Serikali isikubali nauli kupandishwa kiholela

15Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali isikubali nauli kupandishwa kiholela

KIPINDI hiki ambacho ulimwengu unakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo kupanda kwa bei ya mafuta na bidhaa, kimesababisha baadhi ya wafanyabiashara kuanza kupandisha bei za bidhaa na gharama za huduma.

Kupanda kwa bei ya mafuta na baadhi ya bidhaa kumechangiwa na vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine, ambazo ni wazalishaji wa mafuta na bidhaa nyingine, ikiwamo ngano.

Serikali imekuwa ikitoa taarifa kuhusiana na hali hiyo ngumu ya uchumi, huku ikitaja hatua mbalimbali inazojaribu kuzichukua kuhakikisha kwamba wananchi wanapunguziwa makali hayo.

Kadhalika, imekuwa ikitoa angalizo kwa wafanyabiashara kutopandisha bei ya bidhaa na huduma kiholela kinyume cha uhalisia, ingawa inashuhudiwa baadhi wakiendelea kuitumia fursa hiyo kupandisha bei.

Ni kweli kwamba kupanda kwa bei ya mafuta kunaathiri baadhi ya bidhaa, lakini hatukubaliani kabisa na baadhi ya bidhaa kupandishwa bei kwa kisingizio cha bei ya mafuta, kwa sababu hazihusiani kabisa na mafuta.

Hivi sasa kuna shinikizo kubwa kutoka kwa wasafirishaji wa abiria kwa maana ya mabasi ya daladala na mabasi yanayokwenda mikoani kutaka kupandishwa bei ya nauli kutokana na sababu hiyo hiyo, ingawa mapendekezo yao ya viwango vya nauli wanayopendekeza hayana uhalisia na hali halisi.

Mapendekezo ya viwango vya nauli yaliyotolewa juzi wakati wa mkutano wa wadau wa usafirishaji na serikali uliofanyika jijini Dar es Salaam ni uthibitisho kwamba hayakufanyiwa utafiti wa kina kabla ya kuyawasilisha hadharani.

Tunasema hivyo kwa sababu viwango vya kauli wanavyovipendekeza vikikubaliwa, wananchi wengi watashindwa kuvimudu kutokana na hali halisi ya uchumi na vipato vyao.

Katika mkutano huo wa wadau hao waliiomba serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kupandisha bei za usafiri wa daladala na mabasi ya kwenda mikoani kwa maelezo kuwa gharama za maisha zimepanda.

Wanapendekeza nauli kuongezaka kwa asilimia 34 hadi 54 kwa mikoani, huku kwa mijini kilometa 10 iwe Sh. 745.00, kilometa 15 (Sh. 1,117.40), kilometa 20 (Sh. 1,490), kilometa 25 (Sh. 1862.50) na kilomita 30 (Sh. 2235).
 
Chama cha Wamiliki wa Mabasi nchini (TABOA), kinasema nauli za mabasi yaendayo mikoani zinazotumika kwa sasa zina zaidi ya miaka tisa  wakati gharama za vyombo vya usafiri, ilikuwa ndogo, hivyo kuna haja ya kuzibadilisha kwa kuwa sasa zimepanda.
 
Kwamba imekuwa chini kwa muda mrefu kwa sababu mara ya mwisho nauli zilirekebishwa mwaka 2013, na kwamba gharama za maisha zimepanda ukilinganisha miaka hiyo na sasa. Inasema kipindi hicho dola moja ilikuwa ni sawa na Sh.1,596 wakati leo hii dola moja ni Sh. 2,345.
 
Sababu nyingine TABOA inadai gharama za kununulia mabasi nazo zimepanda ukilinganisha na kipindi cha nyuma hadi kufikia Sh. miioni 400 kutoka Sh. milioni 200 kwa mabasi yanayotoka China huku kwa Marcopolo zimepanda hadi Sh. milioni  700, hivyo kuziomba mamlaka kupandisha ili kuendana na kasi hiyo.
 
Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA), wanadai kwa umbali wa kilometa 10 nauli iwe Sh. 745.00, kilometa 15 (Sh. 1,117.40), kilometa 20 (Sh. 1,490), kilometa 25 (Sh. 1,862.50), kilomita 30 (Sh. 2,235), huku wakipendekeza wanafunzi walipie nusu ya gharama hizo.
 
Hata hivyo, Chama cha  Kutetea haki za Abiria Taifa (CHAKUA), kilieleza kuwa wakati  wadau wa usafiri wanajadili kupandishwa nauli wafirikirie pia suala la kuboresha utoaji wa huduma hizo kwa sababu kwa sasa sio nzuri.
 
Kilisema watu wanakata ruti, sehemu ya nauli ya chini wanapandisha, ya nauli ya juu wanapunguza hawaeleweki, na kusisitiza abiria na watoa huduma kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Kimsingi, viwango vilivyopendekezwa ni vikubwa mno, visivyozingatia uhalisi wa hali za wananchi na hivyo tunaishauri kama itaona kuna sababu za msingi, ipandishe nauli mpya kwa kuzingatia uhalisia.