Inawezekana ikachukua muda mrefu kwa Afrika kuweza kufikia tena rekodi iliyowekwa au inayoendelea kuwekwa na timu ya taifa ya nchi hiyo.
Mara ya mwisho timu ya Afrika kufika hatua ya robo fainali iliyokuwa ni miaka 12 iliyopita nchini Afrika Kusini wakati Ghana ilipofikia hatua hiyo na ingeweza kwenda nusu fainali kama ilivyokuwa kwa Morocco kama si Luis Suarez kuukamata mpira uliokuwa unaelekea wavuni kwa makusudi na kuzaa penalti ambayo ilikoswa na Asamoah Gyan. Hiyo ilikuwa 2010.
Timu zingine za Afrika ambazo zimeshawahi kutinga hatua ya robo fainali ni Cameroon ambayo iliweka rekodi ya kuwa ya kwanza kufanya hivyo barani humo mwaka 1990, michuano iliyofanyika nchini Italia.
Miaka 12 baadaye, 2002, timu nyingine ya Afrika, Senegal ilifanya hivyo kwenye michuano iliyofanyika nchi za Korea Kusini na Japan.
Hapa tunaona ni miaka 32 sasa imepita ndiyo Afrika imepata timu nne zilizoweka rekodi ya kukumbukwa kwenye michuano hiyo, timu tatu zikitinga robo fainali na moja ikivuka hapo zilipokuwa zinakomea, Morocco ikienda nusu fainali.
Inawezekana ikaonekana kama imebahatisha, lakini ukifuatilia kwa undani unaona kabisa kuwa Morocco kwa sasa ndiyo inatawala soka la Afrika.
Tukianza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, timu ya Wydad Casablanca, kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, bingwa wake ni RS Berkane na Ligi ya Mabingwa kwa soka la wanawake pia ni AS FAR ya Morocco.
Hapo unaona kabisa kuwa hawakubahatisha, ni mpango wa muda mrefu na mfupi ambayo ilipangwa kitaalamu mpaka kufikia hapo.
Tukirudi kwenye Timu ya Taifa ya Morocco, tunaona kuwa wachezaji wake wengi si wazaliwa wa nchi hiyo, badala yake wana uraia wa nchi mbili. Wengi wana uraia pia wa Ufasansa hadi kocha wao na mmoja amekulia Hispania.
Hii tumeiona hata kwenye Timu za Taifa za Comoro na Madagascar kwenye michuano ya AFCON, ambapo waliwaita wachezaji wanaocheza madaraja ya chini tu nchi za nje, lakini walikuja kutetemesha na kuzifanya nchi zao kufanya vema.
Inaonyesha kuwa siku hizi nchi za Afrika kama hawana mpango wa muda mrefu, basi watafanya mipango ya muda mfupi kwenye timu zao za taifa.
Mpango wa muda mrefu ni kutengeneza shule za soka, miundombinu kama viwanja, vifaa vya mazoezi na hata kuwapeleka vijana kulelewa kwenye 'akademi' mbalimbali nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya taifa baadaye.
Kama nchi ikiona inachelewa inawatafuta wachezaji wenye asili ya nchi walio nje ya nchi, kwa sababu wenzetu wana uraia wa nchini mbili na wachezaji wengi hawaitwi kwenye timu za huko wanakoishi, wanaamua kuchezea nchi zao za asili.
Ukiangalia Morocco wanaonekana hawa wana mipango ya aina zote mbili. Ndiyo maana hata klabu zao zinapata mafanikio. Wanatengeneza wachezaji wazuri nchini kwao, lakini wanachukuwa wachezaji nje ya nchi kwa ajili ya kulitumikia taifa.
Hili liwe somo hata hapa kwetu. Tumekuwa hatuna mipango ya muda mrefu, lakini hatuna ya muda mfupi. Timu ya Taifa, Taifa Stars, inaendeshwa zaidi na Kamati za Ushindi na hamasa kuliko uhalisia wa timu yenyewe. Hatuwaandai vema vijana kitaalamu na kuwa washindani zaidi ya kuwa waburudishaji tu.
Nadhani sasa umefika wakati kwa serikali kuangalia uwezekano wa kuwa na uraia pacha hata kwa wanamichezo tu, kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa.
Wale wachezaji wa Morocco kuna baadhi hata nchi yao hawaijua vizuri, lakini sifa zote zinakwenda kwa nchi husika, kwa nini nasisi tusifikirie kufanya hivyo kuwapata wanamichezo tu?
Tanzania ina wachezaji wengi tu nje ya nchi, lakini wanatatizwa na suala ya uraia pacha. Tukumbuke, tukiwapa hao na kuifanyia kazi nzuri Tanzania, sifa itakuwa kwa nchi nzima kama ilivyo kwa Morocco.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







