Bravo Wizara ya Elimu ushirikishaji wa wadau

11Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Bravo Wizara ya Elimu ushirikishaji wa wadau

JANA Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekonolojia, imesema imekamilisha uundaji wa mfumo wa kusahihisha mitihani, ambao utaanza na ya walimu wa vyuo vya ualimu, lengo likiwa kuepuka udanganyifu.

Mfumo huo ambao ni wa kwanza Afrika, umegharimu zaidi ya Sh. milioni 550, umeundwa na Watanzania wenyewe, jambo lililowezesha kupunguza gharama. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, anasema mfumo huo utasaidia kupunguza au kumaliza udanganyifu kwenye mitihani kwa kuwa anayesahihisha swali moja hatajua anasahihisha mtihani wa nani kwa kuwa hataona namba wala jina.

Alisema baada ya kusahihisha utakwenda kwa anayekagua, anayehakiki na baadaye kuwekewa alama, na kwamba wanaamini kwa utaratibu huo mfumo utadhibiti udanganyifu.

Alisema kwa sasa mfumo utafanyiwa marekebisho kwa kusahihisha mitihani ya walimu wa vyuo vya ualimu na baadaye utasambazwa maeneo mengine, ili kujiridhisha kama inafanyakazi kwa ufanisi unaotakiwa. Alisema lengo ni kuziba mianya yote na kuhakikisha wanaofaulu wanakuwa ni wale waliofanya vizuri inavyotakiwa, na siyo kwa sababu wamesahihishiwa ndivyo sivyo.

Kuvuja kwa mitihani au udanganyifu kwa kuwafaulisha wasiostahili ni hatari kwa taifa kwa kuwa linazalisha watu wasio na sifa zinazotakiwa kwa kuwa walishinda mitihani kwa mbinu chafu, ndiyo maana kumekuwa na jitihada nyingi za kudhibiti ili kutoharibu ubora wa mfumo wa elimu ya nchi.

Tunapongeza sana jitihada za Baraza la Mitihani la Taifa ( NECTA) kuunda mfumo huo zikiwa ni jitihada za kukdhibiti vitendo vya ovyo vya udanganyifu, ambavyo vimewachochea vijana wetu shuleni na vyuo vilivyoko chini ya NECTA kujiingiza katika mbinu chafu wa wizi wa mitihani badala ya kujiamini na kusoma kwa bidii.

Tunatarajia kuwa jitihada zaidi ikiwamo kubuni mifumo mingine ya kudhibiti udanganyifu katika mitihani unatakuwa endelevu, ili kuhakikisha wanapatikana wahitimu wanaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa. Bila hatua, tunaweza kujikuta tukizalisha taifa la wahitimu wajinga badala ya walioelimika na wenye viwango, hivyo kusababisha watu wetu kushindwa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya Tanzania.

Jitihada nyingine za wizara ni kufanya mabadiliko ya mitaala na sera za elimu nchini, ili kuhakikisha inaendana na mabadiliko ya dunia, kuacha utaratibu wa kukaririsha wanafunzi bali waweze kujiajiri watakapomaliza.

Waziri anakiri kuwa mfumo wa elimu uliopo sasa unamfanya mwanafunzi kukariri zaidi, anajifunza mambo mengi ambayo kimsingi hayamsaidii kwenye maisha yake, na ndiyo maana kumekuwa na wahitimu waliofaulu vizuri, lakini wanapofika kazini wanashindwa kufanya vizuri. Tunapongeza utaratibu wa sasa ambao utashirikisha wadau wote muhimu, ikiwamo sekta binafsi katika kujadili mitaala na sera, ili ipatikane nyaraka ambayo ni shirikishi kwa Watanzania wote.

Aidha, tunaridhishwa na uamuzi wa kuwa na rasimu ya kupeleka kwa wadau ambayo inaandaliwa na timu ya wataalamu, itawasilishwa kwenye kongamano la wadau litakalofanyika Mei mwaka huu.

Pia, tunapongeza msimamo wa waziri kuwa mabadiliko mbalimbali ya elimu hayatafanywa na wataalamu pekee kujifungia kwamba wanajua kila kitu, utakuwa shirikishi jambo ambalo lilikosekana kwenye mfumo wetu wa elimu na kuachwa kuwa maamuzi ya waziri na wataalamu wake na ndiyo maana tuliona kuna wakati michezo, masomo ya michepua ya kilimo na biashara yaliondolewa.

Mamlaka ya waziri kufanya mabadiliko ya mfumo wa elimu bila kushirikisha wadau kuiumiza na kuyumbisha sekta hiyo, hivyo ushirikishaji wa sasa unaleta matumaini.

Tunapozungumzia mitaala na mitihani ni jambo muhimu kwa mustakabali wa nchi, linahitaji umakini , ndiyo maana tunasema jitihada ziendelee kuhakikisha kinachopatikana ndicho kitaongoza elimu ya nchi hii kwa miaka mingi ijayo.

Kwa muda mrefu kumekuwa na kiu ya kufumua mfumo wa elimu kwa kuwa haukidhi mahitaji ya sasa na utakapofumuliwa maana yake inatakiwa kupata nyaraka za kuongoza kwa miaka mingi.