Katika hotuba yake ya mwanzo, anazungumza kuwatetea wahamiaji na wakimbizi, akiashiria uongozi wa kusimama na wanyonge wa taifa kubwa lenye nguvu, ushawishi kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia duniani.
Akiwa mjumbe wa Kamati ya Seneti ya Usalama na Masuala ya Kiserikali, anapigania ulinzi bora zaidi kwa wahamiaji ambao Marekani huitwa ‘dreamers’ akitaka uangalizi bora katika vituo vya kuwahifadhi wahamiaji.
Ni kwa mujibu wa andiko lililochapishwa na Mtandao wa Ikulu ya Marekani (White House), yote hayo yanaonyesha kuwa Harris ni mtetezi wa wanyonge, anayetaka haki, maridhiano na kuchukuliana.
Akiwa Seneta, anatetea sheria ya kupambana na njaa, kutoa misaada , kuboresha huduma za afya ya uzazi na kushughulikia athari za mabadiliko ya hali ya hewa kama mjumbe wa Kamati ya Seneti ya Mazingira na Kazi za Umma.
Leo hii Marekani inampa jukumu muhimu katika kuwashirikisha viongozi wa dunia na kuimarisha ushirikiano na ushirika na taifa hilo akilenga mustakabali wa pamoja wa kuwa na Amerika inayosimama na kushirikiana na wengine, unaongeza mtandao huo.
MBIO URAIS
Makamu Harris, anafikia hatua hiyo, pale anapoanza mbio za kuingia ikulu kupitia chama cha Democrat, anatangaza nia ili kuchuana na bosi wake wa sasa Joseph Biden, akiomba uteuzi wa chama hicho kuwa mgombea kwenye uchaguzi mkuu wa Novemba 2020.
Nyota ya Harris inaanza kung’ara anapoinukia kwa kasi na kujitosa katika kinyang'anyiro cha uteuzi wa urais, wenye msimamo wa kiliberali kwenye chama hicho wakimpenda kwa imani kuwa amebeba mustakabali (hatima na mambo ya baadaye) wa chama chao. Akiwa mwanamama kijana .
Licha ya kuingia katika kinyang'anyiro hicho hakuendelea na mchakato na kumwachia mpinzani wake Joe Biden kupanda na kufanikiwa kwenye mbio za urais.
Wengi walidhani kivumbi hicho kilimmaliza na nafasi yake ya kuwania urais ikawa imepotea, wapo waliodhani kuwa asingekuwa na wadhifa wa makamu wa rais , walikosea, akawa mgombea mwenza 2020 akaanza kazi.
Harris anayekaribia miaka 57 sasa ni binti wa wahamiaji kutoka Jamaica na India. Mwanamama huyu amewahi kuwa mwanasheria mkuu wa jimbo la California ambaye alijulikana na wanaharakati wa kiliberali kutokana na umahiri wa kuuliza maswali magumu kwa wateuliwa wa nyadhifa mbalimbali zinazoidhinishwa na Bunge, wakati wa uongozi wa Rais Donald Trump.
Harris alimgonga maswali magumu Jaji wa Mahakama ya Juu Marekani Brett Kavanaugh na Mwanasheria Mkuu Jeff Sessions, wakati wa vikao vya Seneti vya kuwathibitisha.
Mwaka 2016 baada ya kuweka historia ya mwanamke wa kwanza mweusi kuwa Seneta Marekani kutoka jimbo la California, aliinuka na kuzibwaga sera na wakosoaji wa "siasa za utambulisho", au “identity politics” ambazo anasema zinatumiwa kama dharau ili kuweka kando na haki za watu kwa kuangalia rangi, jinsia na usawa wa kijinsia.
Ni mwanamama mwenye msimamo na mtetezi wa haki, anatajwa na vyombo vya habari kuwa alikuwa miongoni mwa Wanademocrati ambao walimbana na kumhoji Kavanaugh katika kikao chake cha uthibitisho cha kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu kuhusu maoni yake kwenye utoaji mimba na pia kuhusu uchunguzi wa uwezekano wa Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016.
