Walinda usalama viwanjani acheni vipigo kwa mashabiki

27Dec 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Walinda usalama viwanjani acheni vipigo kwa mashabiki

MOJA kati ya matukio yaliyowashangaza wengi kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya KMC na Simba, iliyopigwa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, ni mlinda usalama kumpiga mateke shabiki mmoja aliyevuka eneo la kukaa mashabiki kwenda kutaka kushangilia bao la nne pamoja na ...

wachezaji.

Ilikuwa ni baada ya Kibu Denis kufunga bao la nne, na kisha mshambuliaji huyo kukimbilia sehemu ambayo ina mashabiki wengi wa Simba kushangilia karibu yao, lakini kutokana na furaha iliyopitiliza, mashabiki wawili waliruka chini kutoka jukwaani walipokuwa wamekaa na kisha kuwafuata wachezaji kushangilia pamoja.

Lakini kilichotokea hapo ni kipigo alichokipata mmoja wao aliyekuwa amevaa jezi ya Simba, na aliyebaki ilibidi arejee alikotoka kwa kuhofu yasije kumkuta kama mwenzake.

Kamwe, hatuwezi kuwa sehemu ya kuhamasishi mashabiki wa soka kuingia uwanjani wakati mechi ikiendelea, au bao linapofungwa, kwa sababu hairuhusiwi kufanya hivyo, na ni kitu ambacho hakikubaliki, ndiyo maana kwenye viwanja vyote duniani kumekuwa na walinzi wanaofanya kazi hiyo ya kuwalinda wachezaji wasivamiwe na mtu yeyote yule ili soka lichezwe bila bughudha yoyote.

Pamoja na hayo duniani kote matukio ya mashabiki au wanyama kuvamia uwanja haviepukiki uwanjani, na huwa vinatokea, ingawa kwa nadra sana. Hata hivyo, tumekuwa tukishuhudia namna wenzetu kwenye michuano mbalimbali barani Ulaya tukio kama hilo likitokea, walinzi kazi yao inakuwa kumkimbilia mhusika huyo na kumkamata kisha kumtoa bila kumuadhibu na mechi kuendelea.

Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) liliamua watu wanaolinda usalama viwanjani wasiwe askari polisi au mgambo, badala yake ni walinzi maalum ambao wamepata mafunzo kutoka kwenye vyama vya soka na si vinginevyo, hivyo kilichotokea Ijumaa iliyopita tunaamini Shirikisho la Soka nchini (TFF), sasa litakifanyia kazi kwa kuwakumbusha walinda usalama kutotoa vipigo vikali kwa mashabiki wa soka mithili ya mbwa mwizi.

Aliyekuwa anampiga shabiki yule alimchukulia kama mhalifu na si shabiki wa soka aliyekumbwa na mhemko tu kutokana na timu yake kupata ushindi. Alichopaswa kufanya mlinzi yule ni kumkamata na kumrudisha alikotoka kwa sababu yule ni mteja na si mhalifu.

Zama za kuwachukulia wanaokwenda mpirani kuwa ni mashabiki tu wa soka badala ya wateja kama zilivyo biashara zingine zozote zimekwisha, hivyo huu ni wakati wakuwalinda na kuwaheshimu hasa inapoaminika hana dhamira mbaya ya kuhatarisha usalama.

TFF na klabu zinatumia gharama kubwa kuhamasisha mashabiki kwenda viwanjani ili kunufaika kimapato, lakini kama itaanza kuonekana au kuzoeleka kuwa shabiki anapopandwa na mzuka anafanyiwa kama yale aliyoyafanya kijana huyo kwenye mechi ya KMC FC dhidi ya Simba, basi watazidi kupungua uwanjani kila uchao.

Haikuhitaji kuwa na shahada ya sayansi ya roketi ('bachelor degree in rocket science) ili kumtambua kwamba shabiki yule hakuwa hatari au na athari yoyote ile. Kwanza alikuwa amevaa jezi ya Simba kwa hiyo isingewezekana kwamba anakwenda kuwadhuru wachezaji wao, hivyo angeweza kudhibitiwa kwa urahisi na kurudishwa alikotoka bila kupigwa.

Hivyo tunakemea vikali matumizi makubwa ya nguvu na vipigo kwa mashabiki kutoka kwa walinda usalama viwanjani.