Sababu hiyo na nyingine kadhaa, ndizo zinazodaiwa kulalamikiwa na wananchi mbalimbali kutokana na kutoa huduma duni, ambazo hazilingani na mahitaji ya wateja.
Hata hivyo, Waziri wa Nishati January Makamba, anaahidi kuwa chini ya uongozi mpya wa shirika hilo ulioteuliwa hivi karibuni, hakutakuwa na maamuzi ya kisiasa au misukumo ya kisiasa katika uendeshaji wa shirika hilo.
Kwa kauli hiyo, tunaona kwamba sasa serikali imedhamiria kwa dhati kufufua shirika hilo ili litoe huduma kikamilifu, hivyo tunaamini kwamba kuwapo kwa utashi wa kisiasa kunaweza kusaidia shirika kusimama imara.
Sisi tunaamini kwamba kuwapo kwa utashi wa kisiasa kunaweza kusaidia shirika hilo kufanya kazi likiwa huru badala ya kuingiliwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao binafsi na kujikuta likishindwa kujiendesha inavyotakiwa. Wanasiasa wanapoingilia shirika wanaweza kulisababisha hasara na kulifanya lishindwe kutoa huduma inayotakiwa, hivyo kuwafanya wateja na wananchi kwa ujumla kuliona kama halina umuhimu kwao.
Kila mara tumekuwa tukisikia kwenye vyombo vya habari malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusu huduma duni za shirika hilo na hata lugha mbovu kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi dhidi ya wateja wao.
Kadhalika, kumekuwapo malalamiko ya wananchi dhidi ya wafanyakazi kadhaa wa shirika ya kuwadai rushwa ili wapatiwe huduma hususan za kufungiwa umeme.
Hivyo kwa kauli hiyo ya Waziri Makamba kukiri kuwapo kwa upungufu na kuahidi kuyafanyia kazi, tunaona ni nafasi nzuri sasa kuchana shirika hilo lijiendeshe na kutoa huduma inavyotakiwa bila kuingiliwa na wanasiasa.
Tunaichukulia kauli hiyo kuwa huenda ikaleta mabadiliko makubwa kwenye utendaji kuanzia bodi, uongozi na hata mfanyakazi mmoja mmoja ili Watanzania waweze kuhudumiwa bila kikwazo.
Kumekuwapo na mkakati wa kutaka kuzalisha umeme mwingi wa kuuza nje ya nchi kwa megawati 2,100 kupitia mradi wa bwawa la Nyerere, hivyo ushauri wetu ni kwamba utashi wa kisiasa uachwe uchukue nafasi yake ili kufanikisha mikakati yote ya kuwa na nishati ya kutosha.
Tunaamini kwamba utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kugharimu fedha nyingi za wananchi takribani Sh. trilioni 7 usijaribu kuingiliwa na wanasiasa kwa maslahi yao, ili nchi ijitosheleze kwa nishati ya umeme pamoja na kuuza ziara nje ya nchi.
Kuwapo kwa maamuzi ya kisiasa katika uendeshaji wa shirika kunaweza kuwa na athari mbaya kwa kuwa taratibu za uendeshaji hazitafuatwa, badala yake malengo ya wanasiasa ndiyo yatazingatiwa.
Ikumbukwe kwamba maamuzi mabaya yakiwamo ya kisiasa ndiyo yaliyoifikisha TANESCO hapa ilipo ikiwamo mikataba mibovu, ambayo imeisababishia nchi hasara kubwa.
Kimsingi hilo likizingatiwa na kila upande ukatimiza wajibu, nchi inaweza kuwa na umeme wa kutosha hata kuuza nje ya nchi, na pia malalamiko kutoka kwa wateja yatapungua kutokana na huduma bora.
Kwa kuwa waziri anataka shirika hilo kibiashara, nasi tunashauri uwapo wa utashi wa kisiasa ili lengo hilo liweze kutimia, kwani huduma zinaweza kuboreshwa na kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wateja.










