Tangazo hilo la waziri alilitoa wakati akizindua Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Kupitia Taasisi ya JKCI tumeelezwa kuwa serikali imeokoa fedha zilizokuwa zikipeleka wagonjwa kutibiwa nje ya nchi na kuona haja ya kuwafikiria wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo ambao wanashindwa kumudu gharama za matibabu.
Nia hiyo ya serikali inatoa matumaini makubwa hasa kwa wagonjwa wasio na uwezo wa kulipa gharama kubwa na maisha hayo kuwa katika wasiwasi.
Matumaini yetu ni kuona mazungumzo hayo yanazaa matunda na kama alivyosema Waziri Ummy kama mgonjwa akipelekwa nje kwa matibabu serikali inalipia, kwanini wagonjwa wa ndani wasipate pia fursa hiyo.
Wananchi tunasubiri kwa hamu kubwa na tunaombea mazungumzo hayo yanafanikiwe ili kuokoa maisha ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo.
Suala lingine ambalo hatuna budi kumpa kongole Waziri Ummy ni la kutambua umuhimu wa kumpa huduma mgonjwa anayeshindwa kulipia matibabu kwa kumfanyia tathmini ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kipindi wanapositisha huduma.
Umuhimu pia uliotolewa kwa kinamama na watoto hasa kwa kaya duni ambazo zinashindwa kumudu gharama za matibabu pamoja na wazee kwa kutorudishwa nyumbani ni wa kupongeza na kama alivyosema waziri kwa kutofanya hivyo, tunapoteza rasilimali watu.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi, alieleza jinsi taasisi hiyo ilivyookoa mabilioni ya fedha toka ilipoanzishwa kiasi ambacho serikali ilikuwa ikitumia kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi.
Na kwamba taasisi hiyo imeshafanya upasuaji mkubwa wa kifua kwa wagonjwa 2,769 pamoja na mdogo kwa wagonjwa 8,065 toka ilipoanzishwa huku asilimia 85 ya madaktari wanaofanya upasuaji huo ni Watanzania.
Hatua hii ni ya kujivunia kuona madaktari wetu wana uwezo wa kufanya upasuaji huo ambao miaka ya nyuma ilikuwa lazima ufanyike nje ya nchi.
Pia, inajenga imani kubwa kwa Watanzania kuona madaktari wazawa wana utaalamu huo ambao ulikuwa ukifanywa na madaktari wa nje.
Mwenyekiti wa Bodi, Prof. William Mahalu, anawahakikishia Watanzania kuwa jukumu kubwa la taasisi hiyo ni kuondoa au kupunguza asilimia tano ya wagonjwa ambao bado wanalazimika kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu ya moyo.
Kadhalika ni kuhakikisha JKCI itaendelea na utaratibu wake wa kutoa mafunzo kwa mabingwa nchini ili kuongeza huduma za kibingwa ndani na kupunguza gharama kwa serikali.
Watanzania wanamatumaini makubwa na hospitali zao kutokana na kuwa na madaktari wenye uwezo mkubwa ambao pia wanaaminiwa na nchi za nje.
Tunasubiri kwa hamu mazungumzo yatakavyokuja na habari njema ya kuwaokoa wagonjwa wa moyo wasiokuwa na uwezo ili nao waweze kufaidika na fedha za serikali yao.
Mungu ibariki Tanzania