Chama hicho kinaongozwa na Zitto Kabwe, ambaye ana mzizi kutoka Chadema, huku Mwenyekiti ni Juma Haji Duni maarufu ‘Mjelajela’ naye mwenye mzizi wa chama cha CUF, mwezi uliopita walianza mikutano kwenye mikoa mbalimbali nchini kuelezea ahadi zao kichama.
MKOANI TANGA
Wakiwa jijini Tanga katika uwanja wa Tangamano, kiongozi Zitto Kabwe, anasema baada ya maridhiano, wameamua kukutana kuelezea ahadi zao kwa wananchi.
Chama hicho kinasema kuna uwakilishi mdogo bungeni na wameamua kushughulika kero za umma, kwa kuunda baraza kivuli la mawaziri, watakaosemea wananchi kero zao serikalini.
"ACT Wazalendo inawaomba wakazi wa Tanga kuungana kufanikisha katika hili na mkoa wa Tanga na Pwani, ni waathirika wa matendo ya utekaji, mauaji na watu kubambikiziwa kesi," anatamka, akisisitiza ni mambo chama chao lazima kiyazungumze.
Kuhusu usambazaji mbolea, Zitto anaiasa serikali: "Unaweza kutoa mchango mkubwa kwenye kushusha uzalishaji nchini, hususani kwa mazao ya chakula au kushusha mfumo wa bei baada ya mavuno".
Anasema kwa misimu ya miaka miwili mfululizo, upatikanaji mbolea na pembejeo zingine za kilimo kwenye misimu miwili ya sasa, unakabiliwa shida ya kupanda bei, hata kuishia kwenye bei kubwa za vyakula.
"Serikali ilichukua pendekezo letu na hii kwetu ilikuwa hatua muhimu na ilibeba matumaini makubwa kwa wakulima kwa matarajio ya kupunguziwa gharama zilizokuwa zinaendelea kupanda na kuhakikishiwa urahisi wa upatikanaji mbolea.
"Wakala wengi walikuwa wanapatikana maeneo ya mijini, wakati wakulima wapo vijijini, wakulima walilazimika kutumia gharama zaidi kupata mbolea, pia kulikuwapo tatizo la uchache wa wakala na wengine wasio waaminifu kusambaza mbolea bandia," anasema.
JUMA DUNI HAJI
Mwenyekiti wa Chama hicho, Juma Duni Haji, anaeleza mchakato wa upatikanaji Katiba Mpya, akiitaka serikali kuhakikisha unakamilika, kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kuendana na matakwa ya umma.
Anasema mpaka sasa serikali haijaweka hadharani siku mchakato wa sheria ya mabadiliko ya katiba utakaowasilishwa bungeni kwa ajili ya kutoa fursa ya sheria hizo kutumika katika upatikanaji wa katiba mpya.
“Baada ya Rais kujibu hoja za wapinzani kuhusiana na mabadiliko ya siasa za kidemokrasia, hoja kuu iliyojitokeza ni mabadiliko ya katiba na vyama vya upinzani walielezea hili, kwa kutaka sheria ya uchaguzi sheria ya vyama vya siasa, sheria ya polisi iliyokuwa ikitusumbua sana wakati wa mikutano, sheria ya uchaguzi na sheria ya kura za maoni," anasema.
Juma Duni anaongeza katika maoni ya chama hicho katika kikosi kazi cha Rais, kinachoendelea kupelea maoni sasa, wameeleza njia na hatua nzuri za kufikia mabadiliko hayo, kwa serikali inatakiwa kutumia mawazo hayo kwa ajili ya kuipata Tanzania iliyo bora.
“Tunataka utaratibu wa namna ya sheria hizo zitakavyobadilika ili ziwahi na kutumika katika uchaguzi wa 2024 na 2025, tunataka kuona sheria hizi zinabadilishwa kwa kuanzia kupata baraka zake katika Baraza la Mawaziri, sisi tumesema kule Zanzibar, Dar es Salaam, Tanga na mikoa mingine tuliyopita muda rasmi wa kufikia mabadiliko" anasema.
