Wizi huu unahitajika mbadala ulinzi shirikishi

28Jun 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wizi huu unahitajika mbadala ulinzi shirikishi

WIZI majumbani, kupora watu njiani, utapeli unaofanywa usiku na mchana kutumia simu na kwa ujumla kukosekana usalama ni masuala yanayolalamikiwa na wakazi wengi jijini Dar es Salaam.

Mathalani, zipo habari za vikundi vya wahalifu wanaojiita ‘panya road’ hawa wanadaiwa kuibuka na kupora popote na kuwaachia wananchi kilio.

Wapo majambazi wa simu wasio na majina wanaowatumia watu ujumbe wa kutaka pesa kila siku licha ya maelezo ya serikali kuwa namba zimesajiliwa tena kwa kielektroniki.

Wapo wanaofanikiwa kuwaibia mamia ya Watanzania ambao elimu ya utapeli wa simu haijawafikia.

Majambazi wanaoiba kwa kutumia silaha nao wamechachamaa, wanatishia maisha na biashara na wiki iliyopita polisi iliripoti kuua watatu wanaodaiwa walikuwa wanaelekea kuvunja duka la supermarket na kuiba huko Goba Tegeta A jijini Dar es Salaam.

Habari za wizi zinaibuliwa kila kona lakini mojawapo ya taarifa zilizoripotiwa karibuni ni madai ya kuwapo wizi unaofanywa eneo la Mbezi Msumi ambalo sasa ni kama kila nyumba imepitiwa na mali kuibwa.

Msumi ni eneo lililo karibu na Madale, likipakana na Tegeta A na Makabe. Wakazi wengi wa eneo hilo wanalalamikia kuibiwa kwa mfululizo televisheni za kileo maarufu ‘flat screens’, wanaibiwa mapazia na fimbo zake, pamoja funguo za nyumba zao na wezi hao wanaodaiwa kuwa hawana hofu.

Yako madai kuwa familia kadhaa ndani ya muda mfupi mwezi huu wa Juni zimeibiwa kwa utaratibu huo wa wezi kuchukua pazia nyumba nzima, fimbo za pazia hizo, simu, chaja, kuiba vifaa vya ujenzi kama marumaru (tiles), nguo za watoto na mabegi ya shule, kukiwa na hofu kuwa wanatumia dawa za usingizi.

Wapo ambao wameibiwa mpaka vyakula ndani ya friji na walipoamka alfajiri wamekuta milango iko wazi na mbwa wanakula vyakula ndani ya hotpot, vilivyokuwa vimetunzwa frijini.

Wizi huo unadaiwa kufanyika kupitia madirishani kwa kukata mabamba (flat bars) yanayotumiwa kutengeneza madirisha. Mabamba hayo yametumiwa na wengi badala ya nondo yanadaiwa ni mepesi na ni rahisi kukunjwa na kukatwa kwa kutumia ‘plaiz’ au vyuma vingine pamoja na vipande vya nondo.

Ukweli ni kwamba pamoja na kukata madirisha kuna madai kuwa hata funguo bandia zinatumiwa na pia kuna kemikali zinazopakwa kwenye vioo kuvilainisha na kurahisisha kazi ya kuingia ndani kupitia dirishani.

Yanapoelezwa masuala ya wizi mara moja jibu ni ulinzi shirikishi, lakini pia nalo linakwamishwa na hali ya uchumi. Wananchi wa kawaida wanatakiwa kuchangia si chini ya Shilingi 3,000 kila mwezi kwa ajili ya walinzi.

Wenye magari nao huchangia Shilingi kuanzia 5,000 kwa walinzi hao. Ukweli ni kwamba ulinzi shirikishi unakwama, tatizo ni kipato kwenye familia nyingi, hazina fedha.

Hivyo, ni wakati wa kufikiria na kubuni mbinu za kisayansi na kiteknolojia kudhibiti wizi majumbani. Kama kuna taa zinazowakwa kwa ‘sensa’, mageti yanayofunguka kwa teknolojia hiyo, milango inayohisi adui ni vyema serikali, wadau wa utafiti, wabunifu, wafanyabiashara na polisi wanaojua mbinu za kitaalamu za kudhibiti wizi wakaleta teknolojia mbadala ya walinzi shirikishi.

Utaalamu unaweza kuhusisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na taa za nyumba nzima kuzimika pale au kupiga kelele kifaa kinapohisi kuna uharibifu mfano kukatakata madirisha na kushika milango na vitasa au televisheni, ikibidi teknolojia ya alama za vidole nayo itumike.

Aidha, ubunifu unaweza kuelekezwa kwenye kupiga picha na kuzituma kwenye simu za mwenye nyumba, majirani na polisi.

Ni wakati wa kufikiria njia mbadala wa ulinzi shirikishi kupunguza ukubwa na kuzidi kuenea kwa tatizo.