Poulsen apewe muda, maandalizi Stars michuano ijayo yakianza sasa

15Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Poulsen apewe muda, maandalizi Stars michuano ijayo yakianza sasa

NI rasmi sasa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeaga michuano ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar na mechi ya jana dhidi ya Madagascar ilikuwa ya kukamilisha ratiba tu.

DR Congo ambayo ilikuwa nyumbani ikihitaji ushindi dhidi ya Benin ili kufuzu, ndiyo iliyohitimisha ndoto za Tanzania kusonga mbele katika michuano hiyo baada ya Alhamisi iliyopita kuichapa mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kama Stars ingeshinda mechi hiyo, mchezo dhidi ya Madagascar ungekuwa na maana kubwa kwao, lakini haikuwa hivyo na kuiachia nafasi Benin na DR Congo mechi yao jana kuamua timu itakayotinga kumi bora kutafuta tano zitakazoliwakilisha Bara la Afrika kwenye fainali hizo mwakani.

Kwa ujumla, kazi iliyofanywa na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen, ni ya kupongezwa hasa tukizingatia timu alizokutana nazo kwenye michuano hiyo zilisheheni nyota wengi wanaocheza soka la kulipwa Ulaya na Asia huku wachezaji wanaocheza soka la kulipwa kwa Stars wakiwa ni watatu tu.

Kwa kuzingatia hilo, Nipashe tunaona kuna kila sababu ya kumpongeza Poulsen kwa kutufikisha hapo, kwa Stars kumaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi lake la J.

Kikubwa sasa ni Shirikisho la Soka nchini (TFF) kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuanza kuiandaa Taifa Stars kwa michuano ijayo hususan ni ya Mataifa ya Afrika (Afcon), Wachezaji wanocheza Soka la Ndani (CHAN) na Kombe la Dunia 2026.

Tunatoa rai hiyo kutokana na kutambua tayari wapo baadhi ya wadau wa soka na mashabiki wameanza kumnyooshea vidole Poulsen wakimbebesha lawama kibao huku wakitaka atimuliwe, hivyo TFF haina budi kuwapuuza na kuendelea kumpa sapoti ya kutosha Poulsen kwa kuwa anaweza kutufikisha 'Kanani' ya soka kama ushirikiano ukiwapo.

Sisi tunaamini kama Poulsen atapewa muda zaidi na ushirikiano wa kutosha kwa kuwezeshwa kufuatilia baadhi ya wachezaji wa Tanzania wanaocheza nje ya nchi, michuano ijayo iwe ya CHAN, Afcon hata Kombe la Dunia, Tanzania inaweza kufuzu na kufika mbali zaidi.

Lakini kwa wanaomnyooshea vidole Poulsen ni vema sasa wakageukia soka letu la ndani kwa kuhakikisha linazidi kuwa bora ili viwango vya wachezaji wetu vizidi kuimarika na kwenda kuwa msaada kwa timu ya taifa.

Kwa kufanya hivyo, pia wachezaji wetu wataonekana na kusajiliwa klabu kubwa za nje na baadaye kuwa msaada mkubwa kwa Taifa Stars kwenye michuano ijayo.

Lakini kama tutaendelea kutumia ujanja ujanja kwa kutaka timu zetu kwenye ligi ya ndani kupata matokeo kwa kununua mechi ama kubebwa na waamuzi, badala ya wachezaji kuonyesha ubora wao uwanjani, kilio hichi kwa makocha wa timu ya taifa hakitakoma.

Ni vema kila mmoja kutambua soka halina njia ya mkato na matokeo ya kijanjajanja katika michuano yetu ya ndani hayatasaidia kukua kwa viwango vya wachezaji wetu hasa tukizingatia wachezaji wengi wa Taifa Stars wanacheza soka la ndani.

Hivyo, tuzidi kuiboresha ligi yetu ya ndani huku baadhi ya wachezaji ambao timu zao zina makocha wakigeni wakizingatia vema wanachofundishwa, lakini TFF ikiona umuhimu wa kutoa nafasi zaidi kwa nyota wa kigeni kuja kucheza soka nchini ili kutoa changamoto kwa wazawa ambao nafasi yao ya kutoka kwenda kucheza soka nje imekuwa finyu kutokana na ubora wao kuwa chini.

Matarajio yetu ni kuona kila mmoja akitoa mawazo chanya ya nini cha kufanya kuiboresha Taifa Stars kuelekea michuano mingine ijayo, badala ya kuanza kutaka kumbebesha lawama Poulsen kwa timu hiyo kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.