Wakati chama kikiendelea na mchakato huo, tayari kimefuta baadhi ya matokeo ya uchaguzi ukiwamo wa Umoja wa Vijana UVCCM, na kusimamisha mwingine wa Umoja wa Wanawake-UWT kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, miongoni mwa sababu za kufutwa kwa uchaguzi ni ukiukwaji wa maadili, rushwa na upangaji wa safu za uongozi.
Si mara ya kwanza chama hicho kufuta uchaguzi kutokana na sababu hizo, kwani kimewahi kufanya hivyo wakati wa serikali ya awamu ya tano, kitendo ambacho kilitosha makada kuzingatia taratibu za chama na kujifunza.
Wakati wa awamu ya tano CCM, ilifuta matokeo katika kata 41 zilizofanya uchaguzi ngazi mbalimbali, kutokana na kukiuka taratibu za uchaguzi ikiwa ni ishara ya kuelekea kuwa na chama na Tanzania mpya.
Kufutwa kwa uchaguzi huo kulielezwa kuwa ni matokeo ya ukiukwaji wa kanuni na katiba ya CCM, kuendeleza makundi baada ya uchaguzi, kupanga safu za uongozi kwa maamuzi ya nani awe kiongozi, huku ikielezwa jambo hilo ni kinyume na utaratibu na sheria.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa wakati huo Humphrey Polepole, alisema wote waliosababisha kadhia hiyo wangechukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za CCM, wengi walidhani kwamba kufutwa kwa uchaguzi huo kungetosha kuwafunza makada wa chama hicho, kuachana na mtindo huo wa kutofuata taratibu, lakini umejirudia tena mwaka huu.
Ingekuwa ni vyema kama makada hao wangekuwa wanaingia katika uchaguzi kwa kuzingatia taratibu zote za chama na jumuiya zake ili wapigakura wachague viongozi wenye nia ya kukitumikia chama na wale wananchi wanaowakubali.
Imewahi kutokea kwenye uchaguzi ndani ya CCM wakati wa awamu ya tano, baadhi ya maeneo wajumbe wa vikao wa chama hicho kutopewa taarifa sahihi za wagombea na kusababisha kuchagua viongozi wasiokuwa na sifa.
Kwa kuwa chama kinaongozwa kwa mujibu wa katiba na kanuni, makada wazingatie hilo ili kuondoa sintofahamu kama hizo za kufutwa kwa matokeo kutokana na ukiukwaji taratibu na maadili ya chama.
CCM, ni chama kikongwe na tawala, hivyo si vyema baadhi ya wanachama wake wakiharibie sifa mbele ya umma kwa kuingiza mambo ambayo ni kinyume katika uchaguzi wa viongozi, ni wakati wa kukifanya kiwe kioo kwa vyama vingine vya siasa, kwa kufanya mambo kwa utaratibu bila kuingiza 'figisu', ili kuwahamasisha wanaotamani kujiunga wawe na imani nacho.
Ninatambua kwamba CCM ni chama kikubwa, 'figisu' haziwezi kukosekana, lakini pamoja na hayo, jambo la muhimu ni kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki, ili wanachama wapate viongozi wanaowataka.
Rushwa na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za chama visingepewa nafasi badala yake kiendelee kuwa kioo cha vyama vya upinzani, ili viweze kupata mambo muhimu ya kujifunza.
Wakati huo akiwa Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, aliwahi kuonya rushwa ndani ya chama hicho na kusema itakiua na kuwataka wanachama kujiepusha nayo, lakini imeendelea kuwa mwiba hadi leo.
Kufutwa kwa uchaguzi katika maeneo kadhaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ukiukwaji wa maadili, rushwa na upangaji wa safu za uongozi, ni wazi kwamba vitendo hivyo bado vinaishi ndani ya chama hicho.
Hivyo, hata hatua zilizochukuliwa na chama hivi karibuni za kufuta baadhi ya uchaguzi, zingekuwa fundisho la kuwafanya wagombea kurudi kwenye mstari, watafute uongozi kwa kutafuta yaliyomo kwenye katiba ya chama.
Vilevile, ni vyema wale wanaotarajia kuingia kwenye kinyang'anyiro katika ngazi ya mkoa, wajifunze kwa yaliyowakuta wale waliofutiwa uchaguzi, ili katiba ichukue nafasi yake katika kupata viongozi wa chama.



.jpg?itok=nfwjwDzv)






