mazingra na kuweka maeneo safi, pamoja na upandaji miti kwa ajili ya kivuli na matunda.
Alisema, usafi wa mazingira ikiwamo wa majumbani, kutotupwa taka ovyo, kunakoendana na upandaji bustani za maua, utaongeza utunzaji mazingira. Kwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, usafi ni kati ya sababu za umaskini, maradhi hususan na lisipotiliwa mkazo kwa wananchi na viongozi wa kila ngazi hasa kimkoa hadi kata, ni hatari kiafya.
Utaratibu wa usafi kila wiki ya mwisho ya mwezi, Jumamosi kuwa maalumu kwa ajili ya shughuli hiyo nchi nzima, inaongeza uwajibikaji wa viongozi kwenye maeneo yao.
Mkoa wa Dar es Salaam, utaratibu huo ulianza tangu sherehe za Uhuru mwaka 2015, ingawa sasa utekelezaji wake ni duni. Wanachokifanya wafanyabiashara na wajasiriamali wanafunga maduka yao hadi ipite saa na kufungua baada ya muda huo, huku wakiacha kufanya usafi.
Hadi sasa, utaratibu umezorota na kufanya maeneo kadhaa kuwa machafu. Utashuhudia hilo zaidi katika maeneo walikokuwa wamachinga na wafanyabiashara wakaondolewa kwa agizo la nchi nzima.
Wakuu wa mikoa walilisimamia ipasavyo, ingawa sasa upo utaratibu biashara kufanyika usiku, Je, usimamizi wa usafi maeneo haya nani anawajibika.?
Kunapokucha asubuhi baada ya biashara usiku kucha, maeneo haya yanakuwa dampo! Uchafu unazagaa. Kwanini utaratibu usiwekwe kusimamia hili? Chupa za vinywaji zenye rangi ya bluu, nyeusi, ndio usiseme zimejaa mitaroni, barabarani na haziokotwi. Waokota makopo wakidai hazifai kurejelezwa.
Mwisho wa siku wafanyabiashara hawa wanaojitafutia riziki, wataonekana hawaendani na taratibu zinazowekwa, lakini nani anawakumbusha, anawasimamia, watu wako huru!
Waelekezwe biashara ndio zifanyike usiku, lakini viongozi wa mitaa, maofisa afya, biashara, wakuu wa Wilaya na mikoa, kulibaini hili, tembeleeni mlikowaondoa wamachinga na mitaani.
Uamuzi wa usafi ulioanzishwa, yaani kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ilikuwa mwanzo kwa viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri kutekeleza hatua hii kwenye maeneo hayo, na kila kaya, eneo la biashara kuanzia asubuhi hadi saa nne asubuhi kuutumia muda huu kufanya usafi na kusitisha shughuli zao, usafi kwanza.
Hali si nzuri kwa maeneo mengi ya mitaani, barabara zimejaa vumbi, mchanga, taka kwenye mitaro, nafuu ipo katika barabara kuu tu, ndiko kunakofagiliwa kila baada ya siku kadhaa.
Uzoaji taka maeneo kadhaa, umesuasua, mitaa kadhaa ukipita hali ni hiyo, hata sokoni na kuliko na mikusanyiko mingi ya watu, vituo vya daladala.
Baadhi ya maeneo ikiwamo Tegeta, Kunduchi, Bunju, Buguruni, Mombasa, Temeke, Mbagala, Gongo la Mboto kwenye makazi ya watu hali hii ipo.
Wakazi walio wengi kutegemeana na eneo wanaloishi, hulipia ada ya ubebaji taka katika kila kaya kwa kiasi cha shilingi 3,000 ama 5,000 hadi 10,000 kwa mwezi, baadhi ya maeneo taka hazibebwi kwa wakati muafaka.
Nakumbuka watendaji, wakurugenzi wa halmashauri katika mikoa na wilaya nchini, waliagizwa kuhakikisha usafi na uondoshaji wa taka katika maeneo yao unafanyika kabla ya kuchukuliwa hatua.
Walitakiwa kuvunja mikataba kati yao na baadhi ya kampuni za kuzoa taka, hazitekelezi majukumu waliyopewa vilivyo, hata kusababisha ongezeko kubwa la taka mijini. Ifahamike, kati ya asilimia 80 hadi 90 ya taka zinazozalishwa mijini, hazikusanywi na mamlaka husika.
Halmashauri hasa za miji mikubwa zimeendelea kutoa sababu zisizo na mashiko katika kuhakikisha taka zinaondolewa kwa wakati, huku wakikusanya mapato makubwa kutoka kwa wazalishaji wa taka hizo, huku Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 kifungu cha 104 na 139 zinazitaka mamlaka husika kuondoa taka.