Korosho hizo ni zilizobanguliwa katika kiwanda cha Amama Farms kilichoko wilayani Tandahimba mkoani Mtwara.
Taarifa hiyo njema imetolewa na Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Amama Farms kilichoko wilayani Tandahimba kinachojishughulisha na ubanguaji korosho.
Mwakalinda Yassin ambaye ni Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, hakuficha hisia zake kwa kuishukuru serikali kwa kuwatufutia soko la korosho Bara la Ulaya.
Kilio cha wakulima cha kupata soko la uhakika sasa kinaweza kuwa kimesikika na hatimaye sasa kuuza korosho zao kwenye kiwanda hicho na kusafirishwa nje ya nchi.
Kiwanda hicho kimekuwa na wawekezaji mbalimbali kutoka nchi za Ulaya ambao wanahitaji korosho zilizobanguliwa kutoka Tanzania na kwamba sasa nchi imewekeza soko la korosho zilizobanguliwa.
Imeelezwa kuwa kuanzia mwezi Januari hadi kufikia mwezi Desemba kwa mwaka huu wa 2022, kiwanda hicho kimeuza korosho zilizobanguliwa kwenda nchi za Ulaya ikiwamo Uholanzi na Marekani zaidi ya tani 414 na kwa uhakika zimesifiwa kwa ubora mzuri.
Zaidi ya tani 26 zilizobanguliwa na kiwanda hicho zimeshapata soko Uholanzi na Marekani na ziko mbioni kwenda moja kwa moja kwenye nchi hizo kipindi hiki cha mwezi Desemba, mwaka huu.
Tanzania kuweza kubangua korosho zake ni jambo la kujivunia kutokana na siku za nyuma kusafirisha nje ya nchi korosho ghafi kwa ajili ya kuchakatwa na kubanguliwa jambo ambalo kwa sasa linafanyika hapa nchini tena wilayani Tandahimba.
Ni jambo la kuishukuru serikali kwa kutafuta soko hilo na kiwanda hicho kilipofikia kimeomba ushirikiano uendelee vyema ili Tanzania iweze kutangazwa kwa soko hili la korosho za kubanguliwa.
Kabla kiwanda hicho hakijaanza ubanguaji korosho, zilikuwa zikipelekwa katika nchi za Vietenam na India ili zikabanguliwe na baadaye isafirishwe kwenda Ulaya kuuzwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, anasema malengo ya bodi hiyo ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini na pia kubangua.
Unapotegemea kuuza korosho ghafi za Tanzania, soko kuu ni nchi mbili pekee ambazo ni India na Vietnam na kama uhitaji ukikosekana katika nchi hizo korosho inakosa soko la uhakika.
Njia pekee ya kupata soko la uhakika wa korosho ya Tanzania ni kubangua na baadaye kupeleka nchi za nje kama wanavyofanya kiwanda hicho cha Amama Farms.
Akipongeza kwa hatua hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Patrick Sawala, anasema kitendo cha usafishaji wa korosho kutoka Tanzania wilayani Tandahimba mpaka nchi ya Uholanzi si tukio dogo ni jambo kubwa na ni fahari kwa Tanzania na Rais wake.
Bodi ya Korosho imefanya kazi kubwa ya kusimamia zao hilo na wakulima kupata tija na kilimo hicho ambacho kwa upande wa serikali imetoa pembejeo.









