Hersi amesema, wachezaji pamoja na benchi la ufundi walitumia kila mbinu ndani ya uwanja, lakini ilishindikana na kwamba bado wana matumaini ya kufanya vizuri katika mechi ya marudiano.
Amesema, ameona maoni mengi ya mashabiki wao wakitupia lawama kwa benchi la ufundi, wachezaji na hata viongozi, na kudai hiyo ni kuwavunja nguvu wachezaji.
Wachezaji na benchi la ufundi walipambana na anaamini haikuwa bahati kwao, lakini wana nafasi ya kurekebisha makosa yao ndani ya dakika 90 nyingine za kujiuliza watakapokuwa ugenini.
Amesema kinachofanyika hivi sasa ni kuiandaa timu kwa ajili ya mchezo wa marudiano ili kutimiza lengo la kucheza hatua ya makundi ingawa amekiri kuwa mchezo utakuwa mgumu.
Kauli hiyo ya Hersi Nipashe tunaiunga mkono kwa asilimia 100 kwa sababu, tunaamini Yanga ikicheza kwa mbinu, kujituma na bidii ina nafasi kubwa ya kuiondoa Club Africain nyumbani kwao kwenye mchezo wa marudiano nchini Tunisia Novemba 9 mwaka huu.
Tunasema hivyo kwa sababu soka ni mchezo wa makosa na unapofanya kosa moja unaadhibiwa, hivyo Yanga wanaweza kutumia nafasi ya kucheza ugenini kuweza kupata ushindi wanaouhitaji.
Baada ya kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, hivyo inamaana kwamba, sare yoyote ya mabao itaishuhudia Yanga ikifuzu kwenye hatua ya makundi.
Mchezo wa hapa nyumbani haukuwa na mabao yoyote yaliyofungwa, hivyo kama watatoka tena suluhu kule Tunisia, maana yake mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti kama hatapatikana mshindi ndani ya dakika za kawaida na zile za nyongeza.
Hivyo, Yanga kwa namna moja au nyingine matokeo yoyote ya sare ya mabao itawafanya wao watinge moja kwa moja hatua hiyo ya makundi.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, ukiangalia namna mchezo ulivyochezwa hapa nyumbani, ni wazi kabisa klabu ya Club Africain inafungika, kwani Yanga ilitawala mchezo kwa asilimia 63 dhidi ya wapinzani wao hao.
Kama Yanga itacheza kwa kufunguka na klabu Club Africain ikafunguka, kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana mabao mengi kwenye mchezo huo wa marudiano.
Katika mchezo wa kwanza, Club Africain ilicheza kwa kujihami sana na kulinda lango lao, huku wachezaji zaidi ya 9 wakiwa nyuma kuhakikisha hakuna madhara yanayotokea kwenye goli lao.
Kwa sababu watakuwa wakicheza nyumbani kwenye mchezo huo wa marudiano, kwa namna yoyote lazima Club Africain itataka kufunguka ili kwenda mbele kutafuta mabao
Na hapo ndipo Yanga watakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kulishambulia lango la wapinzani wao na kutengeneza nafasi ya kufunga mabao.
Imani yetu ni kubwa kwamba, Yanga inaweza kuvuka katika hatua hiyo, kwani ubora wa wachezaji wake ni mkubwa na walionesha kwenye mchezo wa kwanza kwamba nia na malengo wanayo.
Hivyo wakitumia mbinu za benchi la ufundi pamoja na namna walivyousoma mchezo wa kwanza, tunaamini kabisa wanaweza kufanya lolote ili kupata ushindi ugenini na hatimaye kusonga mbele kwenye hatua ya makundi.
Nipashe tukiwa wadau wakubwa wa soka na pia kwa sababu Yanga inawakilisha taifa kwenye mashindano hayo, tunaitakia kila la heri kwenye mchezo huo wa marudiano na tuna imani wataweza kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Kila la heri Yanga.









