Tanzania ichangamkie fursa lugha ya Kiswahili kiuchumi

08Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tanzania ichangamkie fursa lugha ya Kiswahili kiuchumi

TANZANIA jana iliadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani ambayo pamoja na mambo mengine yamewekwa maagizo kadhaa na serikali juu ya kukuza lugha hiyo ambayo kwa sasa inasambaa kwa kasi duniani.

Kabla ya kuadhimishwa kwa siku hiyo, kulikuwa na makongamano na midahalo yenye mada  mbalimbali katika kuangazia mchango wa Kiswahili katika masuala mbalimbali yakiwamo maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kusaidia mataifa mbalimbali katika harakati za kujikomboa kutoka mikononi mwa wakoloni.

Juzi, kwa mfano, kulikuwa na mdahalo jijini Dar es Salaam kuhusu mchango wa Kiswahili katika ukombozi wa Afrika. Katika mdahalo huo, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, aliliweka bayana kwamba lugha hiyo bado haijaleta matokeo chanya katika maendeleo ya kiuchumi.

Mwanasiasa huyo mkongwe alibainisha kwamba Tanzania ni mwasisi wa Kiswahili na ndiyo inayotumia lugha hiyo kwa kiwango cha juu, lakini cha ajabu haipati fursa za kutosha zinazotokana nayo yakiwamo mapato ya lugha yenyewe. Alisema mapato yanayotokana na Kiswahili duniani ni wastani wa Sh. bilioni 1.3 kwa mwaka lakini Tanzania inaambulia kiasi kidogo.

Sambamba na mapato, fursa zinazotokana na Kiswahili zikiwamo ajira kama vile kufundisha taasisi za elimu ya juu vikiwamo vyuo vikuu zinachangamkiwa na kutumiwa na mataifa mengine yakiwamo jirani kama vile Kenya.

Pia katika idhaa za Kiswahili katika vyombo vya habari vya kimataifa kwa kiasi kikubwa ni Watanzania wachache wanaopata nafasi katika vyombo hivyo. Nafasi zingine ni za wakalimani wengi katika vyombo na taasisi za kimataifa wanatoka kwenye mataifa mengine nje ya Tanzania.

Sambamba na Kinana, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein  Mwinyi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili visiwani humo, aliwataka vijana kutokulala badala yake wachangamkie fursa zinazotokana na Kiswahili badala ya kuachia watu kutoka mataifa mengine.

Ni wazi kwamba kilichosemwa na viongozi hao pamoja na watu wengine walioshiriki kutoa mada au michango katika maadhimisho hayo ni mambo ya msingi. Kuna fursa nyingi za kiuchumi na kijamii zikiwamo ajira kwenye mashirika ya kimataifa lakini ni Watazania wachache wanaothubutu.

Kauli ya Kinana na Rais Dk. Mwinyi zinapaswa kuwa mwangwi wa kuwaamsha Watanzania katika kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza ikiwamo inayotokana na lugha ya Kiswahili.

 Jambo la kujiuliza ni kwamba kutokana na Kiswahili kutumika katika mataifa mbalimbali ikiwamo Umoja wa Afrika (AU), ni Watanzania wangapi wamejitokeza kuchangamkia kazi zinazotangazwa zikiwamo za ukalimani? Hata katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Bunge lake (EALA) ambako makao makuu yako nchini Tanzania mkoani Arusha, ni Watanzania wangapi wanafanya kazi zinazohusiana na Kiswahili?    

Hivi sasa mataifa mbalimbali yamefungua milango katika taasisi zao kuanza kufundisha Kiswahili, hivyo ni wakati mwafaka kwa Watanzania wakiwamo walimu kuchangamkia fursa hizo kwa ajili ya kujipatia ajira.

Ni dhahiri kwamba kama vijana wataanza kuchangamkia nafasi za ajira hususan katika taasisi za kimataifa zinazofundisha au kutumia Kiswahili, tatizo la ajira ambalo limekuwa wimbo usio na mwisho, litapungua.