Rais ameshaagiza, sasa kazi kwenu

23Mar 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Rais ameshaagiza, sasa kazi kwenu

KILIO cha watu wengi kimesikika, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuagiza kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau kuhusu muundo wa tume huru ya uchaguzi.

Alitoa agizo hilo Ikulu, jijini Dar es Salaam juzi wakati akipokea taarifa ya kikosi kazi chenye wajumbe 25, kilichoongozwa na Mwenyekiti wake, Rwekaza Mukandala.

Rais alisema kuwa wajumbe hao wanatakiwa kuangalia maeneo kadhaa, ikiwamo maana na tume huru, iweje, pia kuangalia mifano ya waliokuwa na tume hizo kama wana migogoro au hawana, pia jinsi wanavyoziendesha.

Pia Rais Samia akaagiza kuboreshwa uhusiano baina ya vyama vya siasa na vyombo vya habari, ili kuwa na uhusiano wa karibu muda wote badala ya kuwaandika ifikapo kipindi cha uchaguzi pekee, lakini miaka minne inayobaki wanakuwa hawana uhusiano wa karibu kama ule wa mwaka wa mwisho wa uchaguzi unapokuja.

Kwanza, nimpongeza Rais Samia kwa kuruhusu kikosi kazi hicho kuanza kuratibu maoni kuhusu muundo wa tume huru.

Ni kitu ambacho kimekuja kwa muda mfupi mno na haikutarajiwa. Baadhi waliona ni kama hakitowezekana, au kitakuja baada ya muda mrefu baadaye.

Rais ameshatoa agizo na amemaliza kazi yake, sasa kilichobaki ni waliopewa jukumu hilo kutulia na kuanza kuratibu na kukusanya maoni taratibu ili yakirudi yawe si ya wanasiasa peke yake, bali ni ya wananchi wote, wenye faida kwa watu wote nchini na utamaduni wa Kitanzania.

Wafanye haraka haraka ili wamalize upesi kwa sababu fursa iliyosubiriwa kwa muda mrefu imepatikana, la hasha, ila watulie na warudishe maoni ambayo yakianza kufanya kazi yafanye kwa muda mrefu bila tena kuanza manung'uniko na mlalamiko, kuwa kuna mapungufu.

Kama alivyosema Rais, ni kwanza kabisa waanze kuangalia maana ya hiyo tume itakayoundwa, baadaye waangalie iweje, yaani muundo wake na waangalie mifano ya waliokuwa na tume hizo na jinsi wanavyoziendesha.

Kikosi kazi hicho sasa kinachotakiwa kuwa makini ni pale kwenye migogoro. Kama wana migogoro aliyobainisha Rais, wao watachotakiwa kuangalia hapo inasababishwa na nini, kwa sababu gani na hata kuainisha au kuangalia jinsi gani tume itakavyojiepusha na migogoro ambayo wenzetu wanayo.

Ni vizuri kwamba, wameanza na sisi tunaangalia wale ambao wameshapitia huko, hivyo tuna uwezekano wa kuwa na tume huru ya uchaguzi nzuri zaidi kwa sababu tutaona na kurekebisha mapungufu ambayo wenzetu wanayo.

Hii ndiyo fursa adhimu ambayo Rais ameitoa na haipaswi kufanyiwa masihara hata kidogo. Ni nadra sana kupatikana.

Kikosi kazi hicho sasa kinatakiwa kuangalie kwenye maeneo yote, na kisiegemee kwa wanasiasa pekee ambao ndiyo walioonekana au wanaoonekana kuhitaji zaidi tume hiyo kuliko kada zingine.

Ndiyo, wanasiasa wana upande wao kwenye hili, lakini iangaliwe pia, sehemu ya wapigakura ambao nao wanadamka asubuhi kwenda kushinda vituoni na kupiga kura kumchagua kiongozi anayempenda.

Kwenye hili pia mpigakura naye aangaliwe kwa jicho la pekee, ili kuwapa hamasa au hamu wananchi kwenda kupiga kura, kwani inaonekana kama kila miaka inavyozidi kusonga mbele wapigakura wanaanza kupungua.

Kikosi hicho kije na mapendekezo ambayo yanaweza kumfanya mpigakura hasa vijana ambao ndiyo kada inayodaiwa bado haijahamasika sana kupiga kura, kujiona wana umuhimu kwenda kumchagua kiongozi anayempenda, na si kuwaachia wazee tu.