Hiyo ni kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa tena na Klabu ya Simba kwa kufanikiwa kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo kuiongezea Tanzania pointi nyingi na kuwa miongoni mwa timu 12 Afrika zitakazoingiza timu nne kila moja msimu ujao.
Huo utakuwa ni msimu wa tatu juhudi za Simba zinaipa nafasi Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano hiyo ya hadhi ya juu na utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Hata hivyo, licha ya juhudi hizo za Simba katika misimu hiyo miwili, huu na uliopita, ambao Tanzania iliingiza timu nne, bado wawakilishi wengine watatu, wameshindwa kuzitendea haki nafasi hizo kutokana na kutolewa mapema.
Msimu uliopita, ambao Tanzania kwa mara ya kwanza iliingiza timu nne kwenye michuano hiyo, ambazo ni 'wapiganaji' wenyewe Simba, Yanga, Azam na Namungo FC, wawakilishi hao hawakuzitendea haki nafasi hizo.
Mbali ya Simba iliyofika robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa, ni Namungo pekee ambayo ilijitutumua na kutinga hatua ya makundi kabla ya kuishia hapo, wakati ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika huku zingine zikiishia hatua ya wali.
Yanga ambayo nayo ilikuwa ikiiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa iliishia hatua ya awali wakati Azam FC kwenye Kombe la Shirikisho msimu huo nayo iliishia hatua hiyo ya awali.
Msimu huu tena, Simba na Yanga zikabeba jukumu la kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wakati Azam na Biashara United zikiiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Yanga iliishia hatua ya awali wakati Simba iliyoanzia raundi ya kwanza ikashindwa kufuzu, lakini ikanufaika na kanuni za mashindano hayo, hivyo kuangukia mechi za mchujo na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ambapo kwa sasa ipo robo fainali.
Biashara United, ilionesha ni wapi wakongwe Yanga, na Azam FC wanakosea, baada ya kutinga kucheza mechi ya mchujo kuwania kufuzu hatua ya makundi na mchezo wa kwanza nyumbani ikashinda mabao 2-0 dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya.
Hata hivyo, kutokana na uchanga wao uliochangiwa pia na kutokuwa vizuri kiuchumi, Biashara United ilishindwa kwenda Libya kwenye mechi ya marudiano kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukosa kibali cha kutumia anga ya Sudan na Libya kutokana na kuchelewa kuomba kibali kwa shirika la ndege waliyokodi.
Lakini hayo yote yalitokana na hali yao kiuchumi kuwa yakulegalega, hivyo kushindwa kusafiri mapema tayari kwa mchezo huo, jambo ambalo Shirikisho la Soka Afrika (CAF), liliiondoa katika michuano hiyo na tiketi hiyo kuangukia Al Ahli Tripoli ambayo hadi sasa nayo ipo hatua ya robo fainali.
Hivyo, hizi ni nafasi ambazo Shirikisho la Soka nchini (TFF), linapaswa kuwa makini katika kupata wawakilishi wa nchi kwenye michuano hiyo, ambao wataweza kwenda kutoa ushindani na kuzilinda nafasi hizo nne.
Pamoja na utaratibu wa namna ya kuwapata wawakilishi wetu kwenye michuano hiyo ya CAF, sisi tunaona ni wakati sasa TFF ikajikita katika kufanya tathimini ya kina hasa kwa upande wa uwezo wa kiuchumi kwa kila klabu itakayokata tiketi ya kushiriki michuano hiyo, kabla ya kupeleka majina CAF.
Lakini pia tunazitaka klabu zitakazokata tiketi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao, kujitathimini zenyewe kiuchumi na endapo kuna itakayoona ni kina kirefu kutokana na kutomudu gharama, zitoe nafasi hiyo kwa zenye uwezo huo, huku maandalizi yakianza mapema kwa wawakilishi wetu wote ikiwa ni pamoja na kufanya usajili unaolenga zaidi michuano hiyo ya kimataifa.