Taifa Stars ambayo ipo Kundi F, linaloongozwa na Algeria iliyopo kileleni baada ya kujikusanyia pointi tisa hadi sasa, inashika nafasi ya pili ikiwa na alama nne ikifuatiwa na Niger yenye pointi mbili na Uganda ikiburuza mkia baada ya kuambulia alama moja tu katika mechi zake tatu.
Ni wazi Algeria ina nafasi kubwa ya kuongoza kundi hilo, hivyo timu tatu Tanzania, Niger na Uganda zina kibarua kigumu cha kuwania nafasi moja ya kuungana na Waalgeria hao kufuzu fainali hizo za Afcon zitakazofanyika nchini Ivory Coast mwakani.
Kwa namna msimamo wa kundi hilo ulivyo, tunaamini kama Taifa Stars itautumia vema uwanja wake wa nyumbani katika michezo miwili itakayocheza Benjamini Mkapa, dhidi ya Uganga na baadaye Niger, inaweza kufuzu kwa mara ya tatu katika historia yake kwenye fainali hizo zenye utajiri mkubwa barani Afrika.
Kinachotakiwa ni wachezaji wa Taifa Stars kutobweteka baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uganda katika mchezo uliopita, kwani hii ni mechi nyingine ambayo wapinzani wao wataingia na mbinu tofauti baada ya kujua uchezaji wao, lakini pia Waganda hao wanatambua kabisa kudondosha tena alama tatu dhidi ya Tanzania kutazidi kuwaweka katika nafasi finyu ya kufuzu fainali hizo.
Hivyo ni wakati sasa kwa Taifa Stars, kusahau matokeo yaliyopita na kuingia uwanjani na mbinu tofauti kabisa kama vile wanakwenda kukutana na timu ambayo hawajawahi kucheza nayo, lakini kila mchezaji atakayepewa dhamana ya kuvaa jezi ya taifa kutambua anawakilisha zaidi ya Watanzania milioni 61.
Tunatambua haitakuwa mechi rahisi hasa kutokana na rekodi nzuri Uganda iliyo nayo dhidi ya Tanzania timu hizo zinapokutana katika michuano mbalimbali, jambo ambalo kila mchezaji anapaswa kuvuja jasho haswa.
Ikumbukwe hii itakuwa ni mara ya 61 kwa Taifa Stars kukutana dhidi ya Uganda (The Cranes), huku Waganda hao wakishinda mara 32, wakipoteza mara 13 tu na sare 15, rekodi ambazo zinaendelea kuibeba zaidi pamoja na kupoteza mchezo uliopita.
Tunachotaka kukiona ni wachezaji wa Taifa Stars kusahau ushindi huo na rekodi mbaya dhidi ya Waganda hao na kisha kushuka dimbani kwa kupambana mwanzo mwisho kwa lengo moja tu la kupata matokeo katika mchezo huo muhimu kwao kabla ya ratiba ijayo kuikaribisha Niger uwanjani hapo.
Tahadhari nyingine tunayoitoa kwa Stars ni kutocheza na jukwaa hasa ikizingatiwa watakuwa wakipata sapoti kubwa kutoka kwa mchezaji wao wa 12 uwanjani hapo, ambao ni mashabiki watakaofurika Benjamin Mkapa kuishangilia.
Hatutarajii kuona mbwembwe nyingi zisizo na maana kwa wachezaji kutaka kushangiliwa na mashabiki, badala yake tunataka kuona mpira ukitembea kwa kasi zaidi kuelekea lango la mpinzani kwa kuwa kinachotakiwa ni matokeo kwanza kabla ya mambo yote.
Lakini pia ni wakati wa mashabiki kununua tiketi kwa wingi na kujitokeza uwanjani kuiunga mkono Stars ili iweze kupata matokeo na hatimaye kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu fainali hizo.









