Hao ni wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa wilaya, ambao wajibu wao ni kusimamia shughuli za maendeleo pamoja na kuwatatulia wananchi vikwazo na kero zinazowakabili.
Kwa kuliona tatizo hilo, Rais Samia Suluhu Hassan, ameeleza kukerwa na ugomvi kwa watumishi wa umma wakiwamo wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri na kuahidi kuwa hatozungumza kitu bali kalamu yake ndiyo itakayozungumza.
Alitoa kauli hiyo juzi jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu maalum wa uchaguzi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), na kwamba amekuwa akishangazwa na namna ambavyo viongozi wa umma aliowateua kwenda kumwakilisha wakiacha majukumu yao na kufanya mambo yenye maslahi yao binafsi.
Alisema uongozi wa juu unawaona wanavyolumbana badala ya kutatua kero za wananchi ambazo ndizo zimewaweka katika nafasi walizonazo sasa.
Aidha, alisema kutokana na ugomvi huo maeneo hayo yamekosa maendeleo na kuwafanya wananchi kuendelea kupata shida ya huduma mbalimbali za jamii ikiwamo afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Kauli ya Rais Samia kuhusu utendaji usioridhisha wa viongozi wengi ngazi ya wilaya ni mwendelezo wa kauli zilizowahi kutolewa na viongozi wakuu wa nchi waliomtangulia.
Hali hiyo ndiyo imekuwa ikisababisha wananchi kuvamia misafara ya viongozi wakuu wa taifa wanapokwenda vijijini wakati mwingine wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa maneno kuhusu kero zinazowakabili.
Kwa kuamua kufanya hivyo, tafsiri yake ni kwamba viongozi walioko kwenye maeneo hayo hawaendi kwa wananchi kusikiliza matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi. Huo sio uwajibikaji.
Haiwezekani Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu waende wilaya zote nchini kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi, hivyo ndiyo maana kukawapo na wawakilishi wao kuanzia mikoa hadi wilaya kwa ajili ya kutekeleza majukumu hayo.
Rais alisema maslahi binafsi ndicho chanzo cha migongano baina ya viongozi hao ya kutaka kutumia vibaya fedha za maendeleo zinazotumwa na serikali katika halmashauri husika.
Viongozi wa aina hiyo waliokula kiapo cha maadili hawapaswi kuwapo katika utumishi wa umma, kwa sababu wanaiharibu taswira ya serikali kwa wananchi, hivyo suluhisho ni kuwaondoa na kuweka wanaoweza kutanguliza maslahi ya umma.
Tunakubaliana na alichokisema Rais Samia kwa kuwa ndicho kinachoshuhudiwa katika maeneo kadhaa nchini, kutokana na wananchi kukimbilia kutoa kero zao za maji, afya, elimu, barabara, ardhi na mambo mengine madogo ambayo yanaweza kutatuliwa na viongozi wao.
Tunaona njia pekee ya kuwafanya viongozi wawajibike kwa utumishi wa wananchi ni kuwapangia malengo ambayo ni kuzisikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati mwafaka.
Wale ambao wataendeleza malumbano na kufanyakazi kwa mazoea bila kuleta matokeo, ni sahihi Rais Samia atumie kalamu yake kuwafuta kazi badala ya kuwapigia kelele na kuwafokea kila wakati kuwakumbusha wajibu wao.