Katika Seneti Bunge la Juu la Marekani, hajaacha kutetea watu wa hali ya chini. Akiwasilisha muswada wa kuzipa familia za kipato cha chini malipo ya pesa taslimu na mikopo kodi ili kusaidia kupambana na hali ngumu ya uchumi na kupanda kwa gharama za maisha kuanzia makazi.
Amekuwa mtetezi mkubwa wa mageuzi ndani ya haki za binadamu hasa suala la haki jinai.
Haki jinai ni kuwatendea haki na kuwaheshimu watuhumiwa wanaofanya jinai kwa kuvunja sheria, kwa kuamini kuwa hata kama wamekosa na wamekiuka sheria wanahesabiwa kama watenda makosa lakini siyo kufanywa waovu, kuteswa, kutopewa haki zao na kutokuthaminiwa utu wao.
ZIARA AFRIKA
Anapozuru Afrika kwa wiki moja, baadhi ya vyombo vya habari vinasema safari yake inafanyika wakati ambapo Marekani inajaribu kukabiliana na ushawishi wa Urusi na China kwa bara hilo.
Ananukuliwa na AlJazeera, akisema kuwa Marekani itaongeza uwekezaji barani Afrika na kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi , alipoanza ziara yake Ghana.
Ujio wake unalenga kukabiliana na ushawishi wa wapinzani hasa Urusi na China kwa Afrika na kwamba China imewekeza kwa kiasi kikubwa barani Afrika katika miongo ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kufanikisha maendeleo ya miundombinu kama barabara, madaraja na rasilimali, wakati ushawishi wa Urusi pia umeongezeka, ikiwa ni pamoja na kusaidia kukomesha uasi kwa kutumwa askari wa kujitegemea wa Jeshi la Wagner Group katika nchi kadhaa zikiwamo za ukanda wa Sahel mfano Mali na Guinea.
“Katika safari yake anakusudia kufanya kazi katika kuongeza uwekezaji barani Afrika na kuwezesha ukuaji wa uchumi na fursa,” Harris anasema mara baada ya kuwasili nchini Ghana, taifa la kwanza katika safari ambayo itamfikisha pia Tanzania na Zambia.
"Tunatazamia safari hii kuwa kitu muhimu zaidi katika uhusiano na urafiki wa muda mrefu na wa kudumu kati ya watu wa Marekani na wale wanaoishi katika bara hili," anasema Harris. Katika ripoti ya Al-Jazeera.
Utawala wa Rais Joe Biden, unataka kuimarisha uhusiano na Afrika, ili uwe kama mbadala wa mataifa yanayoshindana, huku kukiwa na ushindani wa kimataifa kuhusu mustakabali wa bara hilo sasa.
“Ni ahadi inayokuja wakati huu kwani zama zilizopita zilionyesha kuwa Marekani ina historia ndefu ya kuingilia masuala ya Afrika, ikidaiwa kuwaunga mkono madikteta dhidi ya vuguvugu la ukombozi na kukwamisha maendeleo kisiasa na kiuchumi, lakini pia ikisukuma kwa bidii kufikia masoko na rasilimali za Afrika na kuacha bara hilo bila chochote," ni maelezo ya Shihab Rattansi wa Al Jazeera. anayekaririwa akiripoti kutoka Washington, DC.
“Kwa hivyo Marekani inasema ni mambo ya zamani sasa, Afrika ni washirika, wote tunaweza kufanikiwa'. Tunachosikia kutoka Afrika ni 'hatutaki kuchagua kati ya China, Russia na Marekani. , lakini tutafanya kile tunachohisi ni kwa manufaa yetu.” Inaongeza Al Jazeera.
Kama ya kweli yamekwisha ni zama za kuiona Marekani ikiisaidia Afrika kwa kuwa upo ule msemo wa Marshall Plan kuwa kila fedha yake inayokuja Afrika itarudishwa kwa wingi kuliko ile iliyotolewa kama msaada au mkopo.










