Kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu kuanza, huchezwa mechi ya Ngao ya Jamii, ambayo humkutanisha bingwa wa Ligi Kuu na wa Kombe la Shirikisho (FA Cup), hivyo miamba hiyo miwili ilikutana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na Yanga kuibuka kidedea baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 likifungwa na Fiston Mayele.
Simba ilipata nafasi hiyo ya kucheza mechi ya Ngao ya Jamii baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, hivyo kucheza na Yanga ambayo fursa hiyo iliiangukia kwao kutokana na kufika fainali ya FA Cup msimu uliomalizika.
Hivyo, pazia la Ligi Kuu 2021/22, leo litafunguliwa kwa kuchezwa mechi tatu katika viwanja tofauti ambapo mjini Morogoro, Mtibwa Sugar itaikaribisha Mbeya Kwanza FC mchezo ukipigwa Uwanja wa Jamhuri wakati Namungo FC ikiwa mwenyeji wa Geita Gold FC katika Dimba la Ilulu mkoani Lindi na Azam FC ikikabiliana na Coastal Union ugenini katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa kupigwa michezo mingine mitatu ambapo Dodoma Jiji itaikaribisha Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wakati Mbeya City ikiwa mwenyeji wa Tanzania Prisons katika Dimba la Sokoine jijini Mbeya huku mabingwa wa ligi hiyo, Simba wakiwa wageni wa Biashara United katika Uwanja wa Karume mjini Musoma.
Michezo ya kwanza ya raundi hiyo ya kwanza kwa kila timu itakamilika Jumatano kwa Polisi Tanzania FC kuikaribisha KMC FC katika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi na Kagera Sugar kuwa wenyeji wa Yanga katika Dimba la Kaitaba mjini Bukoba.
Kwa ujumla msimu huu unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa zaidi ya misimu iliyopita hasa kutokana na kiasi kikubwa cha udhamini kilichowekwa kwenye haki za matangazo ya televisheni baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Kampuni ya Azam Media Limited Mei, mwaka huu kuingia mkataba wenye thamani ya Sh. bilioni 225.6 kwa kipindi cha miaka 10.
Katika mkataba huo ambao mgao wa fedha kwa kila klabu unatakiwa kuelekezwa kwenye mishahara ya wachezaji, kutakuwa na bonasi kuanzia klabu itakayotwaa ubingwa hadi itakayoburuza mkia, ambapo bingwa atazawadiwa Sh. milioni 500, mshindi wa pili milioni 250, watatu milioni 225, wa nne milioni 200 na zitakwenda zikipungua hadi timu ya mwisho na zile zitakazocheza mechi ya mtoano zikilamba milioni 20 kila moja.
Kiasi hicho ni mbali ya fedha zitakazotolewa na wadhamini wenza pamoja mdhamini mkuu wa ligi hiyo ambaye kwa mujibu wa Bodi ya Ligi nchini (TPLB), mazungumzo yamefikia pazuri na anatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Hivyo, ongezeko hilo la fungu ni wazi haitakuwa ligi ya lelemama, kwani tayari timu zote zimeonyesha kudhamiria kufanya vizuri kutokana na aina ya usajili uliofanywa kwa klabu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu. Kwa mantiki hiyo, hatutarajii kuona waamuzi wakiwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa baadhi ya klabu kwa kutozitenda haki kwa kufinyanga sheria 17 zinazoongoza mchezo huo duniani.
Tunataka kuona kila timu ikipata matokeo kutokana na uwezo wake uwanjani na si kubebwa na waamuzi kutokana na mapenzi au ushabiki wao kwa baadhi ya klabu, kupewa rushwa ama vinginevyo.
Waamuzi hawana budi kutambua klabu hizi zimewekeza jasho, nguvu kubwa na fedha katika suala zima la uendeshaji, hivyo Nipashe tunataka haki ikitendeka ndani na nje ya uwanja na si tu kutendeka bali ionekane ikitendeka kweli na ifahamike mapema kwamba hatutafumbia macho hata kidogo kwa mwamuzi ama yeyote yule mwenye dhamira mbaya ya kutaka kufinyanga matokeo kwa nia yake ovu.