Miundombinu yenye thamani fedha muhimu

21Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Miundombinu yenye thamani fedha muhimu

JANA katika gazeti hili ilichapishwa picha ya mwananchi mmoja akipita kwenye nguzo zilizowekwa mbadala baada ya daraja linalounganisha eneo la Mwembe Kiboko Kata ya Kinyerezi na Kifuru Tabata, mkoani Dar es Salaam, lililoharibiwa na mvua na kusababisha hatari na usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo, ...

hasa wazee na watoto.

Picha hiyo inaonyesha tabaka la juu ya barabara hiyo limeondolewa na maji, huku kalavati zikibaki na sasa jinsi ya kupita ni vigumu na hatari kwa watumiaji.

Tunatambua jitihada za serikali kuboresha miundombinu ya barabara kuhakikisha inapitika kipindi chote cha mwaka, katika kuwawezesha wakulima, wafanyabiashara na wananchi wengine kusafirisha mazao na bidhaa.

Katika Bunge la Bajeti la mwaka jana, wakati wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, kila mbunge aliyesimama kuchangia bajeti hiyo alieleza namna gani miundombinu ni tatizo kwa kuwa barabara nyingi hazipitiki wakati wote wa mwaka.

Baadhi ya wabunge walieleza kilio chao kwenye madaraja ambayo hujengwa na kuzolewa na maji ya mvua ndani ya muda mfupi, kiasi cha kukata mawasiliano kati ya eneo na eneo, wilaya na wilaya, mkoa na mkoa.

Mathalani, mwaka jana mwanzoni eneo la Kiyegeya barabara ya Morogoro hadi Dodoma, daraja lilizolewa na mvua kiasi cha wasafiri kuteseka kwa muda mrefu.

Kutokana na tukio hilo, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), alieleza kuwa madaraja ya barabara hiyo yana miaka 40 hayajawahi kufanyiwa matengenezo na kwamba yanahitaji kukarabatiwa.

Tunapongeza jitihada za ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja ambayo yanaleta mabadiliko makubwa kwenye usafiri na maisha ya watu, kusafirisha bidhaa na mazao, pamoja na kuharakisha maendeleo maeneo mbalimbali hasa vijijini.

Barabara husaidia kuunganisha eneo na eneo kwa kuwezesha ukuaji wa uwekezaji na shughuli za kiuchumi ambazo ni muhimu kwa maeneo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Kasi ya ujenzi wa miundombinu inasaidia kufungua fursa za kiuchumi zaidi kwa wananchi, huku serikali ikipata kodi, watu wake kuajiri na kuajiriwa pamoja na manufaa mengi ya ukuaji wa miji na majiji, pamoja na kufunguliwa kwa miji mingi.

Daraja kama hili ni muhimu likajengwa upya, lakini kwa ubora unaotakiwa kwamba kila miundombinu thamani ya fedha ionekane, kama tunavyoona yapo madaraja aliyodumu kwa zaidi ya miaka 40, basi miundombinu yoyote ikijengwa sasa iwe ya kudumu itumiwa na kizazi cha sasa na kijacho.

Wakati mwingine tunaona baadhi ya barabara zilizojengwa ndani ya miezi sita zinaanza kufanyiwa ukarabati, ukifuatilia kwa kina inaelezwa ni rushwa kwa kupunguza vipimo ili baadhi  ya watumishi wasio na uchungu na nchi kujipatia fedha binafsi.

Kwamba wapo ambao hupunguza upana na unene wa barabara au madaraja ili kuhakikisha wanapata fedha, wakati mwingine lawama huelekezwa kwa makandarasi, lakini uhalisia waliompa zabuni wanajua nini kimefanyika.

Ni muhimu kutanguliza utaifa na utu mbele katika kutumia fedha ya umma, ili Watanzania waone thamani ya kodi wanazotozwa.