Jitihada za haraka zinahitajika kunusuru kupanda kwa bidhaa

05Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jitihada za haraka zinahitajika kunusuru kupanda kwa bidhaa

BEI ya mafuta kwa sasa iko juu, imesababisha kuongezeka gharama kwa wananchi na kasi ya ugumu wa maisha kwa kiwango kikubwa kutokana na bei za bidhaa au kwa lugha rahisi mfumuko wa bei.

Juzi, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ilitangaza bei mpya ambazo zimepanda kwa kiasi kikubwa katika historia ya Tanzania, maana yake inakwenda kuathiri moja kwa moja maisha ya Mtanzania wa kipato cha chini.

Kwa mujibu wa EWURA bei ya rejareja mkoani kwa mafuta ya petroli kwa sasa inauzwa Sh. 3,410 kutoka Sh. 3,220, dizeli Sh. 3,322 kutoka Sh.3,143 na mafuta ya taa Sh. 3,765 kutoka Sh. 3,442 kwa lita.

Kupanda kwa bei ya mafuta moja kwa moja kumeathiri Watanzania wengi wanaoishi katika maisha duni ambao wengi wao wanategemea kula mlo mmoja au miwili kwa siku.

Kwa siku ya jana katika masoko makubwa kwenye Jiji la Dar es Salaam kama Soko la Kisutu bei ya bidhaa zilikuwa juu.

Hata katika vyombo vya usafiri nauli zimeongezeka tangu bei ya mafuta ilipoongezeka miezi miwili iliyopita, bodaboda, bajaji, daladala zote zimepandisha nauli.

Suala la kupanda bei za nauli kwa vyombo vya usafiri kupitia ongezeko la bei ya mafuta limeongeza kwa kasi na kusababisha ugumu wa maisha mitaani.

Maumivu ni makubwa kwa watu wenye vipato vidogo na waswahili wanasema, kipato kwa sasa hakikidhi mahitaji, kwa maana ya kuwa kinachopatikana hakimudu gharama za matumizi.

Tunaamini serikali yetu ni sikivu na kilio hiki cha wananchi cha kupunguza makali ya maisha kitasikika.

Kadhalika, tunaamini kwamba ni jambo la heri na muhimu kwa maofisa wa serikali wenye dhamana na suala hili wakaingilia kati, kwani litawasaidia Watanzania wote na hasa wenye vipato vidogo katika jitihada za kumudu mahitaji na kurejesha tumaini jipya la mtaani ambako kuna kundi kubwa la umma.

Imani yetu kwa serikali ni kuharakisha kushuka kwa bei ya mafuta, kwa kuwa hali ni mbaya mtaani kwa kufanya hivyo kutapunguza gharama za maisha na kuongeza mzunguko wa pesa mtaani.

Tunatambua wizarani kuna kitengo cha biashara, ambacho hufuatilia bei za bidhaa kila siku kwenye mikoa mbalimbali na kutoa taarifa, lakini bado haijasaidia kupunguza bei.

Tanzania kuna wasomi wengi wa uchumi wanaoweza kushauri nini kifanyike kuwapunguzia wananchi makali ya maisha, bila kulazimisha wafanyabiashara ambao wanawajibu wa kulipa kodi kupunguza makali.

Kwa nchi zilizoendelea serikali huweka ruzuku kwenye bidhaa ili kuwasaidia wananchi wasiumie na wauzaji wasipate hasara, lakini kwa nchi zetu ni ngumu zaidi ya kufuatilia kwa karibu hali ya soko ili kuona kama bei sio ya maumivu.

Ni wajibu wa serikali kufuatilia kwa karibu hali kwenye masoko na maduka ili kuona bei zinaendana na uhalisia, kwa kuwa wakiachwa kuna uwezekano wa wafanyabiashara kujipanga kuwa na msimamo wa bei ambao unawatengenezea faida kubwa, huku ikiamsha umuhimu wa kuwa na umoja wa walaji na kutetea maslahi ya wengi.

Tunashauri hivyo kwa kuwa uzoefu unaonyesha kuwa katika nchi zinazoendelea hakujawa na uelewa kuhusu mfumo wa soko huru, hivyo tusishangae hata muuza muhogo shambani kwake akipandisha bei kwa kisingizio cha mafuta.