Serikali ipunguze matumizi kusaidia wananchi

14Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali ipunguze matumizi kusaidia wananchi

BEI ya mafuta ya magari imepanda kwa kiasi kikubwa katika historia ya Tanzania, hali iliyosababisha bidhaa nyingine kupanda na kuwapo mfumuko wa bei, hali inayoathiri maisha ya wananchi wa kawaida.

Wengi wamepaza sauti kuitaka serikali ibane matumizi ili iweze kuingiza ruzuku kwenye mafuta yashuke bei na kudhibiti mfumuko, lakini serikali imekuja na mkakati wa kupunguza kodi ya ndani kwenye baadhi ya bidhaa, huku ikionya wafanyabiashara wanaotumia mwanya huo kupaisha bei.

Tunatambua kazi nzuri iliyofanywa ya kuja na mkakati wa kupunguza kodi na kufuatilia wafanyabiashara wanaotumia mwanya huo kupandisha bei, lakini tunaona hizo bado hazitoshi, ni muhimu kwa serikali kuangalia matumizi yake ya kila siku, ili kuwasaidia wananchi kupunguza makali ya maisha.

Pamoja na jitihada hizo, kuna mambo ya msingi ambayo ni lazima serikali iyaangalie ikiwamo kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ambayo kwa sasa yanaonekana yakianza kurejea, jambo linalozua minong’ono kwa walipa kodi.

Mathalani, hafla za kitaifa zinaongezeka na viongozi kukusanyika eneo fulani kwa ajili ya jambo fulani, utengenezaji wa fulana, kofia na kanga kwenye shughuli hizo umerejea na watu kutumia mwanya huo ‘kupiga’ fedha.

Kunapokuwa na halfa ya kitaifa inayohuduriwa na viongozi wa kitaifa maana yake watakuwapo wa mikoa, wilaya, taasisi mbalimbali na walinzi wao ambao watatakiwa kulipwa posho za kujikimu, magari na watoa huduma kama za chakula, vifaa vya umeme na mabango mbalimbali, vyote hivyo vinahitaji fedha ambazo huenda hazikuwa kwenye bajeti.

Viongozi wengi ni wenye hadhi ya kusafiri kwa ndege na wengine magari yao ambayo hutumia mafuta mengi, maana yake kwa mwezi kukiwa na hafla kama hizo kumi yote ni matumizi makubwa ambayo yanatokana na kodi za wananchi.

Semina, makongamano na mikutano yenye kukusanya viongozi wengi inaifanya serikali kuongeza gharama ambazo zinabebwa na wananchi kupitia kodi zao.

Kama haitoshi kuna gharama za mavazi na muda wa maongezi kwa viongozi wa hadhi fulani, huku wengine wakilipiwa hadi wasaidizi wa nyumbani na sehemu nyingine, yote haya ni matumizi ambayo yangeweza kuzuiwa ili yasaidie wananchi kupunguza makali ya maisha.

Ni kawaida kwa fedha nyingi kuelekezwa kwenye mishahara na matumizi mengineyo, ikiwamo posho na chai za watendaji kuliko kwenye miradi ya maendeleo, jambo ambalo linatufanya tuzidi kurudi nyuma badala ya kuwekeza kwenye huduma muhimu za kijamii.

Katika dunia ya sasa yenye maendeleo ya teknolojia, kalenda za kutundika ukutani hazina umuhimu kwa sababu kwenye simu janja hata vitochi, zinapatikana.

Ni lazima serikali ifanye tathmini kwa kupunguza matumizi makubwa ambayo yanaonekana bila kutajiwa kiasi cha fedha kilichotumika kama hafla nyingi, makongamano, semina na mikutano, kutengeneza vipeperushi.

Kama ingekuwa inawekwa wazi matumizi ya safari za kwenda kwenye kusanyiko fulani kwa viongozi wa kitaifa hadi wilayani, kwa mwezi ni matumizi makubwa ambayo tunaamini yangeelekezwa kusaidia wananchi kupunguza makali ya maisha tungeona mabadiliko.

Pamoja na mikakati iliyotangazwa na serikali ya kupunguza kodi, lakini ni muhimu tuone hata viongozi na serikali kwa ujumla inapunguza matumizi, inapoonekana hali ni ile ile wananchi wanaona wako wenyewe katika kukabili hali ngumu waliyonayo.

Tunaamini kwenye kubana matumizi kutaokoa fedha nyingine kupotea, na zitakwenda kuwasaidia wananchi kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo kuiwezesha serikali kuondoa Sh. 100 kwenye kila lita moja ya mafuta ili angalau bei ishuke.

Kwa sasa wasafirishaji wanataka nauli zipande kwa kuwa gharama za uendeshaji zimepanda, jambo ambalo halikwepeki na ikiwi hivyo maana yake gharama za maisha zitazidi kuongezeka na haijulikana vita itaisha lini, na hata ikiisha kutakuwa na kazi ya kushughulikia matokeo ya vita husika.