Yanga ikipambana Tunisia makundi CAF inawezekana

07Nov 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga ikipambana Tunisia makundi CAF inawezekana

KLABU ya Yanga tayari imetua nchini Tunisia tangu Jumamosi wiki hii na kuweka kambi mji wa Sousse umbali wa takriban Km. 140 kufika Jiji la Tunis utakapochezwa mchezo wao wa mkondo wa pili wa mchujo kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club Africain.

Keshokutwa, Jumatano Yanga itashuka katika Uwanja wa Olympique Hamadi Agrebi kuwavaa wenyeji wao, Club Africain, ikiwa na lengo moja tu kupata ushindi ama sare ya mabao ili kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya mechi ya mkondo wa kwanza katika Dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kulazimishwa sare tasa.

Yanga inashuka dimbani huku mashabiki wake wengi nchini wakibaki wamekata tamaa ya timu yao kufanya vizuri katika mchezo huo na kufuzu kutokana na rekodi nzuri ya timu za Ukanda wa Kaskazini, maarufu timu za Kiarabu zikicheza viwanja vya nyumbani.

Pamoja na hofu hiyo kubwa kwa mashabiki, sisi tunaamini hakuna kinachoshindikana kwa Yanga kama wachezaji wakiingia uwanjani kwa ari kubwa na lengo la kupambana mwanzo mwisho kwa dakika 90 za mchezo.

Hiyo ni kutokana na mifano hai ambayo tunayo, mosi ikiwa ni mechi ya michuano hiyo ya CAF mwaka 2003 ambapo mechi ya kwanza Simba ikiwa nyumbani ilishinda 1-0 na kwenda ugenini nchini Misri wenyeji wakapata matokeo kama hayo, lakini Simba ikasonga baada ya kuitoa kwa penalti 3-2.

Mfano mwingine ni mwaka 1979, kwenye michuano hiyo ya CAF, Simba ilikubali kichapo cha mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Mufulira Wanderers ya Zambia na wakati wengi wakiwa wamekata tamaa ilienda ugenini na kupindua matokeo kwa kusonga mbele kwa ushindi wa mabao 5-0, hivyo matokeo ya kikatili katika soka yapo na hilo linawezekana pia kwa Yanga.

Hii inatuonyesha kwamba wachezaji waliamini mechi haijaisha hadi dakika 90 za pili ugenini zitakapomalizika, hivyo kwenda kwa lengo moja tu la kupambania matokeo jambo ambalo linawezekana pia kwa Yanga ambayo inahitaji sare yoyote ya mabao ama ushindi ili kufuzu hatua ya makundi.

Na kama matokeo yatakuwa suluhu, timu hizo zitaingia katika changamoto ya mikwaju ya penalti ambayo siku zote haina mwenyewe, hivyo kinachotakiwa kwa Yanga ni wachezaji kuamini wanaweza huku wakijituma mwanzo mwisho wa dakika 90 za pili nchini Tunisia.

Tunaamini benchi la ufundi na wachezaji wa Yanga wameona ubora na udhaifu wa wapinzani wao hao, hivyo kwa muda wa wiki nzima waliyokuwa nayo, umetosha kufanyia kazi kasoro zao na uimara wa Club Africain ili kupata matokeo keshokutwa.

Lengo letu kama ambavyo tumekuwa tukieleza siku zote pindi klabu za Tanzania zinapoiwakilisha nchini, ni kuona zinasonga mbele na kuliletea taifa sifa lakini pia katika michuano hii ni muhimu kwa Yanga kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kushuhudia watani zao, Simba wakisonga mbele.

Hilo likitokea kwa Yanga, maana yake nchi itakuwa na timu mbili kwenye michuano hiyo ya CAF, hivyo kuiongezea pointi nyingi na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi ya kuingiza timu nne tena kwenye michuano hiyo msimu ujao.

Tunataka kuona suala Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano hiyo ya CAF linakuwa la kawaida kila msimu kama ilivyo kwa Misri, Morocco, Tunisia na nchi nyinginezo, hivyo katika hili hakuna njia ya mkato zaidi ya klabu zetu kupambana zaidi na kufika angalau hatua ya robo fainali, nusu na ikiwezekana fainali kila msimu.

Katika hilo, hatupaswi kuendelea kuitegemea Simba pekee ili kuiongezea nchi pointi kwenye michuano hiyo kwani yapo mataifa mengine mengi yanayoifukuzia nafasi hiyo huku yakiwa na zaidi ya timu moja kwenye michuano hiyo ya CAF, jambo ambalo kama zikisonga mbele zitakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuipiku Tanzania na kujikuta tukirejea kupeleka timu moja Kombe la Shiririkisho na nyingine Ligi ya Mabingwa, hivyo tunaitaki kila la kheri Yanga kufuzu hatua ya makundi kwa maslahi mapana ya taifa.