Hata hivyo, Rais Dk. Samia mbali na kuwa na tume inayokusanya maoni kuhusu sheria na vyombo vyake nchini, ameahidi kufanyia kazi maoni kuhusu katiba ya nchi
MAKAMU MWENYEKITI
Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Bara), Dorothy Semu, anashauri suala la kupanda bei za vyakula, lipewe kipaumbele, hata linasababisha baadhi ya familia kuishia kula mlo mmoja kwa siku.
Dorothy Semu anasema, bado Serikali haijaleta ufumbuzi kuhusiana na suala hilo, hali inayowaumiza zaidi wananchi wenye vipato vidogo.
"Serikali ilisema imeagiza chakula nje isimamie kiingie sokoni kunusuru wananchi na kupanda kwa bei, pia tunaitaka serikali iachie chakula kilichopo kwenye ghala kutokana na hali ya wananchi kuwa ngumu na kuendelea kusumbuliwa na baa la njaa" anashauri.
Makamu Mwenyekiti huyo, anaongeza kuwa wakulima wa ndani wanatakiwa kuwezeshwa kufanya kilimo cha kisasa na kupata pembejeo kwa gharama nafuu, ili wazalishe kwa wingi na kupunguza gharama za uzalishaji, utakaowafanya kuuzia wananchi kwa bei rafiki.
"Serikali inatakiwa pia kuwezesha wakulima kutoka kilimo cha msimu na badala yake watumie njia ya kilimo cha umwagiliaji na kulima kwa mwaka mzima na ijenge uwezo wa kuhifadhi chakula cha kutosha kupitia mradi wa Taifa ( Mamlaka ya Uhifadhi wa Chakula NFRA)" anasema.
KATIBU WA CHAMA
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, akiwa mkutanoni Tunduru mkoani Ruvuma, anasema serikali inatakiwa kufanya maridhiano kwenye migogoro ya wakulima na wafugaji kama inavyofanya katika sekta nyingine.
Aidha anasema, serikali inatakiwa kutumia majukwaa rasmi kama Kamati za Ushauri za Wilaya na Mikoa (RCC na DCC) kujadili masuala hayo kwa upana na kuhusisha wawakilishi wa wakulima na wafugaji, ili kujenga maelewano miongoni mwao.
"Wakati Rais anaongoza maridhiano kwenye siasa yanapaswa kushuka pia kwenye kila sekta, matumizi ya mabavu katika kunusuru migogoro ya wakulima na wafugaji, ni jambo la kikoloni wanapaswa kufanya kama ilivyokuwa kwenye siasa," .
"Athari za migogoro hiyo imesababisha kuwa na mapigano baina ya wakulima na wafugaji, mapigano yanayohatarisha amani na usalama nchini,tatizo hili limekuwa kubwa zaidi katika Wilaya za Tunduru, Ruangwa, Nachingwea, Liwale, Lindi Vijijini na Kilwa"anaeleza.
Katibu Mkuu huyo, anasema hisia walizonazo wananchi wenyeji (wakulima) kwenye maeneo hayo dhidi ya wafugaji na viongozi wa Serikali ni dhairi kuna chuki baina ya makundi hayo na kwamba kwa hali hiyo chama hicho kinatoa maoni ya kushughulikiwa mapema migogoro hiyo.
"Tunafahamu kuwa wakulima na wafugaji ni makundi ya uzalishaji yanayotegemeana na kila mmoja anamuhitaji mwenzie lakini, uamuzi wa Serikali kuwaruhusu wafugaji kwenye ardhi ya Kilimo bila kuwashirikisha wanavijiji wenyewe ni kupandikiza mapigano isiyo ya lazima" anasema.
Shaibu anaisisitiza serikali kuwawekea wafugaji mazingira mazuri ya kufugia kwa kujenga malambo ya kunyweshea mifugo na kuwatengea maeneo ya malisho, utaratibu wa sasa unasababisha vurugu kwani wapo wafugaji wanalisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na pia wananywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji ambavyo vinahudumia.
Chama hicho kimefanya mikutano katika mikoa ya Dar es Salam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara,Ruvuma, Tabora na Kigoma ambapo walitumia nafasi hiyo kutambulisha Mawaziri Kivuli wa chama hicho.










