Kila la heri Simba SC

16Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kila la heri Simba SC

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba, kesho Jumapili watashuka dimbani kucheza mchezo wa robo fainali na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Simba ambayo ndio timu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuendelea kuwemo kwenye michuano hiyo, ilifuzu hatua hiyo kwa kishindo baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya US Gendarmerie ya Niger kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika mechi hiyo ya mwisho ya makundi, Simba ilihitaji ushindi pekee kufuzu hatua hiyo na hicho ndicho kilichotokea.

Kwa kufuzu huko, Simba inaweka rekodi ya kufuzu robo fainali mara tatu ndani ya miaka mitano, mara mbili ikiwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tunaipongeza Simba kwa hatua hiyo kwani inapeperusha vyema bendera ya Tanzania, na hakuna shaka sasa msimu ujao nchi itawakilishwa na timu nne kwenye michuano ya kimataifa.

Pamoja na pongezi hizo, wawakilishi hao wanatakiwa kuingia kwenye mechi hiyo ya robo fainali kwa tahadhari na umakini mkubwa pale kwenye Uwanja wa Mkapa kabla ya kurudiana Aprili 24 mjini Johannesburg.

Haitarajiwi kuwa mechi rahisi kwa vile wapinzani wao pia ni timu bora na yenye uzoefu kwenye michuano hiyo.

Hivyo Simba inahitaji kujipanga vizuri na tunaamini maandalizi ya hali ya juu yaliyofanyika wana nafasi nzuri ya kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo, jambo ambalo hakuna shaka nchi inatamani lifikiwe.

Tunaamini Simba itaibuka na ushindi Jumapili katika mchezo huo na kinachotupa matumaini ni rekodi ambayo imejiwekea timu hiyo inapocheza nyumbani kwenye michuano hiyo na maandalizi ambayo inayafanya.

Katika suala na michuano ya kimataifa kwenye Uwanja wa Mkapa kwa Simba hatuna hofu hata kidogo, tuna uhakika itashinda.

Tuna amini kwa uzoefu wake, hatuoni kama wapinzani wao Pirates kama wataweza kupata hata bao moja kutokana na mikakati iliyopo.

Simba ni tofauti na klabu nyingi za Tanzania, hasa katika mashindano ya kimataifa, hivyo tunawahimiza mashabiki kuondoa hofu na kujitokeza kwa wingi Jumapili kwenda kuishangilia timu.

Umakini unahitajika kuanzia kwa viongozi, benchi la ufundi mpaka wachezaji wenyewe.

Wakati maandalizi ya mechi hiyo yakiendelea, Shirikisho la Soka Afrika, CAF, limetoa taarifa kuwa mechi hiyo ni miongoni mwa zitakazotumia VAR (Video Assistance Referee).

Tunafahamu kuwa hilo ni jambo geni nchini, mara zote maamuzi ya VAR hutumika kwenye Ligi Kuu ya England na michuano mbalimbali ya kimataifa. Simba itakuwa ya kwanza kuonja tamu na chungu ya VAR.

Tunaimani katika maandalizi ya kuelekea mechi hiyo, benchi la ufundi litafanyia kazi hilo na wachezaji wapate kuwa na uelewa zaidi juu ya VAR.

Ni imani yetu Simba imejipanga vyema kufanya yote muhimu kuelekea mechi hiyo na hakuna shaka inayo pia nafasi ya kufanya vizuri.

Hivyo sisi Nipashe tukiwa kama wadau wakubwa wa michezo hapa nchini tunaitakia kila la heri Simba katika mchezo huo na tuna matumaini makubwa kwamba haitawaangusha Watanzania.