Kuna watu wana zaidi ya mwezi hawajapata maji ya bomba na tangu taarifa rasmi ya mgawo maji ilipotangazwa, hawajawahi kukumbukwa.
Hali inasikitisha sana kwa sababu baadhi ya watu inawabidi kuamkia usiku mwingi kuyavizia pengine yatatoka, lakini wanaambulia patupu.
Ingawa kuna baadhi ya maeneo katika Jiji la Dar es Salaam, hayajaguswa na tatizo hilo, lakini maeneo mengine limekuwa tatizo la kudumu.
Zaidi ya wiki mbili zilizopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokwenda Kigamboni, alitoa matumaini ya kusambazwa kwa maji yanayozalishwa eneo hilo yaweze kusaidia maeneo yenye shida hiyo, lakini utekelezaji wake haujaonekana.
Sehemu zingine maji yanaweza kutoka nyumba jirani tena usiku wa manane, lakini kwa msukumo mdogo ambao hauwezi hata kujaza ndoo moja ya lita 20. Nyumba nyingine hayajawahi kutoka kabisa.
Wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akitangaza rasmi kuwapo kwa mgawo wa maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, alitahadharisha mgawo huo usiwe wa upendeleo. Wananchi wameshaanza kulalamika kuwa kuna upendeleo.
Inaeleweka kuwa vyanzo vinavyozalisha maji vinaupungufu mkubwa kutokana na ukame uliosababishwa na kukosekana kwa mvua.
Pia, inaeleweka hilo ni tatizo la kimazingira ambalo hata mamlaka zinazosimamia huduma hiyo ziko nje ya uwezo wao, lakini zitafutwe njia mbadala kuwanusuru wale ambao hawapati kabisa maji.
Kuna watu wanaoishi maeneo ambayo nguvu ya kusukuma maji imeongezwa ili mabomba yote yaweze kutoa nishati hiyo, kwanini kwenye maeneo kama ya Boko ambako yanatoka kwa nadra baadhi ya nyumba tena yasiyokuwa na nguvu yasiongezewe nguvu hiyo hata kwa siku moja ili watu wajaze kwenye matangi yao ya akiba na kuondokana na adha hiyo?
Haiingii akilini kuona baadhi ya maeneo maji yanafunguliwa hadi kupotea ovyo, huku sehemu zingine yakikosa huduma hiyo kwa zaidi ya mwezi sasa.
Tafadhali, suala hili liangaliwe ili kuwanusuru watu na adha hiyo. Ikiwezekana hata magari ya kusambaza maji yapelekwe kwenye maeneo yenye shida hiyo wanunue na kuwa na uhakika wa kupata majisafi na salama.
Tatizo hili ni la nchi nzima na linatoa funzo inapopatikana mvua ya kutosha la kuhifadhi maji yaweze kusaidia wakati wa kiangazi.
Maombi kwa waamini wa dini zote ni muhimu ili Mwenyezi Mungu asikie kilo na kushusha mvua.
Ukiangalia baadhi ya maeneo mbalimbali nchini hali inasikitisha kutokana na ukame ulivyokithiri na kusababisha mimea na wanyama kufa.
Hali hii inatoa fundisho kwa watu kuacha kufanya uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo ili kuchoma mkaa na shughuli zingine za kibinadamu.
Maji ni uhai, bila huduma hiyo chakula kitakosekana, njaa itatawala na matokeo yake ni vifo. Inashuhudiwa katika nchi nyingine hali hiyo ilivyoathiri mifugo na wanadamu.
Katika kukabiliana na tatizo la maji uwekwe utaratibu mzuri wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu.










