Usitishaji vibali ujenzi wa vituo vya mafuta mwafaka

11Nov 2022
Mhariri
DODOMA
Nipashe
Usitishaji vibali ujenzi wa vituo vya mafuta mwafaka

KATIKA maeneo mbalimbali nchini hasa kwenye miji mikubwa na ile inayoendelea kukua, kumekuwa na tatizo la ujenzi holela wa makazi pamoja na miundombinu mingine ya huduma, hali ambayo husababisha sharia, kaninu na taratibu za mipango miji kutokuzingatiwa.

Kutokana na hali hiyo kumekuwa na msongamano wa nyumba ambazo hazijapangiliwa hivyo maeneo mengi kuonekana kutokuwa na mpangilio maalum. Hali hiyo imejitokeza katika miji mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Iringa na Morogoro.

Licha ya kuwapo kwa mpangiilio mbovu wa makazi unaosababisha baadhi ya huduma kama barabara na maji kushindwa kupita kwa urahisi, pia kumejitokeza utitiri wa vituo vya mafuta kandokando ya barabara kubwa na zile za kawaida pamoja na maeneo ya makazi ya watu.

Hatua hiyo imesababisha serikali kuagiza kusitishwa kwa utoaji wa vibali vipya vya ujenzi wa vituo vya mafuta kwa muda wa miezi mitatu ili tathmini ifanyike kwa kuhusisha wizara zinazohusika.

 Akitangaza hatua hiyo jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, alisema suala hilo ni moja ya  maelekezo saba ya serikali baada ya kubaini kushamiri kwa ujenzi holela wa vituo vya mafuta, ukiukwaji wa mipango kabambe ya miji na ugawaji holela wa viwanja vilivyopangwa na kupimwa.

Bila kuuma maneno, Waziri Mabula alisema kuna ujenzi holela wa vituo uliokithiri katika maeneo mbalimbali ambao hauzingatii matakwa ya sheria ya mipango miji na kanuni zake huku akiweka bayana kuwa tatizo hilo kwa kiasi kikubwa, liko katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Ni dhahiri kwamba utitiri wa vituo vya mafuta katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani umekuwa ukiongezeka kila uchao jambo ambalo linasababisha kuwapo kwa maswali mengi yasiyo na majibu. Kwa watu wenye uelewa na wasio na uelewa wanapokuta vituo vya mafuta vikijengwa kwa kufuatana, wanaweza kujiuliza maswali mengi yasio na majibu.

Katika barabara kuu ya Dar es Salaam - Morogoro, kwa mfano, kuna baadhi ya vituo ambavyo kutoka kimoja kwenda kingine umbali wake hauzidi hata mita 500 hali inayosababisha jamii kujiuliza kama sheria, kanuni na taratibu za ujenzi huo zinazingatiwa. 

Mbali na vituo katika barabara kuu, hivi sasa kumekuwa na vituo vingi vya mafuta karibu na makazi ya watu. Hali hiyo pia inaibua maswali kama wizara zenye dhamana na mamlaka katika usimamizi wa ardhi na mipango miji, mazingira na nishati zinafuata miongozo iliyowekwa katika utoaji wa vibali kwa ajili ya ujenzi huo.

Kwa mantiki hiyo, swali la kujiuliza ni je, sheria ya ardhi na mipango miji inazingatiwa? Tathmini ya  mazingira inafanyika na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) yenye dhamana ya kutoa vibali kwa ajili ya ujenzi wa vituo inazingatia sheria?

Wahenga wanasema kutenda kosa si kosa bali kurudia. Kwa mantiki hiyo, hatua ya serikali ya kutangaza kusitishwa kwa utoaji vibali inaungwa mkono ili kuepusha majanga yanayoweza kujitokeza kutokana na ujenzi huo ambao umeibuka kwa kasi katika kipindi kifupi kilichopita.  

Ni vyema wizara husika zikakutana na kuweka mambo sawa ili kuwapo na mwongozo sahihi ili kuepusha maafa yanayoweza kujitokeza hasa katika ujenzi wa vituo katika makazi ya watu.