Tunaweza kuepuka Man, Barcelona za Tanzania

09Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tunaweza kuepuka Man, Barcelona za Tanzania

MPIRA wa miguu ni mchezo maarufu, si Tanzania pekee bali dunia nzima. Umaarufu wa Ligi Kuu ya England (EPL) umevuka mipaka ya nchi hiyo, ambao ni faida kwa klabu kubwa za England.

Klabu kubwa za England zimekuwa zikitumia vizuri wingi huo wa mashabiki hasa katika bara la Asia kwa kufanya ziara za maandalizi ya msimu mpya.

Ukizungumzia mechi za televisheni, ni zile za EPL ndizo zinazoongoza nchini kwa mashabiki kufurika katika maeneo mbalimbali kila mechi zinapochezwa, tena nyingine hushuhudiwa usiku mkubwa.

Ziara hizo mbali ya kuwa sehemu ya maandalizi ya timu lakini pia hutumika kwa kuuza vifaa mbalimbali vya timu kama jezi.

Kutengeneza wigo wa washabiki si kitu kidogo wala cha mzaha. Ukifuatilia historia ya klabu nyingine za England na sehemu nyingine duniani utabaini kuwa zimetumia muda mrefu kutengeneza washabiki kutokana na ukweli kuwa kuna klabu nyingi huko kwao.

Nyingi ya klabu hizo zimeasisiwa karibu au zaidi ya karne moja iliyopita, na sasa zimekuwa taasisi kubwa, tena si tu katika kucheza mpira wa miguu, bali heshima ambayo zimejijengea.

Hapa Tanzania tuna klabu kongwe na zenye wafuasi wengi za Simba na Yanga. Klabu hizi za Dar es Salaam zimeanzishwa zaidi ya miaka 80 iliyopita. Kimsingi klabu hizi ni za aina yake, kwani zina hazina ya washabiki.

Wakati klabu nyingine zinafikiria na kujipanga kwa ajili ya kutengeneza wigo wa mashabiki, zenyewe zina wafuasi wa kutosha. Wafuasi ni zaidi ya mashabiki, kwani hao wameshaamini katika Yanga na Simba. Huwezi kuwabadili kutoka kushabikia timu hizo.

Hawa iwe ni wafuasi, mashabiki au wanachama tu wao hawazitazami klabu zao katika mwelekeo mwingine zaidi ya ushindi. Kwao maendeleo katika klabu ni ushindi tu, iwe kiwango cha mchezo unaochezwa ni mbovu lakini kinatoa matokeo wao hilo si tatizo.

Ni historia kwa sababu sasa hivi ukikutana na mfuasi wa Yanga au Simba mwenye umri wa miaka 50 hawezi kukupa sababu yenye mantiki ni kwa nini alifikia kuipenda klabu anayoishabikia.

Lakini leo ukifuatilia kwa karibu utabaini kuwa si mashabiki tu, bali Tanzania kuna timu zinaitwa Manchester United, Arsenal, Liverpool, Barcelona, West Ham, Real Madrid, Real Zaragoza, AC Milan, Inter Milan, Panama na nyingine, na zinacheza ligi zetu.

Kimsingi ili timu iweze kucheza ligi yoyote rasmi- ile inayotambuliwa na chama cha mpira wa miguu cha wilaya, chama cha mpira wa miguu cha mkoa au Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni lazima iwe imesajiliwa.

Ni vizuri wasajili wetu na hata waanzilishi wa Manchester United ya Tanzania wakafahamu kwa nini hiyo ya England imeitwa Manchester United, ile ya Hispania inaitwa Barcelona au ile ya Italia inaitwa AC Milan.

Sisi Nipashe tunaona kwamba, jambo la kwanza ambalo tunatakiwa kufahamu ni kuwa majina kama Manchester, Barcelona, Madrid, Milan, Tottenham, Blackburn ni miji au vitongoji katika nchi hizo za Uingereza, Hispania na Italia.

Hivyo, klabu hizo mara tu zilipoanzishwa zilianza kuwa na washabiki katika maeneo yao kwa sababu majina tu yanawakilisha miji husika. Mbeya City au Musoma Shooting zina uhalali wa kujitengenezea washabiki katika miji hiyo kwa sababu hiyo niliyoitaja hapo juu.

Tunaona kwamba, sasa ni wakati kwa Ofisi ya Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini wakati wa kusajili klabu kuangalia zaidi ya malengo na madhumuni katika katiba za klabu zinazoomba kusajiliwa. Maana ya majina ya klabu husika nayo iangaliwe.