Takwimu za vifo, wagonjwa zitahamasisha chanjo corona

28Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Takwimu za vifo, wagonjwa zitahamasisha chanjo corona

SERIKALI imeendeleza hatua za kuihamasisha jamii kujitokeza kupata chanjo ya ugonjwa wa UVIKO-19, baada ya kutamka kwamba kuanzia sasa itakuwa inatoa takwimu za wagonjwa na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ndiye aliyetoa tamko aliyeangazia uamuzi huo mkoani Dar es Salaam juzi , akisema lengo ni kutaka kutambua umuhimu wa chanjo, ingawa ni hiari.

Ummy alisema hayo wakati wa kupokea chanjo 800,000 kutoka Serikali ya China, aina ya Sinopham ambayo itatumika kuchanja watu 400,000 dozi mbili.

Alisema hadi sasa chanjo zilizokwishapokelewa ni 8, 821,210 ambazo zinatosha kuchanja Watanzania, 5,082,380 na kwamba hadi juzi waliochanjwa ni 1,922,019 sawa na asilimia 3.33, tangu zilipoanza kutolewa mwaka jana aina ya Moderna, Jansen, Pfizer na Sinopham.

Alisema mwitikio wa kuchanja nchini bado ni mdogo wakati lengo ni kufikia asilimia 60 hadi mwishoni mwa mwaka huu.

Alisema ili kuongeza hamasa, kuanzia sasa serikali itakuwa inatoa takwimu za wagonjwa wanaougua na idadi ya vifo kutokana na ugonjwa huo, ili taarifa hizo zipimwe na jamii na kutambua umuhimu wa chanjo, ingawa bado serikali inasisitiza ni suala la hiari.

Ni ukweli usiopingika kwamba kasi ya Watanzania kuchanja ni ndogo kwa sababu asilimia 3.3 haiendani na muda ambao chanjo hiyo ilianza kutolewa nchini Julai mwaka jana.

Tunadhani kwamba taarifa mbalimbali za upotoshaji zilizokuwa zikitolewa ziliwafanya watu wengi kuamini kuwa ugonjwa huo hauko Tanzania sambamba na kuaminishwa kuwa chanjo ina madhara.

Suala lingine ambalo limechangia watu kusuasua katika kupata chanjo ni kutotolewa takwimu za vifo na wagonjwa, hivyo kuwafanya watu kutochukua hatua za tahadhari dhidi ya maambukizi.

Nchi nyingi zikiwamo za jirani zilianzisha utaratibu wa kutoa takwimu hizo kila siku, na hakika ilisaidia raia wake kuelewa kwamba kuna ugonjwa huo na watu wanaugua na wengine kufa.

Ingawa hata hivyo imechelewa, lakini tunaona kwamba serikali imefanya jambo hilo jema kwa lengo la kuijulisha jamii ukubwa wa tatizo za UVIKO-19 na hatua za kuchukua, ikiwamo kwenda kupata chanjo.

Katika moja ya nchi jirani, watu takribani milioni 10 walikuwa wamepata chanjo ya UVIKO-19, kwa mujibu wa takwimu za wiki mbili zilizopita, hali ambayo inadhihirisha kuwa utoaji wa takwimu unasaidia kuwahamasisha watu kuchanja.

Utaratibu wa utoaji takwimu za vifo na wagonjwa una lengo zuri la kuihamasisha jamii na si vinginevyo. Tunasema hivyo kwa kuwa kuna wanaoweza kupotosha kwamba kufanya hivyo ni kuwatia woga wananchi.

Tanzania sio kisiwa, hivyo inapaswa kushirikiana na mataifa mengine duniani katika masuala mbalimbali, ikiwamo mapambano dhidi ya ugonjwa huu ambao unaendelea kuleta majanga.

Kama alivyosema Waziri Ummy, bado kuna haja ya kuendelea kutolewa hamasa na elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chanjo hii ili kufikia malengo ya kuchanja asilimia 60 ya Watanzania ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Viongozi wa serikali, taasisi na wa dini ni vizuri wakaendeleza hamasa kwa Watanzania kuchanja, ili kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19.