Ziara ya Sanjay Dutt ilete mageuzi tasnia ya filamu

13Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ziara ya Sanjay Dutt ilete mageuzi tasnia ya filamu

KAZI iendelee, hii kauli inatakiwa iendelee kuzunguka na kuonekana kwa vitendo kwenye vichwa vya Watanzania wote ili kuhakikisha ndoto zetu zinatimia.

Kama ambavyo kwa upande wa mchezo wa mpira wa miguu, ndoto kubwa ya kila taifa ni kuona wanataka tiketi ya kushiriki katika mashindano makubwa ambayo si mengine bali ni fainali za Kombe la Dunia.

Fainali hizo kuchezwa kila baada ya miaka minne, lakini hutanguliwa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ambazo pia hujumuisha timu zilizo imara kutoka kwenye bara letu.

Wachezaji huandaliwa na nchi huweka mikakati ili kufikia ndoto hizo, lakini kuna wakati suala la bahati huchukua nafasi yake licha ya kila nchi kufanya maandalizi yaliyo bora na vikosi vyake kuundwa na wachezaji nyota.

Tukirudi katika upande wa sanaa ya filamu nchini, mapema wiki hii taifa lilipokea msanii mkongwe wa filamu, Sanjay Dutt ambaye ni raia wa India.

Tunaamini ziara ya mwigizaji huyo mkongwe haukuja kwa bahati mbaya, ujio wake unatakiwa kutumika kama sehemu ya darasa la kuwafundisha wasanii wetu kutoka hapa walipo na kufika kwenye daraja lingine.

Umefika wakati wasanii wa filamu Tanzania wakaamka na kutengeneza kazi ambazo zitalenga soko la kimataifa na hilo linawezekana kama watakubali kuwekeza katika kiwango cha juu.

Bila ya uwekezaji imara na wa kiwango kikubwa lakini wenye malengo, wasanii wa filamu wa hapa nchini wataendelea kuwa wasindikizaji kwenye tasnia hiyo inayotengeneza idadi kubwa ya ajira kwa watu wa rika mbalimbali.

Wasanii wanatakiwa wafahamu kuandaa kazi zenye ubora ndio zitapelekea kupata matunda mazuri sokoni na kufanya kazi kwa kuripua, watajiweka katika nafazi za chini na baadhi yao huweza kuichukia sanaa hiyo kutokana na kushindwa kumudu gharama za kujiendesha.

Dutt ambaye alipata nafasi ya kuonana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameahidi kushirikiana na wasanii wa Tanzania katika kuleta mapinduzi ya kazi wanazozifanya ili zitambulike kimataifa.

Kupitia kwa mafanikio ambayo ameyapata msanii huyo mkongwe, hata wasanii na wadau wa tasnia ya filamu wa hapa nchini wanaweza kufikia ndoto zao endapo watafanya kazi zao kwa weledi na kuacha kuiona tasnia hiyo ni sehemu ya kupatia umaarufu.

Inafahami wazi kazi ya sanaa 'inalipa' na kama hilo ni kweli, basi wasanii wetu ambao walipata nafasi ya kuzungumza na mkongwe huyo kufanya mabadliko kwenye kazi zao na hatimaye tutashuhudia filamu zilizotengenezwa na kuandaliwa na wasanii wetu zikishinda tuzo mbalimbali za kimataifa.

Tuzo hizo haziendi bure, zitaenda sambamba na soko la dunia na hatimaye pia jina la nchi litapata heshima kupitia kazi za wasanii hao kama ambavyo wanataaluma wengine wamekuwa wakipeperusha vyema bendera ya nchi kupitia vipaji walivyonavyo.

Hakuna kinachoshindikana, kikubwa ni wadau wa tasnia ya filamu kukubali kwenda na kasi ya ushindani iliyopo katika dunia hii ya kidijitali.