Mpaka sasa hakuna klabu kati ya hizo mbili iliyokubali au kukanusha, lakini vyanzo kutoka ndani ya Simba pamoja na dalili zinaonesha kuwa kipa huyo huu ni msimu wake wa mwisho kukipiga Msimbazi.
Kama ni kweli kwamba tayari Singida Big Stars wameipata saini ya kipa huyo, watakuwa wamelamba dume na nawapa kongole kwa kuamua kuanza kufanya usajili wa haraka sana.
Kwa asilimia kubwa ni kwamba Singida Big Stars msimu ujao ni moja kati ya timu itakayoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, hivyo wameanza kusaka wachezaji wenye viwango vya kucheza mechi za kimataifa pia wakianza na langoni.
Vyovyote itakavyokuwa, lakini hii ni kengele kwa klabu zingine ambazo zina nafasi kwa msimu ujao kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kuanza kufanya usajili mapema kwa ajili ya kutengeneza vikosi vyao.
Singida Big Stars ambayo ilipanda daraja msimu huu ni klabu inayoshangaza kidogo, kwani pamoja na uchanga wake, lakini imeonyesha iko vizuri kwenye masuala ya utawala, hasa katika kusaka wachezaji bora na wenye vipaji, na sasa wameanza kujitofautisha tena kwa kuanza kujiandaa mapema na usajili.
Ni moja kati ya klabu zilizofanya usajili bora zaidi msimu huu hapa nchini, ikiwa na wachezaji ambao hata klabu kubwa kama Simba, Yanga na Azam zinawamezea mate.
Cha ajabu ni kwamba wengi hawakuwa wanajulikana kabla, na wala hawajachafua kurasa za magazeti na mitandao, badala yake kazi zao zinaonekana uwanjani zaidi kuliko kwenye midomo ya watu. Wanaonekana kuwa wana maskauti wazuri zaidi.
Sipati picha sasa kwenye usajili wa wachezaji ambao watakwenda kucheza Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Hili ni somo kwa Klabu za Simba, Yanga na Azam nazo kuanza kusajili wachezaji kwa msimu ujao, badala ya kusubiri ligi zote zimeisha, halafu ndiyo zinaanza kutafuta wachezaji ambao wamepandishwa gharama na mawakala, baada ya kuanza kutaka kunyang'anyana.
Afrika hii ina wachezaji wengi mno wenye vipaji, lakini klabu zetu zimeshindwa kabisa kuwa na maskauti wazuri, badala yake wamekuwa na kundi la wachezaji wachache tu walioonekana wakicheza dhidi yao na kuanza kugombania, tena kila msimu utasikia majina ya watu hao hao tu.
Hata Bara la Amerika Kusini kama Brazil, Peru, za zingine kuna wachezaji wenye vipaji kwa gharama za kawaida tu, shida ni wigo wa mawakala wao. Kina Bruno Gomes wapo wengi sana, lakini wanahitajika watu kama viongozi wa Singida Big Stars kuwapata.
Kwa klabu kama Simba, Yanga na Azam kwa muda huu zilitakiwa tayari zimeshajua mwakani zinamsajili nani kuongeza nguvu kwenye kikosi chao kwa kuwapa mikataba ya awali, na ligi zinapomalizika, basi nao wanamaliza shughuli kwa kuwasainisha mikataba halisi.
Hii inasaidia sana pale msimu wa kujiandaa na mashindano 'pre-season' inapoanza, kuwa na wachezaji wote wanaohitajika, badala ya kukaa kambini na wachezaji wanaokuja kuachwa baadaye, wanasajiliwa wengine ambao hawana utimamu wa mwili kwa wakati huo.
Hili limeiathiri sana Simba kwa misimu miwili sasa, kwani inachelewa sana kusajili, badala yake inaingia kambini kujiandaa na msimu na wachezaji wengine ambao baadaye wanakuja kuachwa au kutolewa kwa mkopo, lakini wale waliotakiwa kukaa na kocha akiwapa ufiti na mbinu, wanasajiliwa baadaye kabisa siku zimeisha kiasi cha wachezaji wao kutokuwa na utimamu, wakihitaji muda mrefu mno ili kuwa kwenye viwango vyao na wakati huo michuano inakuwa imeshaanza.
Tena kwa safari hii wanacheza Super Cup itakayoanza Agosti, hivyo wanatakiwa wabadilike sana. Msimu ujao timu nne zinazoiwakilisha nchi zijaribu kubadilika, zisajili mapema ili wakati wanakwenda 'pre-season' wawe tayari na wachezaji wote wa msimu husika, badala ya kusajiliwa wakati kipindi hicho kimemalizika.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







