Klabu zisajili kwa malengo

02Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Klabu zisajili kwa malengo

DIRISHA la usajili kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania, Championship, daraja la kwanza na Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa 2022/2023 limefunguliwa rasmi jana na litafungwa Agosti 31.

Kikubwa kwa sasa ni kuanza kupitia yale mapendekezo ya mwalimu ambayo alitoa kuna yale majalada ya wakati ule wa usajili wa dirisha dogo mahali ambapo hapakukamilishwa basi pafanyiwe kazi.

Pia kwa mwendo ambavyo umekwenda tunaamini kwamba, kila baada ya mechi huwa kunakuwa na vikao vya kamati ya ufundi wanajua tatizo lipo wapi.

Zipo timu ambazo zimeanza kusajili wachezaji wapya na zipo ambazo zimeanza kuwaongezea mikataba wachezaji wao basi iwe ni kwa mapendekezo ya benchi la ufundi.

Yale masuala ya nina mchezaji wangu anajua sijui huyu atatusaidia muda wake umekwisha ni zamu ya benchi la ufundi kufanya kazi.

Ikumbukwe timu nne za juu zina tiketi mkononi ya kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao, michuano ambayo huandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, CAF.

Yanga ambayo ni bingwa wa Ligi Kuu ikifuatiwa na Simba ambazo zitawakilisha nchi kwenye michuano la Ligi ya Mabingwa Afrika, zinapaswa kuzingatia ukweli kwamba zisajili kwa mapendekezo ya mabenchi yao ya ufundi.

Hivyo, kutokana na wakongwe hao wa soka nchini, Simba na Yanga kuwa na uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa, zimekuwa zikihusishwa na wachezaji wengi.

Presha imekuwa kubwa kuanzia kwa mashabiki hadi viongozi wa klabu hiyo, kila mmoja akitaka kuona wanafanya usajili mkubwa wakuvutia kuelekea msimu ujao ambao miamba hiyo inaeleza kupania kufanya vizuri kimataifa.

Kutokana na presha hiyo, Nipashe tunaona kuna uwezekano ikawapoteza viongozi wa klabu na wote waliopewa jukumu la kufanya usajili, wakajikuta wakisajili kwa ushindani wa nani zaidi badala ya kufuata maoni na mapendekezo ya mabenchi yao ya ufundi ili mwisho wa siku waweze kutimiza malengo waliowekewa.

Tumelazimika kukumbusha hilo hasa kutokana na uzoefu mkubwa tulionao katika kipindi cha usajili hususan kwa klabu hizo mbili, ambazo huishia kushindana katika mbio za usajili na mwisho wa siku kujikutana zikisajili wachezaji wengi wa nafasi moja na kusahau mapendekezo muhimu kutoka kwa makocha wao.

Ikumbukwe pia nafasi za kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi ni 12 tu, ambazo ni chache sana, hivyo viongozi wa Simba na Yanga hawana budi kuwa makini kwa kusajili wachezaji katika nafasi muhimu ambao wanaona ni nadra kupata wazawa wakukidhi viwango wanavyohitaji.

Tunataka kuona wachezaji wanaosajiliwa kutoka nje wanakuja kutoa mchango mkubwa kwa klabu hizo na si kusajili wakuja kukaa benchi kutokana na kuzidiwa ama kuwa na ubora sawa na wazawa.

Hivyo, hiki si kipindi cha Simba na Yanga kuanza kukimbizana katika kuonyeshana jeuri ya fedha kuelekea dirisha la usajili, badala yake tunataka kuona kila klabu ikisajili kutokana na mapendekezo ya mabenchi yao ya ufundi ikiwa ni pamoja na wachezaji waliowafuatilia kwa muda mrefu.

Aidha, viongozi wa klabu hizo hawana budi kutumia vema nafasi hizo 12 kwa umakini mkubwa kwa kusajili wachezaji wenye viwango vya juu huku wakimulika kwa umakini historia yao ya majeraha ili kuepuka wale wakucheza mechi moja inayofuata wanakuwa nje ya uwanja wakijiuguza kwa kipindi kirefu.

Tunaamini kama klabu hizo kongwe nchini, zitaacha mashindano katika mbio za usajili na kufuata kile ambacho mabenchi yao ya ufundi yamependekeza, zinaweza kupata wachezaji wazuri watakaowasaidia kwenye michuano ijayo ya kimataifa na kufika mbali.

Lakini lengo letu ni kuona usajili unaofanywa unakuwa wa tija na kuzaa matunda kwa angalau msimu huu tushuhudie timu zaidi ya moja zikitinga hatua ya robo fainali, nusu na hatimaye fainali kwenye michuano hiyo ya CAF, na hilo litawezekana tu kama zitatuliza kichwa kuelekea kipindi hiki cha usajili na si kusajili kwa mashindano.